Mawasiliano Na Mchumba Baada Kuposa Na Kabla Ya Ndoa
SWALI:
INARUHUSIWA KUWASILIANA MARA KWA MARA NA MCHUMBA WAKO? KWA SIMU AMA BARUA AMA E-MAIL?
JIBU:
Sifa zote njema Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allahu 'anhum jamiy'an) na watangu wema mpaka Siku ya Qiyaamah.
Ama kuhusu kuwasiliana baina ya mvulana aliyeposa na posa yake kukubaliwa na msichana na walii wake basi hakuna tatizo lolote ikiwa mawasiliano yao ni katika mipaka ya kishariy'ah na mbele ya Mahaarim.
Wanachuoni wanaonelea mawasiliano baina ya wachumba kwa simu au kwa njia nyingine za faragha zozote zile hayaruhusiwi. Yote ni katika kuepusha fitnah na Shaytwaan kuingia baina yao kabla ya ndoa.
Mara nyingi mawasiliano ya karibu kabla ya ndoa, yameleta uharibifu mkubwa na madhara katika jamii na kusababisha posa nyingi kuharibika na hata watu kutumbukia katika zinaa.
Mbali na mawasiliano hayo mvulana anaweza kwenda nyumbani kwa mchumba wake bora tu wasikae faragha wao peke yao katika mazungumzo. Inabidi awe pamoja nao Mahaarim wa msichana. Hii ni kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Hakai faragha mwanamume na mwanamke ila wa tatu wao ni Shaytwaan. Na hakika Shaytwaan hutembea katika mwili wa mwana Aadam kama itembeavyo damu”.
Hii ni kuwa bado nyinyi hamjakuwa mume na mke, na mmoja kati yenu anaweza kuvunja ndoa hiyo baada ya kuwa mmekubaliana hapo awali. Mwanamume anaweza kusema basi hataki tena harusi au mwanamke vilevile kuamua kuwa hakuna tena harusi, na baya zaidi ni uwezekano wa kutokea maovu katika kipindi hicho.
Ile desturi ya wachumba kuwa wanakwenda pamoja katika mabustani, sinema au kusafiri kabla ya kuoana si desturi ya Kiislamu, japo kuna nchi nyingi za Waislamu wanafanya hivyo.
Na Allaah Anajua zaidi