013-Lu-ulu-un-Manthuwrun: Atakayepitiwa Na Usingizi Bila Kusoma Nyiradi Zake Alipize Kabla Adhuhuri
Lu-ulu-un-Manthuwrun
(Mkusanyiko Wa Hadiyth Mbali Mbali Na Mafunzo Yake)
Hadiyth Ya 13
Atakayepitiwa Na Usingizi Bila Ya Kusoma Nyiradi Zake Alipize Kabla Ya Adhuhuri
عَنْ عُمَرَ بْنَ الْخَطَّابِ (رضي الله عنه) يَقُولُ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه و آله وسلم): ((مَنْ نَامَ عَنْ حِزْبِهِ أَوْ عَنْ شَيْءٍ مِنْهُ فَقَرَأَهُ فِيمَا بَيْنَ صَلاَةِ الْفَجْرِ وَصَلاَةِ الظُّهْرِ كُتِبَ لَهُ كَأَنَّمَا قَرَأَهُ مِنْ اللَّيْلِ)) رواه مسلم
Imepokelewa kutoka kwa ‘Umar bin Al-Khattwaab (رضي الله عنه) amesema: Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Atakayelala na kupitiwa na hizbu yake [nyiradi zake] au chochote kutoka humo kisha akaisoma baina ya Swalaah ya Alfajiri na Swalaah ya Adhuhuri, ataandikiwa kama kwamba ameisoma usiku)) [Muslim]
Mafunzo Na Mwongozo:
1. Umuhimu wa Muislamu kuhifadhi na kuendeleza nyiradi zake kila siku.
2. Anayepitwa na nyiradi zake, akimbilie kuzisoma nyakati zilotajwa katika Hadiyth ili apate fadhila zake kamilifu. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَهُوَ الَّذِي جَعَلَ اللَّيْلَ وَالنَّهَارَ خِلْفَةً لِّمَنْ أَرَادَ أَن يَذَّكَّرَ أَوْ أَرَادَ شُكُورًا ﴿٦٢﴾
Naye Ndiye Aliyejaalia usiku na mchana ufuatane kwa atakaye kukumbuka au atakaye kushukuru. [Al-Furqaan (26: 62)]
3. Rahma ya Allaah (سبحانه وتعالى) kwa waja Wake kuwalipa thawabu wakati wanaposhindwa kupata wasaa au wanapokalifika na jambo kama ugonjwa n.k. Rejea: Al-Baqarah (2: 286)
Pia Hadiyth: Imepokelewa kutoka kwa Anas (رضي الله عنه) kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:
((إِذَا ابْتَلَى اللَّهُ الْعَبْدَ الْمُسْلِمَ بِبَلَاءٍ فِي جَسَدِهِ قَالَ اللَّهُ لِلْمَلَكِ: اكْتُبْ لَهُ صَالِحَ عَمَلِهِ الَّذِي كَانَ يَعْمَلُ فَإِنْ شَفَاهُ غَسَلَهُ وَطَهَّرَهُ وَإِنْ قَبَضَهُ غَفَرَ لَهُ وَرَحِمَهُ))
((Allaah Akimjaribu mja Muislamu kwa kumpa mtihani katika mwili wake, Humwambia Malaika: “Mwandikie ‘amali zake njema alizokuwa akizitenda”. Akimpa shifaa [Akimponyesha] Humwosha na kumtakasa, na Akichukua roho yake, Humghufuria na Akamrehemu)) [Ahmad katika Musnad na amesema Al-Albaaniy: Hadiyth Hasan Swahiyh]
4. Rahmah ya Allaah (سبحانه وتعالى) na Uadilifu Wake kwamba Anatambua hali za waja Wake kushughulishwa na mambo kadhaa ya dunia yao na Aakhirah yao, Akawaamrisha wapunguze ‘ibaadah zao kama vile kusoma Qur-aan. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
إِنَّ رَبَّكَ يَعْلَمُ أَنَّكَ تَقُومُ أَدْنَىٰ مِن ثُلُثَيِ اللَّيْلِ وَنِصْفَهُ وَثُلُثَهُ وَطَائِفَةٌ مِّنَ الَّذِينَ مَعَكَ ۚ وَاللَّـهُ يُقَدِّرُ اللَّيْلَ وَالنَّهَارَ ۚ عَلِمَ أَن لَّن تُحْصُوهُ فَتَابَ عَلَيْكُمْ ۖ فَاقْرَءُوا مَا تَيَسَّرَ مِنَ الْقُرْآنِ ۚ عَلِمَ أَن سَيَكُونُ مِنكُم مَّرْضَىٰ ۙ وَآخَرُونَ يَضْرِبُونَ فِي الْأَرْضِ يَبْتَغُونَ مِن فَضْلِ اللَّـهِ ۙ وَآخَرُونَ يُقَاتِلُونَ فِي سَبِيلِ اللَّـهِ ۖ فَاقْرَءُوا مَا تَيَسَّرَ مِنْهُ ۚ وَأَقِيمُوا الصَّلَاةَ وَآتُوا الزَّكَاةَ وَأَقْرِضُوا اللَّـهَ قَرْضًا حَسَنًا ۚ وَمَا تُقَدِّمُوا لِأَنفُسِكُم مِّنْ خَيْرٍ تَجِدُوهُ عِندَ اللَّـهِ هُوَ خَيْرًا وَأَعْظَمَ أَجْرًا ۚ وَاسْتَغْفِرُوا اللَّـهَ ۖ إِنَّ اللَّـهَ غَفُورٌ رَّحِيمٌ﴿٢٠﴾
Hakika Rabb wako (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) Anajua kwamba unasimama (kuswali) karibu na thuluthi mbili za usiku au nusu yake, au thuluthi yake; na kundi miongoni mwa wale walio pamoja nawe. Na Allaah Anakadiria usiku na mchana. Anajua kwamba hamuwezi kuukadiria wakati wake na kusimama kuswali, basi Amepokea tawbah yenu. Basi someni kile kilicho chepesi katika Qur-aan. (Allaah) Anajua kwamba watakuweko miongoni mwenu wagonjwa, na wengine wanasafiri katika ardhi wanatafuta fadhila za Allaah, na wengineo wanapigana katika njia ya Allaah. Basi someni kile kilicho chepesi humo. Na simamisheni Swalaah, na toeni Zakaah, na mkopesheni Allaah karadhi nzuri. Na chochote kile cha kheri mnachokadimisha kwa ajili ya nafsi zenu, mtakikuta kwa Allaah. Ni bora, na ujira mkubwa zaidi. Na muombeni Allaah maghfirah, hakika Allaah ni Mwingi wa kughufuria, Mwenye kurehemu. [Al-Muzzammil (73: 20)]
Rejea pia Hadiyth namba (12).
5. Asiitegemee mtu Hadiyth hii kwa kutokujihimiza kuamka usiku kufanya ‘Ibaadah, bali ajitahidi kila njia kujiwezesha kuamka kupata fadhila za Qiyaamul-Layl (Kisimamo cha usiku kwa ajili ya kuswali):
Rejea: As-Sajdah (32: 16-17), Al-Israa (17: 79), Adh-Dhaariyaat (51: 15-18), Al-Muzzammil (73: 2-8).
6. Kuna fadhila tukufu za nyiradi na ‘amali za usiku, hivyo inatakiwa mja ajipinde katika kuzitekeleza.
7. Kuchuma fadhila za nyakati baina ya Alfajiri na Adhuhuri kwa kuleta nyiradi alizokosa mja yeyote yule.