014-Lu-ulu-un-Manthuwrun: Kuzishikilia Sunnah Kwa Magego Ili Kubakia Imara Na Kujiepusha Ikhtilaaf

Lu-ulu-un-Manthuwrun

(Mkusanyiko Wa Hadiyth Mbali Mbali Na Mafunzo Yake)

Hadiyth Ya 14  

Kuzishikilia Sunnah Kwa Magego Ili Kubakia Imara Na Kujiepusha Na Ikhtilaaf

www.alhidaaya.com

 

عن أبي نَجِيح الْعِرْبَاضُ  بن سارية (رضي الله عنه) قال: وَعَظَنَا رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه و آله وسلم) مَوْعِظَةً بَلِيغَةً وَجِلَتْ مِنْهَا الْقُلُوبُ  وَذَرَفَتْ مِنْهَا الْعُيُونُ. فَقُلْنَا:  يَا رَسُولَ اللَّهِ كَأَنَّها مَوْعِظَةُ مُوَدِّعٍ فأوْصِنا. فَقَالَ: ((أُوصِيكُمْ بِتَقْوَى اللَّهِ وَالسَّمْعِ وَالطَّاعَةِ وَإِنْ تأَمَّرَ عَلَيْكُم عَبْدٌ حَبَشِيّ ، وَأَنَّهُ مَنْ يَعِشْ مِنْكُمْ فَسَيَرَى اخْتِلاَفًا كَثِيرًا ، فَعَلَيْكُمْ بِسُنَّتِي وَسُنَّةِ الْخُلَفَاءِ الرَّاشِدِينَ الْمَهْدِيِّينَ ، عَضُّوا عَلَيْهَا بِالنَّوَاجِذِ وَإِيَّاكُمْ وَمُحْدَثَاتِ الأُمُورِ فَإِنَّ كُلَّ بِدْعَةٌ ضَلاَلَةٌ)) رواه أبو داوود والترمذي وقال حديث حسن صحيح

 

Imepokelewa kutoka kwa Abuu Najiyh Al-‘Irbaadhw bin Saariyah (رضي الله عنه) amesema: Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alitupa mawaidha mazito (yenye maana kubwa), nyoyo zikaogopa na macho yakabubujikwa machozi. Tukasema: Ee Rasuli wa Allaah! Yanaonekana kama kwamba mawaidha ya kutuaga, basi tuusie.  Akasema: ((Nakuusieni kuwa na taqwa ya Allaah na kusikiliza na kutii japokuwa mtaongozwa na mtumwa Mhabashi. Hakika atakayeishi umri mrefu miongoni mwenu ataona ikhtilaaf nyingi. Kwa hiyo, shikamaneni na Sunnah zangu na mwenendo wa Makhalifa waongofu, yashikilieni kwa magego [mambo yao]. Na tahadharini na mambo yenye kuzushwa, kwani kila uzushi ni upotovu)) [Abuu Daawuwd, At-Tirmidhiy, na amesema: Hadiyth Hasan Swahiyh].

 

 

Mafunzo Na Mwongozo:

 

 

1.Wajibu wa kumcha Allaah (سبحانه وتعالى) kwa kufuata maamrisho na makatazo Yake kama Anavyosema:

 

قُلْ أَطِيعُوا اللَّـهَ وَأَطِيعُوا الرَّسُولَ ۖ فَإِن تَوَلَّوْا فَإِنَّمَا عَلَيْهِ مَا حُمِّلَ وَعَلَيْكُم مَّا حُمِّلْتُمْ ۖ وَإِن تُطِيعُوهُ تَهْتَدُوا ۚ وَمَا عَلَى الرَّسُولِ إِلَّا الْبَلَاغُ الْمُبِينُ ﴿٥٤﴾

Sema: “Mtiini Allaah na mtiini Rasuli.” Mkigeukilia mbali, basi hakika jukumu lake ni lile alobebeshwa tu nanyi ni juu yenu yale mliyobebeshwa. Na mkimtii mtaongoka; na hapana juu ya Rasuli isipokuwa ubalighisho bayana.

 

 

وَعَدَ اللَّـهُ الَّذِينَ آمَنُوا مِنكُمْ وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ لَيَسْتَخْلِفَنَّهُمْ فِي الْأَرْضِ كَمَا اسْتَخْلَفَ الَّذِينَ مِن قَبْلِهِمْ وَلَيُمَكِّنَنَّ لَهُمْ دِينَهُمُ الَّذِي ارْتَضَىٰ لَهُمْ وَلَيُبَدِّلَنَّهُم مِّن بَعْدِ خَوْفِهِمْ أَمْنًا ۚ يَعْبُدُونَنِي لَا يُشْرِكُونَ بِي شَيْئًا ۚ وَمَن كَفَرَ بَعْدَ ذَٰلِكَ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْفَاسِقُونَ ﴿٥٥﴾

Allaah Amewaahidi wale walioamini miongoni mwenu na wakatenda mema kwamba bila shaka Atawafanya makhalifa katika ardhi kama Alivyowafanya makhalifa wale waliokuwa kabla yao, na bila shaka Atawamakinishia Dini yao Aliyowaridhia, na bila shaka Atawabadilishia amani badala ya khofu yao; wawe wananiabudu Mimi wasinishirikishe na chochote; na yeyote yule atakayekufuru baada ya hapo, basi hao ndio mafasiki.

 

وَأَقِيمُوا الصَّلَاةَ وَآتُوا الزَّكَاةَ وَأَطِيعُوا الرَّسُولَ لَعَلَّكُمْ تُرْحَمُونَ ﴿٥٦﴾

Na simamisheni Swalaah, na toeni Zakaah, na mtiini Rasuli ili mpate kurehemewa. [An-Nuwr 24: 54-56)]

 

 

Rejea pia:  Al-Anfaal (8: 46), Al-Ahzaab (33: 70), At-Tawbah (9: 119), Muhammad (47: 33).

 

Na jambo hilo limepatiwa kipaumbele kwa kutajwa mwanzo kwa kuwa umuhimu wake ni mkubwa sana.

 

 

2. Wajibu wa kumtii kiongozi anayeongoza kwa kufuata Shariy’ah japokuwa ni mtu anayeonekana kuwa duni, na inapotokea ikhtilaaf, arudie mtu katika Qur-aan na Sunnah.

 

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا أَطِيعُوا اللَّـهَ وَأَطِيعُوا الرَّسُولَ وَأُولِي الْأَمْرِ مِنكُمْ ۖ فَإِن تَنَازَعْتُمْ فِي شَيْءٍ فَرُدُّوهُ إِلَى اللَّـهِ وَالرَّسُولِ إِن كُنتُمْ تُؤْمِنُونَ بِاللَّـهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ ۚ ذَٰلِكَ خَيْرٌ وَأَحْسَنُ تَأْوِيلًا ﴿٥٩﴾

Enyi walioamini! Mtiini Allaah na mtiini Rasuli na wenye madaraka katika nyinyi. Mkizozana katika jambo basi lirudisheni kwa Allaah na Rasuli mkiwa mnamwamini Allaah na Siku ya Mwisho. Hivyo ni bora na matokeo mazuri zaidi. [An-Nisaa (4: 59)]

 

 

3. Hadiyth hii ni miongoni mwa miujiza ya Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) kubashiria yatakayotokea, kwani zimeshadhihirika ikhtilaaf nyingi baina ya Waislamu.

 

 

4. Kufuata amri za Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) ni dalili ya mapenzi ya Allaah (سبحانه وتعالى) na tahadharisho la kumkhalifu. Rejea: Aal-‘Imraan (3: 31), An-Nuwr (24: 63).

 

 

5. Umuhimu wa kufuata Sunnah za Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) na kuzishikilia bila ya kutoka nje ya mipaka na njia iliyonyooka ikapeleka kufarikiana Waislamu na kujitokeza makundi makundi. Rejea: Al-An’aam (6: 153).

 

Na kila kundi hufurahia watu wake wakijiona kuwa wako katika haki. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

مِنَ الَّذِينَ فَرَّقُوا دِينَهُمْ وَكَانُوا شِيَعًا ۖ كُلُّ حِزْبٍ بِمَا لَدَيْهِمْ فَرِحُونَ ﴿٣٢﴾

 (Wala msiwe) Miongoni mwa wale walioitenganisha dini yao wakawa makundi makundi. Kila kundi wananafurahia waliyonayo.  [Ar-Ruwm (30: 32)]

 

 

 

6. Kufuata Sunnah za Makhalifa Waongofu na kuamini kauli ya Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) kuhusu Sunnah zao khaswa pale inapokuwa ni jambo walilolitenda wao bila ya kutendwa na Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم).

 

 

7.  Kujiepusha kabisa na bid’ah (Uzushi), kwani hatari yake ni upotofu na motoni. [Hadiyth: ((Na kila upotofu unapeleka motoni)) [Muslim]

 

 

8. Vitendo vya bid’ah havina thamani wala havitapokelewa.

 

Rejea Hadiyth namba (15).

 

 

8. Kuonyesha usawa ulioletwa na Uislamu baina ya waja bila kujali tofauti ya ukoo, kabila, utaifa na mwengineo. Ndio tukaamrishwa kumfuata kiongozi mchaji Allaah hata kama ni mtumwa.

 

Rejea: Al-Hujuraat (49: 13)

 

 

9. Utiifu kwa Amiri ni wajibu, maadamu hajakuamrisha jambo la kumuasi Allaah (سبحانه وتعالى) na Rasuli Wake (صلى الله عليه وآله وسلم).

 

 

10. Fadhila za Maswahaba wa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) waliopata hadhi ya kuwa Makhalifa baada ya Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم).

 

 

 

Share