058-Lu-ulu-un-Manthuwrun: Ishi Duniani Kama Mgeni Au Mpita Njia

 

Lu-ulu-un-Manthuwrun

(Mkusanyiko Wa Hadiyth Mbali Mbali Na Mafunzo Yake)

 

Hadiyth Ya 58

Ishi Duniani Kama Mgeni Au Mpita Njia

 

Alhidaaya.com

 

 

 

عَنْ عَبْدِ اللَّهِ بْنِ عُمَرَ (رضي الله عنهما) قَالَ أَخَذَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ بِمَنْكِبِي فَقَالَ: ((كُنْ فِي الدُّنْيَا كَأَنَّكَ غَرِيبٌ أَوْ عَابِرُ سَبِيلٍ)). وَكَانَ ابْنُ عُمَرَ يَقُولُ: "إِذَا أَمْسَيْتَ فلاَ تَنْتَظِرْ الصَّبَاحَ وَإِذَا أَصْبَحْتَ فلاَ تَنْتَظِرْ الْمَسَاءَ وَخُذْ مِنْ صِحَّتِكَ لِمَرَضِكَ وَمِنْ حَيَاتِكَ لِمَوْتِكَ"  البخاري

 

 Imepokelewa kutoka kwa ‘Abdullaah bin ‘Umar (رضي الله عنهما) amesema: Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alinikamata mabega yangu akasema: ((Kuwa duniani kama mgeni au mpita njia)). Na Ibn ‘Umar alikuwa akisema: “Utakapofika jioni usingojee asubuhi, na ukipambaukiwa usingojee jioni. Na chukua siha yako kabla ya maradhi yako, na uhai wako kabla ya kufa kwako.” [Al-Bukhaariy]

 

 

 

Mafunzo Na Mwongozo:

 

 

 

1. Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) kumkamata ‘Abdullaah bin ‘Umar mabegani ni dalili ya mapenzi yake kwa Maswahaba wake na pia inadhihirisha umuhimu wa jambo analotaka kumwarifu.

 

 

2. Kuishi duniani ni kama mgeni apitaye njia, kwani dunia si ya kudumu, bali Aakhirah ndio yenye maisha ya kudumu. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

وَمَا هَـٰذِهِ الْحَيَاةُ الدُّنْيَا إِلَّا لَهْوٌ وَلَعِبٌ ۚ وَإِنَّ الدَّارَ الْآخِرَةَ لَهِيَ الْحَيَوَانُ ۚ لَوْ كَانُوا يَعْلَمُونَ ﴿٦٤﴾

Na huu uhai wa dunia si chochote isipokuwa ni pumbao na mchezo; na hakika Nyumba ya Aakhirah bila shaka hiyo ndiyo yenye uhai wa kweli hasa (wa milele), lau wangelikuwa wanajua! [Al-‘Ankabuwt (29: 64)].

 

Na Allaah (سبحانه وتعالى) Amepiga mfano mzuri wa maisha ya dunia Anaposema:

 

 

وَاضْرِبْ لَهُم مَّثَلَ الْحَيَاةِ الدُّنْيَا كَمَاءٍ أَنزَلْنَاهُ مِنَ السَّمَاءِ فَاخْتَلَطَ بِهِ نَبَاتُ الْأَرْضِ فَأَصْبَحَ هَشِيمًا تَذْرُوهُ الرِّيَاحُ ۗوَكَانَ اللَّـهُ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ مُّقْتَدِرًا ﴿٤٥﴾

Na wapigie mfano wa uhai wa dunia kama maji Tuliyoyateremsha kutoka mbinguni, yakachanganyika kwayo mimea ya ardhi (ikasitawi), kisha yakawa makavu yaliyovurugika yanapeperushwa na pepo. Na Allaah daima juu ya kila kitu ni Mwenye Uwezo wa juu kabisa. [Al-Kahf (18: 45)]

 

 

3. Mgeni anayepita njia kuelekea aendako bila shaka amejitayarisha kubeba mahitajio yake, hali kadhalika mwana Aadam anahitaji kujibebea masurufu kuelekea safari ya Aakhirah, na masurufu bora kabisa ni taqwa.

 

Rejea: Al-Baqarah (2: 197).

 

 

4. Kukimbilia kufanya ‘amali njema na kutokufanyia usiri kwa kukhofia mauti yamfike mtu kabla ya kudiriki kutena hizo ‘amali. Mfano wa kumdhukuru Allaah (سبحانه وتعالى) na kutoa sadaka Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تُلْهِكُمْ أَمْوَالُكُمْ وَلَا أَوْلَادُكُمْ عَن ذِكْرِ اللَّـهِ ۚ وَمَن يَفْعَلْ ذَٰلِكَ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْخَاسِرُونَ﴿٩﴾

  Enyi walioamini! Zisikupurukusheni mali zenu na wala watoto wenu mkaacha kumdhukuru Allaah. Na yeyote atakayefanya hivyo basi hao ndio waliokhasirika.

 

 

وَأَنفِقُوا مِن مَّا رَزَقْنَاكُم مِّن قَبْلِ أَن يَأْتِيَ أَحَدَكُمُ الْمَوْتُ فَيَقُولَ رَبِّ لَوْلَا أَخَّرْتَنِي إِلَىٰ أَجَلٍ قَرِيبٍ فَأَصَّدَّقَ وَأَكُن مِّنَ الصَّالِحِينَ﴿١٠﴾

  Na toeni katika yale Tuliyokuruzukuni kabla hayajamfikia mmoja wenu mauti akasema: “Rabb wangu! Lau Ungeliniakhirisha mpaka muda wa karibu hivi, basi ningetoa swadaqah na ningelikuwa miongoni mwa Swalihina.”

 

وَلَن يُؤَخِّرَ اللَّـهُ نَفْسًا إِذَا جَاءَ أَجَلُهَا ۚ وَاللَّـهُ خَبِيرٌ بِمَا تَعْمَلُونَ﴿١١﴾

  Lakini Allaah Haiakhirishi kamwe nafsi yeyote inapokuja ajali yake na Allaah ni Mwenye upeo wa khabari za dhahiri na za kufichika kwa yale myatendayo. Al-Munaafiquwn  (63: 9-11)

 

 

Rejea pia: Ibraahiym (14: 31), Al-Baqarah (2: 254).

 

 

5. Siha na uhai ni neema mbili kwa Muumin apasazo kuzitumia kwa kutenda mema yatakayomfaa Aakhirah.

 

Rejea Hadiyth namba (9).

 

 

6. Hili ni fundisho kuwa tusikae duniani kama kwamba tutaishi milele.

 

 

7. Haifai kwa Muislamu kuifadhilisha dunia juu ya Aakhirah yake.

 

Rejea Hadiyth namba (57), (59), (60), (62).

 

 

8. Umuhimu wa kuutumia muda wako vyema hapa duniani.

 

 

 

Share