059-Lu-ulu-un-Manthuwrun: Kuipa Mgongo Dunia Kutampatia Mtu Mapenzi Ya Allaah Pamoja Na Ya Watu
Lu-ulu-un-Manthuwrun
(Mkusanyiko Wa Hadiyth Mbali Mbali Na Mafunzo Yake)
Hadiyth Ya 59
Kuipa Mgongo Dunia Kutampatia Mtu Mapenzi Ya Allaah Pamoja Na Ya Watu
عَنْ سَهْلِ بْنِ سَعْدٍ السَّاعِدِيِّ (رضي الله عنه) قَالَ: أَتَى النَّبِيَّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ رَجُلٌ فَقَالَ: يَا رَسُولَ اللَّهِ، دُلَّنِي عَلَى عَمَلٍ إِذَا أَنَا عَمِلْتُهُ أَحَبَّنِي اللَّهُ وَأَحَبَّنِي النَّاسُ. فَقَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: ((ازْهَدْ فِي الدُّنْيَا يُحِبَّكَ اللَّهُ وَازْهَدْ فِيمَا فِي أَيْدِي النَّاسِ يُحِبُّوكَ)) إبن ماجه وغيره بأسانيد حسنة
Imepokelewa kutoka kwa Sahl bin Sa'ad As-Saa’idiyy (رضي الله عنه) amesema: “Alikuja mtu kwa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akamwambia: “Ee Rasuli wa Allaah! Nijulishe ‘amali ambayo nikiifanya Allaah Atanipenda na watu pia watanipenda.” Akasema: ((Ipe mgongo dunia Allaah Atakupenda, na vipe mgongo vilivyomo kwa watu, watu watakupenda)). [Ibn Maajah na wengineo kwa isnaad Hasan]
Mafunzo Na Mwongozo:
1. Kuipa mgongo dunia (zuhd) ni miongoni mwa sifa za Maswahaba na watu Wema waliopita mfano mmojawapo wa mwenye sifa hii ni Swahaba mtukufu Abu Dharr Al-Ghaffaariy (رضي الله عنه).
2. Umuhimu wa kupata mapenzi ya Allaah (سبحانه وتعالى).
Rejea Hadiyth namba (44), (85).
Pia Hadiyth ya Al-Qudsiy Allaah (سبحانه وتعالى) Anasema: ((Yeyote yule atakayefanya uadui kwa walii Wangu, Nitatangaza vita dhidi yake. Mja Wangu hanikaribii na kitu chochote Ninachokipenda kama ‘amali Nilizomfaradhishia, na mja Wangu huzidi kunikaribia kwa ‘amali njema za Sunnah ili Nimpende. Ninapompenda, Huwa masikio yake yanayosikilizia, macho yake anayoonea, mikono yake anayopigania, miguu yake anayotembelea nayo, lau angeniomba kitu bila shaka Ningempa, lau angeniomba himaya bila shaka Ningelimkinga, na Sisiti juu ya kitu chochote kama Ninavyosita [kuichukua] roho ya mja Wangu Muumin: Anachukia mauti, Nami Nachukia kumdhuru)). [Al-Bukhaariy]
3. Kukinai na rizki ya halali aliyoruzukiwa mtu na kuridhika nayo baada ya kufanya juhudi ya kutafuta na kuifanyia kazi.
Rejea: Al-Maaidah (5: 88).
4. Mazuri yote yaliyomo duniani; mali, mapambo n.k. thamani yake iwe katika mkono wa mtu na si moyoni mwake. Wala asiathirike mtu na dunia bali aathirike na Aakhirah na iwe ndio lengo lake, kwani huko ndiko kwenye maisha ya kudumu: Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
بَلْ تُؤْثِرُونَ الْحَيَاةَ الدُّنْيَا ﴿١٦﴾
Bali mnakhiari uhai wa dunia.
وَالْآخِرَةُ خَيْرٌ وَأَبْقَىٰ ﴿١٧﴾
Na hali Aakhirah ni bora zaidi ya kudumu. [Al-A’laa (87: 16-17).
5. Kutosheka na kutokutafuta rizki ya haramu, na kuzuia nafsi matamanio yake, na kushukuru ya halali na kuitolea sadaka katika Njia ya Allaah (سبحانه وتعالى).
Rejea: [Al-Baqarah (2: 172), An-Nahl (16: 114).
6. Kuipa dunia mgongo (zuhd) si kwa umasikini na kujidhalilisha kuwa daruweshi na mavazi mabovu na kutembea bila viatu na kubeba mitasbihi mikubwa na uvivu, bali ni kuikinaisha nafsi na kuizuia isitamani ya dunia bali itamani ya Aakhirah.
7. Kuridhia mja kwa alichopewa pasi na kutamani vya watu, kwani kutamani vya watu ni njia moja ya kupatikana kwa mizozo na ukhalifu duniani.
Rejea Hadiyth namba: (57), (58), (60) (62).