060-Lu-ulu-un-Manthuwrun: Ingelikuwa Dunia Sawa Na Bawa La Mbu, Allaah Asingelimnywesha kafiri maji.
Lu-ulu-un-Manthuwrun
(Mkusanyiko Wa Hadiyth Mbali Mbali Na Mafunzo Yake)
Hadiyth Ya 60
Ingelikuwa Dunia Sawa Na Bawa La Mbu, Allaah Asingelimnywesha Kafiri Maji
عَنْ سَهْلِ بْنِ سَعْدٍ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: ((لَوْ كَانَتْ الدُّنْيَا تَعْدِلُ عِنْدَ اللَّهِ جَنَاحَ بَعُوضَةٍ مَا سَقَى كَافِرًا مِنْهَا شَرْبَةَ مَاءٍ)) رواه الترمذي وقال: حديث حسن صحيح
Imepokelewa kutoka kwa Sahl bin Sa'ad (رضي الله عنه) amesema: Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Ingelikuwa [thamani ya] dunia ni sawasawa na bawa la mbu mbele ya Allaah, Asingelimnywesha kafiri hata tama moja la maji)). [At-Tirmidhiy na amesema: Hadiyth Hasan Swahiyh]
Mafunzo Na Mwongozo:
1. Dunia haina thamani yoyote mbele ya Allaah (سبحانه وتعالى) hata kama imejaa mazuri vipi. Thamani yake ni kama bawa la mbu mbele ya Allaah (سبحانه وتعالى). Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
اعْلَمُوا أَنَّمَا الْحَيَاةُ الدُّنْيَا لَعِبٌ وَلَهْوٌ وَزِينَةٌ وَتَفَاخُرٌ بَيْنَكُمْ وَتَكَاثُرٌ فِي الْأَمْوَالِ وَالْأَوْلَادِ ۖ كَمَثَلِ غَيْثٍ أَعْجَبَ الْكُفَّارَ نَبَاتُهُ ثُمَّ يَهِيجُ فَتَرَاهُ مُصْفَرًّا ثُمَّ يَكُونُ حُطَامًا ۖ وَفِي الْآخِرَةِ عَذَابٌ شَدِيدٌ وَمَغْفِرَةٌ مِّنَ اللَّـهِ وَرِضْوَانٌ ۚ وَمَا الْحَيَاةُ الدُّنْيَا إِلَّا مَتَاعُ الْغُرُورِ ﴿٢٠﴾
Jueni kwamba uhai wa dunia ni mchezo na pumbao na mapambo, na kufakharishana baina yenu na kushindana kukithiri katika mali na watoto; ni kama mfano wa mvua inayowafurahisha wakulima mimea yake, kisha yananyweya, basi utayaona yamepiga manjano, kisha yanakuwa mabua yaliyonyauka na kupondekapondeka. Na Aakhirah kuna adhabu kali, na maghfirah kutoka kwa Allaah na radhi. Na uhai wa dunia si chochote isipokuwa ni sterehe fupi za kughuri. [Al-Hadiyd (57: 20)]
Rejea pia: Aal-‘Imraan (3: 14-15).
2. Neema anazozichuma mtu duniani hazitomfaa isipokuwa anayezifanya kuwa ni za maisha yake ya kupita njia tu, na akapandikiza mema ili achume Aakhirah. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
مَن كَانَ يُرِيدُ حَرْثَ الْآخِرَةِ نَزِدْ لَهُ فِي حَرْثِهِ ۖ وَمَن كَانَ يُرِيدُ حَرْثَ الدُّنْيَا نُؤْتِهِ مِنْهَا وَمَا لَهُ فِي الْآخِرَةِ مِن نَّصِيبٍ﴿٢٠﴾
Yeyote yule aliyekuwa anataka mavuno ya Aakhirah Tunamzidishia katika mavuno yake; na yeyote yule aliyekuwa anataka mavuno ya dunia, Tutampa humo, lakini Aakhirah hatokuwa na fungu lolote. [Ash-Shuwraa (42: 20)]
Rejea Hadiyth namba (58), (62).
3. Rizki zote hata maji zinakutoka kwa Allaah (سبحانه وتعالى).
4. Kudhalilishwa kwa kafiri.
5. Mbu ni kitu dhalili mno na kinachochukiza, na Allaah (سبحانه وتعالى) Amekipendelea kukipigia mfano kwa maadui wake.
6. Mwerevu ni yule anayetambua hakika ya jambo akaogopa kitu kinachochukiwa na Allaah (سبحانه وتعالى).