061-Lu-ulu-un-Manthuwrun: Dunia Ni Kama Kivuli Anachokitumia Msafiri Kwa Muda Tu
Lu-ulu-un-Manthuwrun
(Mkusanyiko Wa Hadiyth Mbali Mbali Na Mafunzo Yake)
Hadiyth Ya 61
Dunia Ni Kama Kivuli Anachokitumia Msafiri Kwa Muda Tu
عَنْ عَبْدِ اللَّهِ ابن مسعود (رضي الله عنه) قَال: نَامَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ عَلَى حَصِيرٍ فَقَامَ وَقَدْ أَثَّرَ فِي جَنْبِهِ، فَقُلْنَا يَا رَسُولَ اللَّهِ! لَوْ اتَّخَذْنَا لَكَ وِطَاءً. فَقَالَ: ((مَا لِي وَمَا لِلدُّنْيَا؟ مَا أَنَا فِي الدُّنْيَا إِلاَّ كَرَاكِبٍ اسْتَظَلَّ تَحْتَ شَجَرَةٍ ثُمَّ رَاحَ وَتَرَكَهَا)) الترمذي وقال: حَدِيثٌ حَسَنٌ صَحِيحٌ
Imepokelewa kutoka kwa ‘Abdullaah bin Mas’uwd (رضي الله عنه) amesema: “Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alilala kwenye jamvi la mtende likamfanyia alama ubavuni mwake tukasema: Ee Rasuli wa Allaah! Tukufanyie godoro laini? Akasema: ((Mimi na dunia wapi? Mfano wangu na dunia ni kama mpandaji [anayesafiri kwa mnyama] aliyepumzika kivulini chini ya mti, [muda mfupi tu] kisha akaondoka na kukiacha)). [At-Tirmidhiy na amesema Hadiyth Hasan Swahiyh]
Mafunzo Na Mwongozo:
1. Dhihirisho la zuhd ya Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم), yaani kuipa mgongo dunia.
2. Mapenzi na huruma za Maswahaba kwa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) kama yeye vile anavyowapenda na kuwaonea huruma. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
لَقَدْ جَاءَكُمْ رَسُولٌ مِّنْ أَنفُسِكُمْ عَزِيزٌ عَلَيْهِ مَا عَنِتُّمْ حَرِيصٌ عَلَيْكُم بِالْمُؤْمِنِينَ رَءُوفٌ رَّحِيمٌ﴿١٢٨﴾
Kwa yakini amekujieni Rasuli anayetokana na nyinyi wenyewe, yanamtia mashaka (na huzuni) yanayokutaabisheni, anakujalini, mwenye huruma kwa Waumini ni mwenye huruma mno, mwenye rahmah. [At-Tawbah (9: 1280]
Na pia Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
مُّحَمَّدٌ رَّسُولُ اللَّـهِ ۚ وَالَّذِينَ مَعَهُ أَشِدَّاءُ عَلَى الْكُفَّارِ رُحَمَاءُ بَيْنَهُمْ
Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم) ni Rasuli wa Allaah. Na wale walio pamoja naye ni wakali zaidi dhidi ya makafiri; wanahurumiana baina yao [Al-Fat-h (48: 29)]
3. Maisha ya dunia ni nyumba ya kupita, na maisha ya Aakhirah ndiyo ya milele. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَمَا هَـٰذِهِ الْحَيَاةُ الدُّنْيَا إِلَّا لَهْوٌ وَلَعِبٌ ۚ وَإِنَّ الدَّارَ الْآخِرَةَ لَهِيَ الْحَيَوَانُ ۚ لَوْ كَانُوا يَعْلَمُونَ ﴿٦٤﴾
Na huu uhai wa dunia si chochote isipokuwa ni pumbao na mchezo; na hakika Nyumba ya Aakhirah bila shaka hiyo ndiyo yenye uhai wa kweli hasa (wa milele), lau wangelikuwa wanajua! [Al-‘Ankabuwt (29: 64)]
Rejea pia: Al-An’aam (6: 32), Ghaafir (40: 39).
Rejea Hadiyth namba (58), (60).
4. Kujihimiza kujenga Aakhirah kwa ‘amali njema.
5. Mifano ya Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) yenye hikma, busara, mazingatio na mafunzo mazito.
6. Ni vizuri kutoa mifano ili kufahamisha jambo lieleweke kwa undani na kuzidisha iymaan ya mtu.