062-Lu-ulu-un-Manthuwrun: Sadaka Haipunguzi Mali, Msamaha Unazidisha Hadhi, Na Kunyenyekea Kunampandisha Mtu Daraja

 

Lu-ulu-un-Manthuwrun

(Mkusanyiko Wa Hadiyth Mbali Mbali Na Mafunzo Yake) 

Hadiyth Ya 62

Sadaka Haipunguzi Mali, Msamaha Unazidisha Hadhi,

Na Kunyenyekea Kunampandisha Mtu Daraja

Alhidaaya.com

 

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه)  عَنْ رَسُولِ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ: ((مَا نَقَصَتْ صَدَقَةٌ مِنْ مَالٍ،  وَمَا زَادَ اللَّهُ عَبْدًا بِعَفْوٍ إلاَّ عِزًّا، وَمَا تَوَاضَعَ أَحَدٌ لِلَّهِ إِلاَّ رَفَعَهُ اللَّهُ عَزَّ وَ جَلَّ)) مسلم

                                                                                                

Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Kutoa sadaka hakupunguzi mali, Allaah Humzidishia mja ‘izzah (hadhi) kwa ajili ya kusamehe kwake.  Na   yeyote anayenyenyekea kwa ajili ya Allaah, Allaah Aliyetukuka Atampandisha Daraja [Atamtukuza].  [Muslim]

 

 

Mafunzo Na Mwongozo:

 

 

1. Kila anapotoa mtu sadaka, ndipo Allaah (سبحانه وتعالى) Anapomuongezea au Humlipa malipo mema Aakhirah, kwani Ameahidi hivyo kama Anavyosema:

 

مَّن ذَا الَّذِي يُقْرِضُ اللَّـهَ قَرْضًا حَسَنًا فَيُضَاعِفَهُ لَهُ وَلَهُ أَجْرٌ كَرِيمٌ ﴿١١﴾

Nani ambaye atamkopesha Allaah karadha nzuri kisha (Allaah) Amuongezee maradufu na apate ujira mtukufu. [Al-Hadiyd (57: 11)]

 

Rejea pia: Al-Baqarah (2: 245),  (261), Al-Anfaal (8: 60), At-Tawbah (9: 121), Sabaa (34: 39), At-Taghaabun (64: 17).

 

 

2. Kutoa katika Njia ya Allaah (سبحانه وتعالى) ni miongoni mwa sifa za Muumin.  Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

إِنَّمَا الْمُؤْمِنُونَ الَّذِينَ إِذَا ذُكِرَ اللَّـهُ وَجِلَتْ قُلُوبُهُمْ وَإِذَا تُلِيَتْ عَلَيْهِمْ آيَاتُهُ زَادَتْهُمْ إِيمَانًا وَعَلَىٰ رَبِّهِمْ يَتَوَكَّلُونَ﴿٢﴾

Hakika Waumini ni wale ambao Anapotajwa Allaah, nyoyo zao zinajaa khofu na wanaposomewa Aayaat Zake huwazidishia iymaan, na kwa Rabb wao wanatawakali.

 

الَّذِينَ يُقِيمُونَ الصَّلَاةَ وَمِمَّا رَزَقْنَاهُمْ يُنفِقُونَ﴿٣﴾

Ambao wanasimamisha Swalaah na katika yale Tuliyowaruzuku hutoa.

 

أُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُؤْمِنُونَ حَقًّا ۚ لَّهُمْ دَرَجَاتٌ عِندَ رَبِّهِمْ وَمَغْفِرَةٌ وَرِزْقٌ كَرِيمٌ﴿٤﴾

Hao ndio Waumini wa kweli!  Wana daraja (za Jannah) kwa Rabb wao na maghfirah na riziki karimu. [Al-Anfaal (8: 2-4)]

 

Rejea pia: Al-Baqarah (2: 1-5), (265), (274), Aal-‘Imraan (3: 134),  At-Tawbah (9: 111), Al-Hajj (22: 35), As-Sajdah (32: 16), Ash-Shuwraa (42: 38), Adh-Dhaariyaat (51: 19), Al-Ma’aarij (70: 24).

 

 

 

3. Waliobashiriwa Jannah miongoni mwa Maswahaba; Abuu Bakr, ‘Umar, ‘Uthmaan bin ‘Affaan, ‘Abdur-Rahmaan bin ‘Awf (رضي الله عنهم) walitoa mali zao kwa wingi na walizidi kupata kheri na Baraka.

 

4. Kusamehe ni miongoni mwa sifa za Muumin zinazomrejeshea faida mwenyewe. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

الَّذِينَ يُنفِقُونَ فِي السَّرَّاءِ وَالضَّرَّاءِ وَالْكَاظِمِينَ الْغَيْظَ وَالْعَافِينَ عَنِ النَّاسِ ۗ وَاللَّـهُ يُحِبُّ الْمُحْسِنِينَ ﴿١٣٤﴾ 

Ambao wanatoa (kwa ajili ya Allaah) katika hali ya wasaa na katika hali ya shida, na wanazuia ghadhabu, na wenye kusamehe watu. Na Allaah Anapenda wafanyao ihsaan. [Aal-‘Imraan (3: 134)]

 

Rejea pia: An-Nuwr 24: 22) (134).

 

5. Kunyenyekea ni sifa kuu miongoni mwa sifa za Muumin inayompandisha daraja mbele ya Allaah (سبحانه وتعالى).

 

6. Kunyenyekea ni dalili ya kutokuwa na kiburi, na ni ufunguo wa Jannah.

 

Rejea Hadiyth namba (66).

 

 

Share