065-Lu-ulu-un-Manthuwrun: Hatoingia Jannah Mwenye Chembe Ya Kiburi; Kukataa Haki Na Kudharau Watu

 

Lu-ulu-un-Manthuwrun

(Mkusanyiko Wa Hadiyth Mbali Mbali Na Mafunzo Yake)

 

Hadiyth Ya 65

Hatoingia Jannah Mwenye Chembe Ya Kiburi; Nayo Ni Kukataa Haki Na Kudharau Watu

 

 

عَنْ عَبْدِ اللَّهِ بْنِ مَسْعُودٍ  (رضي الله عنه) عَنْ النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ: ((لاَ يَدْخُلُ الْجَنَّةَ مَنْ كَانَ فِي قَلْبِهِ مِثْقَالُ ذَرَّةٍ مِنْ كِبْر))  قَالَ رَجُلٌ: إِنَّ الرَّجُلَ يُحِبُّ أَنْ يَكُونَ ثَوْبُهُ حَسَنًا وَنَعْلُهُ حَسَنَةً.  قَالَ:  ((إِنَّ اللَّهَ جَمِيلٌ يُحِبُّ الْجَمَالَ،  الْكِبْرُ بَطَرُ الْحَقِّ وَغَمْطُ النَّاسِ)) مسلم

 

Imepokelewa kutoka kwa ‘Abdullaah bin Mas’uwd (رضي الله عنه) kwamba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Hatoingia Jannah ambaye moyoni mwake mna kiburi uzito wa chembe (au sisimizi)). Mtu mmoja akauliza: “Mtu hupenda nguo yake iwe nzuri na viatu vyake viwe vizuri [itakuwaje?]” Akasema: ((Hakika Allaah ni Mzuri Anapenda Uzuri. Kiburi ni kukataa haki na kudharau watu)).  [Muslim]

 

 

Mafunzo Na Mwongozo:

 

 

1. Uovu wa kuwa na kiburi ni sifa mbaya sana Anayoichukia Allaah (سبحانه وتعالى), kwani hata kama mtu ana chembe cha kiburi hatoingia Jannah. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

وَلَا تُصَعِّرْ خَدَّكَ لِلنَّاسِ وَلَا تَمْشِ فِي الْأَرْضِ مَرَحًا ۖ إِنَّ اللَّـهَ لَا يُحِبُّ كُلَّ مُخْتَالٍ فَخُورٍ ﴿١٨﴾

 “Na wala usiwageuzie watu uso wako kwa kiburi, na wala usitembee katika ardhi kwa maringo, hakika Allaah Hampendi kila mwenye majivuno mwenye kujifakharisha. [Luqmaan  (31: 18)]

 

Na Anasema pia Allaah (سبحانه وتعالى):

 

وَاللَّـهُ لَا يُحِبُّ كُلَّ مُخْتَالٍ فَخُورٍ ﴿٢٣﴾

na Allaah Hapendi kila mwenye kujinata, anayejifakharisha. [Al-Hadiyd (57: 23)]

 

 

 

Rejea pia:  An-Nisaa (4: 36),  Ghaafir (40: 35).

 

 

 

2. Allaah Anatahadharisha mwenye kiburi kumuingiza Motoni. Hadiyth:

 

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ قَالَ هَنَّادٌ قَالَ قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ:  ((قَالَ اللَّهُ عَزَّ وَجَلَّ الْكِبْرِيَاءُ رِدَائِي وَالْعَظَمَةُ إِزَارِي فَمَنْ نَازَعَنِي وَاحِدًا مِنْهُمَا قَذَفْتُهُ فِي النَّارِ)) أبو داود ، ابن ماجه و أحمد

Kutoka kwa Abu Hurayrah  (رضي الله عنه)    ambaye amesema: Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم)  amesema:  ((Allaah Amesema: Kiburi ni joho Langu,  na utukufu ni kanzu Yangu, yule ashindanaye na Mimi katika kimoja katika hayo nitamvurumisha Motoni)) [Abu Daawuwd, Ibn Maajah na Ahmad]

 

 

 

3. Kibri ni maasi ya kwanza kutendwa pale Ibliys alivyofanya kiburi kutokumsujudia Aadam (عليه السلام) na kujiona yeye ni bora zaidi.  Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

إِذْ قَالَ رَبُّكَ لِلْمَلَائِكَةِ إِنِّي خَالِقٌ بَشَرًا مِّن طِينٍ ﴿٧١﴾

Pale Rabb wako Alipowaambia Malaika: “Hakika Mimi Namuumba mtu kutokana na udongo.

 

فَإِذَا سَوَّيْتُهُ وَنَفَخْتُ فِيهِ مِن رُّوحِي فَقَعُوا لَهُ سَاجِدِينَ ﴿٧٢﴾

 “Basi Nitakapomsawazisha na Nikampuliza humo roho Niliyoiumba; basi mwangukieni kumsujudia.”

 

فَسَجَدَ الْمَلَائِكَةُ كُلُّهُمْ أَجْمَعُونَ ﴿٧٣﴾

Wakamsujudia Malaika wote pamoja.

 

إِلَّا إِبْلِيسَ اسْتَكْبَرَ وَكَانَ مِنَ الْكَافِرِينَ ﴿٧٤﴾

Isipokuwa Ibliys, alitakabari na akawa miongoni mwa makafiri.

 

 

قَالَ يَا إِبْلِيسُ مَا مَنَعَكَ أَن تَسْجُدَ لِمَا خَلَقْتُ بِيَدَيَّ ۖ أَسْتَكْبَرْتَ أَمْ كُنتَ مِنَ الْعَالِينَ ﴿٧٥﴾

 (Allaah) Akasema: “Ee Ibliys! Nini kilichokuzuia usimsujudie Niliyemuumba kwa Mikono Yangu? Je, umetakabari, au umekuwa miongoni mwa waliojitukuza?”

 

قَالَ أَنَا خَيْرٌ مِّنْهُ ۖ خَلَقْتَنِي مِن نَّارٍ وَخَلَقْتَهُ مِن طِينٍ ﴿٧٦﴾

  (Ibliys) akasema: “Mimi ni bora kuliko yeye, Umeniumba kutokana na moto, naye Umemuumba kutokana na udongo.” [Swaad (38: 75-76)]

 

 

Rejea pia:  Al-Hijr (15: 32-33), Al-A’raaf (7: 12).

 

 

4. Kiburi kinaweza kuwa ni kukataa haki katika shariy’ah za Dini kama alivyokataa Ibliys amri ya Allaah (سبحانه وتعالى).

 

 

5. Kiburi kinaweza kuwa ni kudharau watu, kujiona, kujigamba, kujifakharisha kwa watu kwa ukabila, uzuri, mavazi, mali, elimu n.k. yote hayamfai mtu kitu Aakhirah akiwa ana chembe ya kiburi moyoni mwake.

 

Rejea Kisa cha Qaaruwn kilichotajwa katika Qur-aan: Al-Qaswasw (28: 76-83)].

 

 

6. Kujipamba na kuvaa mavazi mazuri masafi ni katika mambo mazuri katika Uislamu.

 

Rejea: Al-A’raaf (7: 31-32).

 

 

Share