066-Lu-ulu-un-Manthuwrun: Nyumba Za Jannah Kwa Mwenye Tabia Njema, Anayeacha Mabishano Na Mjadala Hata Kama ni Mwenye haki, na Anayeacha Uongo

 

Lu-ulu-un-Manthuwrun

(Mkusanyiko Wa Hadiyth Mbali Mbali Na Mafunzo Yake)

 

Hadiyth Ya 66

 

Nyumba Za Jannah Kwa Mwenye Tabia Njema, Anayeacha Mabishano Na Mjadala

Hata Kama ni Mwenye haki, na Anayeacha Uongo

Alhidaaya.com

 

 

 

عَنْ أَبِي أُمَامَةَ البَاهِلي (رضي الله عنه) قَال: قَال رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: ((أَنَا زَعِيم بَيْت فِي رَبَض الْجَنَّة لِمَنْ تَرَكَ الْمِرَاء وَإِنْ كَانَ مُحِقًّا، وَبِبَيْتٍ فِي وَسَط الْجَنَّة لِمَنْ تَرَكَ الْكَذِب وَإِنْ كَانَ مَازِحًا، وَبِبَيْتٍ فِي أَعْلَى الْجَنَّة لِمَنْ حَسُنَ خُلُقه)) حديث صحيح رواه أبو داود بإسناد صحيح

 

Imepokelewa kutoka kwa Abu Umaamah Al-Baahiliy (رضي الله عنه) amesema: Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:  ((Mimi ni mdhamini wa nyumba ya kando ya Jannah kwa anayeacha mabishano [wenye shaka] hata kama ni mwenye haki, na ni mdhamini wa nyumba iliyo katikati ya Jannah kwa anayeacha uongo japo ni kwa mzaha, na mdhamini wa nyumba iliyo mahala pa juu zaidi ya Jannah kwa ambaye tabia yake ni njema)). [Hadiyth Swahiyh ameipokea Abu Daawuwd isnaad yake ni Swahiyh]

           

 

Mafunzo Na Mwongozo:

 

 

1. Fadhila ya subira pindi mtu anapodhulumiwa lakini akaacha mjadala usioleta manufaa ili kuepusha magomvi, na akasemehe juu ya kwamba ana haki ya kupigania kwa kulipiza kisasi. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

وَجَزَاءُ سَيِّئَةٍ سَيِّئَةٌ مِّثْلُهَا ۖ فَمَنْ عَفَا وَأَصْلَحَ فَأَجْرُهُ عَلَى اللَّـهِ ۚ إِنَّهُ لَا يُحِبُّ الظَّالِمِينَ﴿٤٠﴾ وَلَمَنِ انتَصَرَ بَعْدَ ظُلْمِهِ فَأُولَـٰئِكَ مَا عَلَيْهِم مِّن سَبِيلٍ﴿٤١﴾ إِنَّمَا السَّبِيلُ عَلَى الَّذِينَ يَظْلِمُونَ النَّاسَ وَيَبْغُونَ فِي الْأَرْضِ بِغَيْرِ الْحَقِّ ۚ أُولَـٰئِكَ لَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ﴿٤٢﴾ وَلَمَن صَبَرَ وَغَفَرَ إِنَّ ذَٰلِكَ لَمِنْ عَزْمِ الْأُمُورِ﴿٤٣﴾

Na jazaa ya uovu ni uovu mfano wake. Lakini atakayesamehe na akasuluhisha, basi ujira wake uko kwa Allaah, hakika Yeye Hapendi madhalimu. Na bila shaka anayelipiza kisasi baada ya kudhulumiwa, basi hao hawana sababu ya kulaumiwa. Hakika sababu ya kulaumiwa ni juu ya wale wanaodhulumu watu na wanakandamiza katika ardhi bila ya haki. Hao watapata adhabu iumizayo.Na atakayevuta subira na akasamehe, hakika hilo bila shaka ni katika mambo ya kuazimiwa. [Ash-Shuwraa (42: 40-43)]

 

 

 2. Kuacha mzaha na maneno ya upuuzi ni sifa miongoni mwa sifa zitakazompatia Muumin Jannah ya Firdaws [Al-Muuminuwn (23: 1-11)].

 

 

3. Tabia njema ni mzizi wa kumuongoa Muislamu kwa kila upande na kumpatia fadhila za kila aina na malipo makuu kabisa ni ya mwenye tabia njema.

 

 

4. Nabiy  (صلى الله عليه وآله وسلم) amesisitiza sana Muislamu kuwa na tabia njema katika Hadiyth kadhaa, na malipo yake si Jannah pekee bali pia ni kuwa karibu naye huko Jannah. Akasema pia katika Hadiyth ifuatayo kuwa yeye ametumwa kwa Ummah huu wa Kiislamu ili kutimiza tabia njema:

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ رَضِيَ الله عَنْهُ أَنَّ رَسُولَ اللهِ صلى الله عليه وسلم قَالَ‏:‏ ((إِنَّمَا بُعِثْتُ لِأُتَمِّمَ صَالِحَ الأَخْلاقِ‏))

Abuu Hurayrah (رضي الله عنه)  amesema: Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم)  amesema: ((Hakika nimetumwa ili nikamilishe khulqa (tabia) njema)) [Ahmad na ameisahihisha Al-Albaaniy Swahiyh Al-Jaami’ (2349), Swahiyh Adab Al-Mufrad (207)]

 

 

Rejea pia: Hadiyth namba (65), (67), (127).

 

 

5. Fadhila za kuacha uongo ambao unamuingiza mtu katika unafiki na adhabu ya moto hata kama ni kwa mzaha tu.

 

 

6. Tusiwe ni wenye kupuuzia jambo hata tukiliona kuwa ni dogo sana kwa mizani zetu.

 

 

 

 

Share