067-Lu-ulu-un-Manthuwrun: Sahilisheni, Msifanye Uzito, Wabashirieni Msiwakimbize Watu Katika Dini

 

Lu-ulu-un-Manthuwrun

(Mkusanyiko Wa Hadiyth Mbali Mbali Na Mafunzo Yake)

 

Hadiyth Ya 67

Sahilisheni, Msifanye Uzito, Wabashirieni Msiwakimbize Watu Katika Dini

Alhidaaya.com

 

 

عَنْ أَنَسِ (رضي الله عنه) عَنْ النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ: ((يَسِّرُوا وَلاَ تُعَسِّرُوا وَبَشِّرُوا ولاَ تُنَفِّرُوا)) متفق عليه

 

Imepokelewa kutoka kwa Anas (رضي الله عنه)  kwamba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Sahilisheni wala msifanye uzito, wapendekezeni watu kheri na muwabashirie wala msiwakimbize)). [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

 

Mafunzo Na Mwongozo:

 

 

1. Dini yetu ya Kiislamu ni nyepesi ila watu wenyewe wanaitilia uzito. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

  وَمَا جَعَلَ عَلَيْكُمْ فِي الدِّينِ مِنْ حَرَجٍ ۚ  

Na Hakukufanyieni ugumu wowote ule katika Dini. [Al-Hajj (22: 78)].

 

 

2. Haipasi kuwafanyia Waislamu uzito katika Dini pale mtu anapowalingania (da’wah) ikasababisha kuwakimbiza.  Haipasi hata kwa makafiri pale anapowalingania waingie katika Uislamu, bali anapaswa atumie mawaidha mema na hikma kama Anavyoamrisha Allaah (سبحانه وتعالى):

 

 ادْعُ إِلَىٰ سَبِيلِ رَبِّكَ بِالْحِكْمَةِ وَالْمَوْعِظَةِ الْحَسَنَةِ ۖ وَجَادِلْهُم بِالَّتِي هِيَ أَحْسَنُ ۚ إِنَّ رَبَّكَ هُوَ أَعْلَمُ بِمَن ضَلَّ عَن سَبِيلِهِ ۖ وَهُوَ أَعْلَمُ بِالْمُهْتَدِينَ﴿١٢٥﴾

Lingania katika njia ya Rabb wako kwa hikmah na mawaidha mazuri. Na jadiliana nao kwa ambayo ni mazuri zaidi. Hakika Rabb wako Yeye Anamjua zaidi aliyepotea njia Yake, Naye Anawajua zaidi waliohidika. [An-Nahl (16: 125)]

 

 

3. Muislamu anapaswa kumbashiria mwenziwe kila la kheri na kumpendelea mazuri.

 

Rejea Hadiyth namba  (21).

 

 

 

4. Hadiyth hii ni dalili ya kwamba Uislamu ni Dini nyepesi na sahali katika amri na fardhi zake na Shariy’ah ambazo hazimkalifishi mtu zaidi ya asiyoyaweza.

 

Rejea Al-Baqarah (2: 185) (286), Al-Maaidah (5: 6), An-Nuwr (24: 61), Al-Fat-h (48: 17), At-Tawbah (9: 91).

 

 

 

5. Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) mwenyewe ametumwa kwetu kutusahilishia mambo yetu ya Kidini.

 

Rejea Al-A‘raaf (7: 157).

 

 

 

6. Mtu kujitakia mazito katika Dini ni sababu kuu ya watu kushindwa kutekeleza amri za Allaah (سبحانه وتعالى) na Rasuli Wake (صلى الله عليه وآله وسلم). Mazito hayo anayojitakia mtu ni kama vile kutenda ‘ibaadah ambazo hazimo katika Shariy’ah, mfano: Kuweka matanga ambayo yanamgharimu mtu kulisha watu. Hali kadhalika kualika watu katika kusherehekea mawlid, kukusanya watu kusoma du’aa pindi mtu kafikwa na jambo fulani, mkusanyiko wa khitma, mkusanyiko wa kumdhukuru Allaah, yote haya ni kujishughulisha katika matendo ambayo anayapotezea mali yake na muda wake. Mali hiyo na muda huo angeliweza kutumia katika yaliyoamrishwa katika Shariy’ah kwa kutoa katika njia ya Allaah, na muda kuutumia katika ‘ibaada zilizo sahihi.

 

 

 

 

 

 

 

Share