069-Lu-ulu-un-Manthuwrun: Aliye Na Daraja Mbaya Mno Mbele Ya Allaah Siku ya Qiyaamah Ni Yule Anayeeneza Siri Ya Mkewe

 

Lu-ulu-un-Manthuwrun

(Mkusanyiko Wa Hadiyth Mbali Mbali Na Mafunzo Yake)

 

Hadiyth Ya 69

Aliye Na Daraja Mbaya Mno Mbele Ya Allaah Siku ya Qiyaamah

Ni Yule Anayeeneza Siri Ya Mkewe

Alhidaaya.com

 

 

عَنْ أبي سَعِيدٍ الْخُدْرِيَّ (رضي الله عنه) قَال: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: ((إِنَّ مِنْ أَشَرِّ النَّاسِ عِنْدَ اللَّهِ مَنْزِلَةً يَوْمَ الْقِيَامَةِ الرَّجُلَ يُفْضِي إِلَى امْرَأَتِهِ وَتُفْضِي إِلَيْهِ ثُمَّ يَنْشُرُ سِرَّهَا)) مسلم

 

Imepokelewa kutoka kwa Abu Sa’iyd Al-Khudriyy (رضي الله عنه) amesema: Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Hakika mwenye daraja mbaya mno mbele ya Allaah siku ya Qiyaamah, ni mwanamume anayejamiiana na mkewe kisha akaeneza siri yake)). [Muslim]

 

 

Mafunzo Na Mwongozo:

 

 

1. Kutoa siri ni miongoni mwa madhambi makubwa. Na Allaah (سبحانه وتعالى) Hamsamehe mwenye kufichua maasi yake ilhali Allaah (سبحانه وتعالى) Amemsitiri. Hadiyth ya Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم):

 

عن ابي هُرَيْرَةَ، يَقُولُ سَمِعْتُ رَسُولَ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم يَقُولُ: (( كُلُّ أُمَّتِي مُعَافًى إِلاَّ الْمُجَاهِرِينَ، وَإِنَّ مِنَ الْمَجَانَةِ أَنْ يَعْمَلَ الرَّجُلُ بِاللَّيْلِ عَمَلاً، ثُمَّ يُصْبِحَ وَقَدْ سَتَرَهُ اللَّهُ، فَيَقُولَ: يَا فُلاَنُ عَمِلْتُ الْبَارِحَةَ كَذَا وَكَذَا، وَقَدْ بَاتَ يَسْتُرُهُ رَبُّهُ وَيُصْبِحُ يَكْشِفُ سِتْرَ اللَّهِ عَنْهُ )) البخاري ‏

 

Kutoka kwa Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) kasema: Nimemisikia Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akisema: ((Dhambi za Ummah wangu zitasamehewa isipokuwa za Al-Mujaahiriyn [wanaotenda maasi waziwazi au wanaofichua maasi yao kwa watu].  Mfano wa kufichua huko siri ni mtu anayetenda kitendo usiku kisha akaamka hali ya kuwa Allaah Amemsitiri, lakini anasema: “Ee fulani, jana usiku nilitenda kadhaa wa kadhaa.” Ilhalia amekesha usiku akiwa katika sitara ya Rabb wake lakini yeye asubuhi anajifichulia sitara ya Allaah)) [Al-Bukhaariy]

 

 

2. Kuhifadhi haki za mke na mume. Hii inamhusu mke pia ambaye anatakiwa ajilinde yeye sitara yake, na ahifadhi mambo ya mumewe hasa anapokuwa mumewe hayupo naye, na kutokutoa siri zao. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

فَالصَّالِحَاتُ قَانِتَاتٌ حَافِظَاتٌ لِّلْغَيْبِ بِمَا حَفِظَ اللَّـهُ ۚ

Basi wanawake wema ni wale watiifu wenye kujihifadhi katika hali ya kutokuweko waume zao kwa kuwa Allaah Ameamrisha wajihifadhi. [An-Nisaa (4: 34)]

 

 

3. Tahadharisho kali la kutangazia siri ya chumbani mwa wanandoa kwamba atapata daraja mbaya mno mbele ya Allaah (سبحانه وتعالى).

 

 

 4. Uislamu unahimiza kuhifadhiana siri baina ya mke na mume na watu kwa ujumla.

 

Rejea Hadiyth namba (23).

 

 

5. Vitendo vya ndoa baina ya mume na mke ni vitendo vya aibu vinavyopasa Muislamu awe na hayaa, na hivyo ni kuthibitisha iymaan yake.

 

Rejea Hadiyth namba (68).

 

 

6. Uovu wa kutoa siri baina ya wanandoa ni mkubwa. Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema kuwa mfano wake ni kama wa shaytwaan mwanamme na mwanamke kukutana njiani na kufanya kitendo hicho mbele ya macho ya watu]. [Abuu Daawuwd Taz. Swahiyh Al-Jaami' (7037)]

 

 

 

 

 

Share