070-Lu-ulu-un-Manthuwrun: Usiwe Mwenye Kuzoea Kufanya ‘Ibaadah Ya Sunnah, Naafilah, Kisha Ukaiacha

 

Lu-ulu-un-Manthuwrun

(Mkusanyiko Wa Hadiyth Mbali Mbali Na Mafunzo Yake)

Hadiyth Ya 70

Usiwe Mwenye Kuzoea Kufanya ‘Ibaadah Ya Sunnah, Naafilah, Kisha Ukaiacha

Alhidaaya.com

 

 

 

عَنْ عَبْدُ اللَّهِ بْنُ عَمْرِو بْنِ الْعَاصِ (رضي الله عنهما)  قَالَ: قَالَ لِي رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: ((يَا عَبْدَ اللَّهِ، لاَ تَكُنْ مِثْلَ فلاَنٍ كَانَ يَقُومُ اللَّيْلَ فَتَرَكَ قِيَامَ اللَّيْلِ)) متفق عليه

Imepokelewa kutoka kwa ‘Abdullaah bin ‘Amru bin Al-‘Aasw (رضي الله عنهما) amesema: “Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) aliniambia: ((Ee ‘Abdullaah! Usiwe kama fulani, alikuwa akiamka usiku kuswali akaacha Qiyaamul-layl (kisimamo cha usiku kuswali)). [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

 

 

Mafunzo Na Mwongozo:

 

 

1. Fadhila za kudumisha ‘amali njema japokuwa ni kidogo kama alivyosema Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم): ((‘Amali bora kabisa Azipendazo Allaah ni zenye kudumu japokuwa ni chache)). [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

 

2. Umuhimu wa kuwa na istiqaamah (msimamo) katika ‘Ibaadah kama Allaah (سبحانه وتعالى) Alivyomuamrisha Rasuli Wake (صلى الله عليه وآله وسلم):

 

 وَاعْبُدْ رَبَّكَ حَتَّىٰ يَأْتِيَكَ الْيَقِينُ﴿٩٩﴾

Na mwabudu Rabb wako mpaka ikufikie yakini (mauti). [Al-Hijr (15: 99)] 

Rejea pia: Fusswilat (41: 30-32), Al-Ahqaaf (46: 13-14), Al-Ma’aarij (70: 23).

 

Rejea pia Hadiyth namba (7)

 

Na pia Hadiyth:

 

 

عن أبي عمر، وقيل: أبي عَمرة سفيان بن عبد الله رضي الله عنه قَالَ: قُلْتُ: يَا رَسُول الله، قُلْ لي في الإسْلامِ قَولًا لا أسْأَلُ عَنْهُ أَحَدًا غَيْرَكَ. قَالَ: ((قُلْ: آمَنْتُ بِاللهِ، ثُمَّ استَقِمْ)). رواه مسلم

Abuu 'Umar na pia imesemwa anajulikana kama: Abuu ‘Amrah Sufyaan bin ‘Abdillaah (رضي الله عنه)  amesema: Nilimwambia Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم): Niambie neno katika Uislamu ambalo sitamuuliza yoyote zaidi yako. Akasema: ((Sema: Nimemuamini Allaah, kisha uthibitike imara)) [Muslim]

 

Kwa maana: Kuendelea kufanya ‘Ibaadah na kuwa na msimamo madhubuti katika Dini.

 

 

 

3. Kuacha ‘Ibaadah au ‘amali njema alizozizoea mtu, ni dalili ya kushughulishwa na dunia na kuwa mbali na Allaah (سبحانه وتعالى).

 

 

4. Uislamu unapendelea wastani au ukatikati hata katika ‘Ibaadah, ili asijikalifishe mtu au kujichosha. Hadiyth kadhaa zimetajwa makatazo ya kujikalifisha au kufanya ‘ibaadah kwa wingi mno, miongoni mwazo ni:

 

وعن أنس رضي الله عنه قَالَ: دَخَلَ النَّبيُّ صلى الله عليه وسلم المَسْجِدَ فَإِذَا حَبْلٌ مَمْدُودٌ بَيْنَ السَّارِيَتَيْنِ، فَقَالَ: ((مَا هَذَا الحَبْلُ؟)) قالُوا: هَذَا حَبْلٌ لِزَيْنَبَ، فَإِذَا فَتَرَتْ تَعَلَّقَتْ بِهِ. فَقَالَ النَّبيُّ صلى الله عليه وسلم: ((حُلُّوهُ، لِيُصلِّ أَحَدُكُمْ نَشَاطَهُ فَإِذَا فَتَرَ فَلْيَرْقُدْ)). مُتَّفَقٌ عَلَيه

 

Na amepokea Anas (رضي الله عنه) kwamba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) aliingia Masjid, akaona kamba imefungwa baina ya nguzo mbili. Akauliza: ((Kamba hii ni ya nini?)) Wakasema: Hii ni kamba ya Zaynab, anapochoka hujiegemeza kwayo. Basi Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akasema: ((Ifungueni na kila mmoja wenu aswali kwa nguvu zake, atakapochoka alale)) [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Na pia:

 

عن أنس رضي الله عنه قَالَ: جَاءَ ثَلاثَةُ رَهْطٍ إِلَى بُيُوتِ أزْوَاجِ النَّبيّ صلى الله عليه وسلم، يَسْأَلُونَ عَنْ عِبَادَةِ النَّبيّ صلى الله عليه وسلم فَلَمَّا أُخْبِروا كَأَنَّهُمْ تَقَالُّوهَا وَقَالُوا: أَيْنَ نَحْنُ مِنَ النَّبيِّ صلى الله عليه وسلم قدْ غُفِرَ لَهُ مَا تَقَدَّمَ مِنْ ذَنْبِهِ وَمَا تَأخَّرَ. قَالَ أحدُهُم: أمَّا أنا فَأُصَلِّي اللَّيلَ أبدًا. وَقالَ الآخَرُ: وَأَنَا أصُومُ الدَّهْرَ وَلا أُفْطِرُ. وَقالَ الآخر: وَأَنا أعْتَزِلُ النِّسَاءَ فَلا أتَزَوَّجُ أبَدًا. فجاء رسولُ الله صلى الله عليه وسلم إليهم، فَقَالَ: ((أنْتُمُ الَّذِينَ قُلْتُمْ كَذَا وَكَذَا؟ أَمَا واللهِ إنِّي لأخْشَاكُمْ للهِ، وَأَتْقَاكُمْ لَهُ، لَكِنِّي أصُومُ وَأُفْطِرُ، وأُصَلِّي وَأَرْقُدُ، وَأَتَزَوَّجُ النِّساءَ، فَمَنْ رَغِبَ عَنْ سُنَّتِي فَلَيْسَ مِنِّي)). مُتَّفَقٌ عَلَيه

Imepokelewa na Anas (رضي الله عنه) kwamba kundi la watu watatu lilikuja katika nyumba za wake wa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم)  wakiuliza kuhusu ‘ibaadah za Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم).  Walipoelezwa waliziona kama ni kidogo, wakasema: Sisi hatuko sawa na Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم), yeye ameshaghufuriwa madhambi yake yaliyotangulia na yatakayokuja. Mmoja wao akasema: Ama mimi, nitaswali daima usiku wote. Mwengine akasema: mimi nitafunga mwaka mzima. Mwengine akasema: Mimi nitawaepuka wanawake, sitaoa kamwe. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akawaendea na kuwauliza: ((Ninyi ndio mliosema kadhaa na kadhaa? Ama wa-Allaahi mimi ninamkhofu Allaah zaidi ya nina taqwa zaidi kulikoni ninyi; lakini mimi ninafunga na kufungua, ninaswali na ninalala, na pia ninaoa wake. Atakayekengeuka na Sunnah zangu basi si katika mimi)) [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

 

Rejea pia Hadiyth namba 12].

 

 

 

 

 

Share