084-Lu-ulu-un-Manthuwrun: Mimi Ni Vile Mja Wangu Anavyonidhania. Niko Pamoja Naye Anaponitaja

 

Lu-ulu-un-Manthuwrun

 

(Mkusanyiko Wa Hadiyth Mbali Mbali Na Mafunzo Yake)

 

Hadiyth Ya 84

 

Mimi Ni Vile Mja Wangu Anavyonidhania. Niko Pamoja Naye Anaponitaja

 

 

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ النَّبِيُّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: ((يَقُولُ اللَّهُ تَعَالَى: أَنَا عِنْدَ ظَنِّ عَبْدِي بِي وَأَنَا مَعَهُ إِذَا ذَكَرَنِي، فَإِنْ ذَكَرَنِي فِي نَفْسِهِ ذَكَرْتُهُ فِي نَفْسِي، وَإِنْ ذَكَرَنِي فِي مَلَإٍ ذَكَرْتُهُ فِي مَلَإٍ خَيْرٍ مِنْهُمْ، وَإِنْ تَقَرَّبَ إِلَيَّ بِشِبْرٍ تَقَرَّبْتُ إِلَيْهِ ذِرَاعًا،

 وَإِنْ تَقَرَّبَ إِلَيَّ ذِرَاعًا تَقَرَّبْتُ إِلَيْهِ بَاعًا، وَإِنْ أَتَانِي يَمْشِي أَتَيْتُهُ هَرْوَلَةً)) متفق عليه

 

 Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) ambaye amesema: Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم)  alisema: ((Allaah Ta’aalaa Anasema: Mimi ni vile mja Wangu anavyonidhania. Niko pamoja naye anaponitaja. Anaponitaja katika nafsi yake, Ninamtaja katika nafsi Yangu, anaponitaja katika hadhara, Ninamtaja katika hadhara bora zaidi. Na anaponikaribia shibiri Ninamkaribia dhiraa, anaponikaribia dhiraa, Ninamkaribia pima, anaponijia kwa mwendo [wa kawaida] Ninamwendea mbio)). [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

 

 

Mafunzo Na Mwongozo:

 

 

 

1. Wajibu wa kuwa na husnudhw-dhwann (dhana nzuri) kwa Allaah (سبحانه وتعالى) na kutokukata tamaa na Rahma Yake pindi mtu anapokuwa katika shida na dhiki au mtu anapotaka jambo fulani afanikiwe. Basi asichoke wala asikate tamaa kwani kukata tamaa ni kukufuru kama alivyosema Nabiy Ya’quwb (عليه السلام) kuwaambia wanawe katika kumtafuta Nabiy Yuwsuf (عليه السلام) :   

 

وَلَا تَيْأَسُوا مِن رَّوْحِ اللَّـهِ ۖ إِنَّهُ لَا يَيْأَسُ مِن رَّوْحِ اللَّـهِ إِلَّا الْقَوْمُ الْكَافِرُونَ ﴿٨٧﴾

Wala msikate tamaa na faraja ya Allaah; hakika hawakati tamaa na faraja ya Allaah isipokuwa watu makafiri.”  [Yuwsuf (12: 87)]

 

 

Rejea pia Al-Baqarah (2: 249) pindi Muumini anapofikwa na hali ngumu kabisa ambayo anakaribiwa kushindwa nguvu.

 

 

 

2. Kuwa na husnudhw-dhwann (dhana nzuri) na Allaah (سبحانه وتعالى) katika kumuomba maghfirah na tawbah kwani Yeye Anapokea tawbah za waja Wake hata yawe ni madhambi makubwa vipi madam tu mja atarudi kuomba maghfirah na atatubia kwa Allaah (سبحانه وتعالى) kama Anavyosema:

 

قُلْ يَا عِبَادِيَ الَّذِينَ أَسْرَفُوا عَلَىٰ أَنفُسِهِمْ لَا تَقْنَطُوا مِن رَّحْمَةِ اللَّـهِ ۚ إِنَّ اللَّـهَ يَغْفِرُ الذُّنُوبَ جَمِيعًا ۚ إِنَّهُ هُوَ الْغَفُورُ الرَّحِيمُ﴿٥٣﴾

Sema: Enyi waja Wangu ambao wamepindukia mipaka juu ya nafsi zao: “Msikate tamaa na rahmah ya Allaah; hakika Allaah Anaghufuria dhambi zote; hakika Yeye Ndiye Mwenye kughufuria, Mwenye kurehemu.” [Az-Zumar (39: 53)]

 

 

 

3. Kuwa na husnudhw-dhwann (dhana nzuri) na Allaah (سبحانه وتعالى) katika kumuomba du’aa pia ambayo ni mojawapo wa sababu ya kutakabaliwa du’aa kama alivyosema Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم):

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ): ((ادْعُوا اللَّهَ وَأَنْتُمْ مُوقِنُونَ بِالإِجَابَةِ وَاعْلَمُوا أَنَّ اللَّهَ لاَ يَسْتَجِيبُ دُعَاءً مِنْ قَلْبٍ غَافِلٍ لاَهٍ))

Kutoka kwa Abuu Hurayrah (رضي الله عنه)  kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم)  amesema: ((Muombeni Allaah huku mkiwa mna yakini kujibiwa, na jueni kwamba Allaah Hatakabali du’aa inayotoka katika moyo ulioghafilika au usiojali)) [Swahiyh At-Tirmidhiy (3479), Swahiyh Al-Jaami’ *245), Swahiyh At-Targhiyb (1653)]

 

 

 

 

4. Wasiya wa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) siku tatu kabla ya kufariki kwake kwamba Muumini awe na husnudhw-dhwann (dhana nzuri) kwa Rabb Wake:   

 

 

عَنْ جَابِرٍ، قَالَ سَمِعْتُ النَّبِيَّ صلى الله عليه وسلم قَبْلَ وَفَاتِهِ بِثَلاَثٍ يَقُولُ: ((لاَ يَمُوتَنَّ أَحَدُكُمْ إِلاَّ وَهُوَ يُحْسِنُ بِاللَّهِ الظَّنَّ)) مسلم

 Imepokelewa kutoka kwa Jaabir (رضي الله عنه) ambaye amesema: Nimesikia Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akisema: ((Asife mtu isipokuwa awe ana husnudhw-dhwann (dhana nzuri) na Allaah)) [Muslim]

 

 

 

5. Miongoni mwa sifa za Waumini ni kuwa na husnudhw-dhwann (dhana nzuri) kwamba watakutana na Allaah (سبحانه وتعالى) huko Aakhirah. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

الَّذِينَ يَظُنُّونَ أَنَّهُم مُّلَاقُو رَبِّهِمْ وَأَنَّهُمْ إِلَيْهِ رَاجِعُونَ ﴿٤٦﴾

Ambao wana yakini kwamba hakika wao ni wenye kukutana na Rabb wao na hakika wao Kwake ni wenye kurejea. [Al-Baqarah (2; 46)]

 

 

 

 

6. Kinyume chake ni sifa za wanafiki na makafiri, na waovu wanaomdhania Allaah (سبحانه وتعالى) suw’udhw-dhwann (dhanna mbaya). Hao watapata adhabu za Allaah (سبحانه وتعالى) kama Anavyosema (سبحانه وتعالى):

 

وَيُعَذِّبَ الْمُنَافِقِينَ وَالْمُنَافِقَاتِ وَالْمُشْرِكِينَ وَالْمُشْرِكَاتِ الظَّانِّينَ بِاللَّـهِ ظَنَّ السَّوْءِ ۚ عَلَيْهِمْ دَائِرَةُ السَّوْءِ ۖ وَغَضِبَ اللَّـهُ عَلَيْهِمْ وَلَعَنَهُمْ وَأَعَدَّ لَهُمْ جَهَنَّمَ ۖ وَسَاءَتْ مَصِيرًا﴿٦﴾

Na Awaadhibu wanafiki wa kiume na wanafiki wa kike na washirikina wa kiume na washirikina wa kike, wanaomdhania Allaah dhana ovu.  Utawafikia mgeuko mbaya; na Allaah Awaghadhibikie, na Awalaani, na Awaandalie  Jahannam, na paovu palioje mahali pa kuishia. [Al-Fat-h (48: 6)]

 

Ni sawa na wanafiki   katika vita vya Uhud wakimdhania Allaah (سبحانه وتعالى) dhana mbaya. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

 

  وَطَائِفَةٌ قَدْ أَهَمَّتْهُمْ أَنفُسُهُمْ يَظُنُّونَ بِاللَّـهِ غَيْرَ الْحَقِّ ظَنَّ الْجَاهِلِيَّةِ ۖ يَقُولُونَ هَل لَّنَا مِنَ الْأَمْرِ مِن شَيْءٍ ۗ قُلْ إِنَّ الْأَمْرَ كُلَّهُ لِلَّـهِ ۗ يُخْفُونَ فِي أَنفُسِهِم مَّا لَا يُبْدُونَ لَكَ ۖ يَقُولُونَ لَوْ كَانَ لَنَا مِنَ الْأَمْرِ شَيْءٌ مَّا قُتِلْنَا هَاهُنَا ۗ  

Kundi likawashughulisha nafsi zao wakamdhania Allaah pasi na haki dhana ya kijahili; wanasema: “Je, tuna amri yoyote sisi katika jambo hili?” Sema: “Hakika amri yote ni ya Allaah.” Wanaficha katika nafsi zao yale wasiyokubainishia. Wanasema: “Lau tungelikuwa tuna amri yoyote katika jambo basi tusingeliuliwa hapa.”  [Aal-‘Imraan (3: 154)]

  

 

7. Fadhila za kumdhukuru Allaah (سبحانه وتعالى) ni nyingi mno na ‘ibaadah hii haina kikomo. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

 يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اذْكُرُوا اللَّـهَ ذِكْرًا كَثِيرًا ﴿٤١﴾

Enyi walioamini!  Mdhukuruni Allaah kwa wingi wa kumdhukuru.

 

وَسَبِّحُوهُ بُكْرَةً وَأَصِيلًا ﴿٤٢﴾

Na Msabbihini asubuhi na jioni.

 

هُوَ الَّذِي يُصَلِّي عَلَيْكُمْ وَمَلَائِكَتُهُ لِيُخْرِجَكُم مِّنَ الظُّلُمَاتِ إِلَى النُّورِ ۚ وَكَانَ بِالْمُؤْمِنِينَ رَحِيمًا ﴿٤٣﴾

Yeye Ndiye Anakurehemuni, na Malaika Wake wanamuomba Akughufurieni na Akurehemuni ili Akutoeni kutoka katika viza kuingia katika Nuru. Naye daima ni Mwenye kurehemu Waumini.

 

تَحِيَّتُهُمْ يَوْمَ يَلْقَوْنَهُ سَلَامٌ ۚ وَأَعَدَّ لَهُمْ أَجْرًا كَرِيمًا ﴿٤٤﴾

Maamkizi yao Siku watakayokutana Naye; ni ‘Salaam’; na Amewaandalia ujira wa ukarimu. [Al-Ahzaab (33: 41-44)]

 

Rejea pia: Al-Baqarah (2: 152), Aal-‘Imraan (3: 191-195), Ar-Ra’d (13: 28).

 

Rejea pia Hadiyth namba (85).

 

 

 

8. Kumdhukuru Allaah (سبحانه وتعالى) kwa dhahiri na siri, nyakati zote, katika kila hali ni ‘amali tukufu kabisa inayomkurubisha mja kwa Rabb wake kwani mja anapomdhukuru Allaah (سبحانه وتعالى), Naye hukumbuka kama Anavyosema:

 

فَاذْكُرُونِي أَذْكُرْكُمْ وَاشْكُرُوا لِي وَلَا تَكْفُرُونِ﴿١٥٢﴾

Basi nidhukuruni na Mimi Nitakukumbukeni; na nishukuruni wala msinikufuru. [Al-Baqarah (2: 152)] 

 

 

 

9. Anayetaka kukumbukwa na Allaah (سبحانه وتعالى) basi na amdhukuru na amshukuru apate malipo mema.  Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

وَالذَّاكِرِينَ اللَّـهَ كَثِيرًا وَالذَّاكِرَاتِ أَعَدَّ اللَّـهُ لَهُم مَّغْفِرَةً وَأَجْرًا عَظِيمًا ﴿٣٥﴾

Na wanaomdhukuru Allaah kwa wingi wanaume na wanawake; Allaah Amewaandalia maghfirah na ujira adhimu. [Al-Ahzaab (33: 35)]

 

 

 

10. Hadiyth inadhihirisha mapenzi ya Allaah (سبحانه وتعالى) kwa waja Wake wanaomdhukuru sana na wanaotenda ‘ibaadah ziada.

 

 

 

11. Dhihirisho la daraja ya vikao baina ya waja, Malaika, na Manabii. Wanavyuoni wamesema: “Hakika Manabii Wateule katika watu, ni bora kuliko Malaika Wateule kama Jibriyl. Na Malaika Wateule ni bora kuliko watu wa kawaida. Na watu wa kawaida nao ni wale wenye kutii, ni bora kuliko Malaika wa kawaida. Na Malaika wa kawaida ni bora kuliko watu wenye kufanya maasi.” [Nuzhat Al-Muttaqiyn (2: 217)]

 

 Rejea pia Hadiyth namba (98).

 

 

Share