085-Lu-ulu-un-Manthuwrun: Kumdhukuru Allaah Kunampandisha Cheo Mja Na Ni Miongoni Mwa ‘Amali Bora Kabisa

 

Lu-ulu-un-Manthuwrun

 

(Mkusanyiko Wa Hadiyth Mbali Mbali Na Mafunzo Yake)

 

Hadiyth Ya 85

 

Kumdhukuru Allaah Kunampandisha Cheo Mja Na Ni Miongoni Mwa ‘Amali Bora Kabisa

 

 

 

 

عَنْ أَبِي الدَّرْدَاءِ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ النَّبِيُّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: ((ألاَ أُنَبِّئُكُمْ بِخَيْرِ أَعْمَالِكُمْ، وَأَزْكَاهَا عِنْدَ مَلِيكِكُمْ، وَأَرْفَعِهَا فِي دَرَجَاتِكُمْ، وَخَيْرٌ لَكُمْ مِنْ إِنْفَاقِ الذَّهَبِ وَالفِضَّةِ، وَخَيْرٌ لَكُمْ مِنْ أَنْ تَلْقَوْا عَدُوَّكُمْ فَتَضْرِبُوا أَعْنَاقَهُمْ وَيَضْرِبُوا أَعْنَاقَكُمْ؟)) قَالُوا : بَلَى: قَالَ: ((ذِكْرُ اللَّهِ تَعَالَى)) رواه الترمذي. قَال الحاكم أبو عبد الله: إسناده صحيح

Imepokelewa kutoka kwa Abu Ad-Dardaa(رضي الله عنه)   ambaye amesema: “Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Hivi niwaambieni khabari ya matendo yenu bora zaidi, na ambayo ni masafi mno mbele ya Rabb wenu, na ambayo ni ya juu mno katika daraja zenu, na ambayo ni bora kwenu kuliko kutoa dhahabu na fedha, na ambayo ni bora kuliko kukutana na adui zenu mkawapiga shingo zao, nao wakakupigeni shingo zenu?))  Wakasema [Maswahaba]: Ndio. Akasema ((Ni kumdhukuru Allaah Ta’aalaa)). [At-Tirmidhiy na amesema Abu ‘Abdillaah: Isnaad yake ni Swahiyh]

 

 

Mafunzo Na Mwongozo:

 

 

1. Fadhila za kumdhukuru Allaah (سبحانه وتعالى) ni nyingi, na hii ni miongoni mwazo za kupewa ujira adhimu.   Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

وَالذَّاكِرِينَ اللَّـهَ كَثِيرًا وَالذَّاكِرَاتِ أَعَدَّ اللَّـهُ لَهُم مَّغْفِرَةً وَأَجْرًا عَظِيمًا ﴿٣٥﴾

 Na wanaomdhukuru Allaah kwa wingi wanaume na wanawake; Allaah Amewaandalia maghfirah na ujira adhimu. [Al-Ahzaab (33: 35)]

 

 

 

2. Kumdhukuru Allaah (سبحانه وتعالى) kunasababisha utulivu wa moyo, furaha na amani. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

 

الَّذِينَ آمَنُوا وَتَطْمَئِنُّ قُلُوبُهُم بِذِكْرِ اللَّـهِ ۗ أَلَا بِذِكْرِ اللَّـهِ تَطْمَئِنُّ الْقُلُوبُ ﴿٢٨﴾

Wale walioamini na zikatua nyoyo zao kwa kumdhukuru Allaah. Tanabahi!  Kwa kumdhukuru Allaah nyoyo hutulia! [Ar-Ra’d (13: 28)]

 

 

Rejea pia: Aal-‘Imraan (2: 191-195), Al-Ahzaab (33: 41-44).

 

Rejea pia Hadiyth namba (84). 

 

 

 

3. Ukitaka Allaah (سبحانه وتعالى) Akukumbuke basi mdhukuru kwa wingi kama Anavyosema:

 

 اذْكُرُونِي أَذْكُرْكُمْ وَاشْكُرُوا لِي وَلَا تَكْفُرُونِ﴿١٥٢﴾

Basi nidhukuruni na Mimi Nitakukumbukeni; na nishukuruni wala msinikufuru. [Al-Baqarah (2: 152)]

 

 

4. Kudumisha kumdhukuru Allaah (سبحانه وتعالى) wakati wote, kwani kuna faida na manufaa mengi kwa Muislamu; faida hizo zimetajwa katika Hadiyth hiyo tukufu kuwa ni kuwa na daraja bora kabisa mbele ya Allaah (سبحانه وتعالى), na kwamba kumdhukuru Allaah (سبحانه وتعالى) kunashinda kutoa dhahabu na fedha katika njia ya Allaah na kwamba kuliko kupigana jihaad. 

 

 

 

5. Rahmah na fadhila za Allaah (سبحانه وتعالى) kuwapatia thawabu na kuwapandisha vyeo waja kwa kutenda ‘amali nyepesi kabisa inayohitaji ulimi pekee katika kumdhukuru.

 

 

 

6. Kumdhukuru Allaah (سبحانه وتعالى) kila wakati kutamzuia mtu kunena yasiyopasa; kutokufanya ghiybah (kusengenya), namiymah (kufitinisha), na kumzuia mtu kila aina ya maovu yanayotokana na ulimi.

 

 

 

7. Ulimi ni kiungo muhimu kabisa katika mwili wa bin Aadam, unaweza kumfikisha mtu Jannah au motoni.

 

 

 

8. Umuhimu wa kudumisha du’aa ya kuwezesha kumdhukuru Allaah (سبحانه وتعالى) inayosomwa baada ya Swalaah ambayo Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alimuusia Mu’aadh bin Jabal (رضي الله عنه):

 

عَنْ مُعَاذِ بْنِ جَبَلٍ، أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم أَخَذَ بِيَدِهِ وَقَالَ: ((يَا مُعَاذُ وَاللَّهِ إِنِّي لأُحِبُّكَ وَاللَّهِ إِنِّي لأُحِبُّكَ))‏.‏ فَقَالَ: ((أُوصِيكَ يَا مُعَاذُ لاَ تَدَعَنَّ فِي دُبُرِ كُلِّ صَلاَةٍ تَقُولُ: اللَّهُمَّ أَعِنِّي عَلَى ذِكْرِكَ وَشُكْرِكَ وَحُسْنِ عِبَادَتِكَ))‏ ‏.‏ وَأَوْصَى بِذَلِكَ مُعَاذٌ الصُّنَابِحِيَّ وَأَوْصَى بِهِ الصُّنَابِحِيُّ أَبَا عَبْدِ الرَّحْمَنِ ‏.‏

 

Imepokelewa kutoka kwa Mu’aadh bin Jabal (رضي الله عنه) kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alimshika mkono wake akasema: ((Ee Mu’aadh!  Wa-Allaahi mimi nakupenda! Wa-Allaahi mimi nakupenda!)) Akasema: ((Nakuusia ee Mu’aadh usiache kusema katika kila baada ya Swalaah:

 

 

اللّهُـمَّ أَعِـنِّي عَلـى ذِكْـرِكَ وَشُكْـرِك وَحُسْـنِ عِبـادَتِـك

Allaahumma A’inniy ’alaa dhikrika washukrika wahusni ’Ibaadatika

 

Ee Allaah nisaidie juu Kukudhukuru, na kukushukuru na kukuabudu kwa uzuri upasao. 

   [Hadiyth ya Mu’aadh bin Jabal (رضي الله عنه) - Abu Daawuwd (2/86), An-Nasaaiy (3/53) na ameisahihisha Al-Albaaniy (رحمه الله) katika Swahiyh Abi Daawuwd (1/284)].

 

 

 

9. Hima ya Maswahaba (رضي الله عنهم) kutaka kujua mambo kutoka kwa mwalimu wao mkuu; Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم).

 

 

10. Muislamu kutodharau kufanya jambo la kheri hata likionekana ni dogo katika nadharia ya mmoja wetu.

 

 

11. Rahmah ya Allaah (سبحانه وتعالى) kwa waja Wake kwa kuwapatia thawabu nyingi kwa jambo ambalo laonekana ni dogo sana.

 

 

 

 

Share