095-Lu-ulu-un-Manthuwrun: Kuepushwa Moto Na Kuingizwa Jannah Ni Kumwamini Allaah Na Kuwatendea Watu Analopenda Kutendewa
Lu-ulu-un-Manthuwrun
(Mkusanyiko Wa Hadiyth Mbali Mbali Na Mafunzo Yake)
Hadiyth Ya 95
Kuepushwa Moto Na Kuingizwa Jannah Ni Kumwamini Allaah
Na Kuwatendea Watu Analopenda Kutendewa
عَنْ عَبْدِ اللَّهِ بْنِ عَمْرٍو (رضي الله عنهما) قَال: قَال رَسُولُ الله صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: ((مَنْ أَحَبَّ أَنْ يُزَحْزَحَ عَنْ النَّارِ وَيَدْخُلَ الْجَنَّةَ فَلٍتَأْتِهِ مَنِيَّتُهُ وَهُوَ يُؤْمِنُ بِاللَّهِ وَالْيَوْمِ الآَخِرِ، وَالْيَاْتِ إِلَى النَّاسِ مَا يُحِبُّ أَنْ يُؤْتَى إِلَيْه)) مسلم
Imepokelewa kutoka kwa ‘Abdullaah bin ‘Amr (رضي الله عنهما) ambaye amesema: Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Anayependa aepushwe na moto na aingizwe Jannah, basi afanye hima mauti yake yamfikie ilihali anamwamini Allaah na Siku ya Mwisho, na awatendee watu analopenda kutendewa)). [Muslim]
Mafunzo Na Mwongozo:
1. Iymaan ni ufunguo wa kuingia Jannah. Basi Muislamu aamini nguzo zote sita za iymaan, ya kwanza kabisa ni kumwamini Allaah (سبحانه وتعالى). Nguzo hizo zimetajwa katika Hadiyth ndefu ya Jibriyl kumjia Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) kumuuliza maswali kadhaa akajibu kuhusu iymaan:
(أنْ تُؤمِنَ باللهِ، وَمَلائِكَتِهِ، وَكُتُبهِ، وَرُسُلِهِ، وَاليَوْمِ الآخِر، وتُؤْمِنَ بالقَدَرِ خَيرِهِ وَشَرِّهِ)). مسلم
((Ni kumwamini Allaah, Malaika Wake, Vitabu Vyake, Rasuli Wake na siku ya Qiyaamah, na kuamini Qadar (majaaliwa ya Allaah) ya kheri zake na shari zake)) [Muslim]
2. Iymaan pia imeambatana na kupendeleana kheri yale ambayo mtu anapendelea nafsi yake kama ilivyotajwa katika Hadiyth
عنْ أَنَسٍ (رضي الله عنه) عَنْ النَّبِيِّ (صلى الله عليه و آله وسلم) قَالَ: ((لاَ يُؤْمِنُ أَحَدُكُمْ حَتَّى يُحِبَّ لإِخِيهِ مَا يُحِبُّ لِنَفْسِهِ)) متفق عليه
Imepokelewa kutoka kwa Anas (رضي الله عنه) kwamba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Hatoamini mmoja wenu mpaka ampendelee nduguye anayojipendelea nafsi yake)) [Al-Bukhaariy na Muslim]
Rejea Hadiyth namba (21).
3. Uislamu umefunza kila jambo la kumwepusha mtu moto na la kumwingiza Jannah. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema katika Hadiyth:
عن عبد الله بن مسعود رضي الله عنه غن النبي صلى الله عليه وسلم: ((مَا تَرَكْتُ مِن شَيءٍ يُقَرِّبُكُمْ إِلى الجَنَّةِ إِلاَّ أَمَرْتُكُمْ بِهِ، وَلاَ مِن شيءٍ يُبعدُكُمْ عَنِ النَّارِ إِلاَّ نَهَيْتُكُمْ عَنْهُ))
Kutoka kwa ‘Abdullaah bin Mas-‘uwd (رضي الله عنه) kwamba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Sijaacha jambo lolote litakalokukurubisheni na Jannah isipokuwa nimekuamrisheni. Na wala lolote litakalokuepusheni na moto isipokuwa nimekukatazeni)) [Al-Haakim (2/5), Al-Bayhaqiy fiy Shu’ab Al-Iymaan (7/299), ameisahihisha Al-Albaaniy: As-Silsilah Asw-Swahiyhah (2866)]
4. Hatima ya bin Aadam ni ima Jannah au moto, na anayefaulu ni yule mwenye kuingia Jannah. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
كُلُّ نَفْسٍ ذَائِقَةُ الْمَوْتِ ۗ وَإِنَّمَا تُوَفَّوْنَ أُجُورَكُمْ يَوْمَ الْقِيَامَةِ ۖ فَمَن زُحْزِحَ عَنِ النَّارِ وَأُدْخِلَ الْجَنَّةَ فَقَدْ فَازَ ۗ وَمَا الْحَيَاةُ الدُّنْيَا إِلَّا مَتَاعُ الْغُرُورِ ﴿١٨٥﴾
Kila nafsi itaonja mauti. Na hakika mtalipwa kikamilifu ujira wenu Siku ya Qiyaamah. Basi atakayewekwa mbali na moto na akaingizwa Jannah kwa yakini amefuzu. Na uhai wa dunia si lolote ila ni starehe ya udanganyifu. [Aal-‘Imraan (4: 185)]
Rejea pia Huwd (11: 105-108), Ash-Shuwraa (42: 7).
5. Himizo la kutenda ‘amali njema na kudumisha hadi yamfikie mauti na hivyo ni kudiriki husnul-khaatimah (mwisho mwema).
6. Thibitisho la kauli ya Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم)
عَنْ مُعَاذِ بْنِ جَبَلٍ قَالَ : قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّه عَلَيْهِ وَسَلَّمَ : ((مَنْ كَانَ آخِرُ كَلامِهِ لا إِلَهَ إِلا اللَّهُ دَخَلَ الْجَنَّةَ)) رواه أبو داود ( 3116 ) وحسَّنه الألباني في " إرواء الغليل ( 3 / 149 ) .
Kutoka kwa Mu’aadh bin Jabal (رضي الله عنه) kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Atakayekuwa maneno yake ya mwisho ni Laa ilaaha illa Allaah ataingia Jannah)). [Abuu Daawuwd, Ahmad na ameisahihisha Al-Albaaniy katika Irwaa Al-Ghaliyl (3/149), Swahiyh Al-Jaami’ (6479), Swahiyh Abiy Daawuwd (3116)]
7. Mapendekezo na himizo la kutendeana wema baina ya Waislamu na kupendeleana kila aina za kheri na kuepushana shari.
Rejea Hadiyth namba (20), (21), (22), (23)
8. Sababu za kujiepusha na moto na kuingia Jannah ni nyepesi kabisa mtu kuzidiriki akiazimia kama anavyosema Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) .
عَنْ عَبْدِ اللَّهِ ـ رضى الله عنه ـ قَالَ قَالَ النَّبِيُّ صلى الله عليه وسلم ((الْجَنَّةُ أَقْرَبُ إِلَى أَحَدِكُمْ مِنْ شِرَاكِ نَعْلِهِ، وَالنَّارُ مِثْلُ ذَلِكَ)) البخاري
Kutoka kwa ‘Abdullaah (رضي الله عنه) amesema: Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Jannah iko karibu zaidi kwa mmoja wenu kuliko nyuzi za viatu vyake, na moto kama hivyo)). [Al-Bukhaariy]