097-Lu-ulu-un-Manthuwrun: Wanakhasimiana Hawataingia Jannah Hadi Wapatane Na Hawatapokelewa ‘amali Zao
Lu-ulu-un-Manthuwrun
(Mkusanyiko Wa Hadiyth Mbali Mbali Na Mafunzo Yake)
Hadiyth Ya 97
Wanaokhasimiana Hawataingia Jannah Hadi Wapatane Na Hawatapokelewa ‘Amali Zao
عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ: ((تُفْتَحُ أَبْوَابُ الْجَنَّةِ يَوْمَ الإثْنَيْنِ وَيَوْمَ الْخَمِيسِ، فَيُغْفَرُ لِكُلِّ عَبْدٍ لاَ يُشْرِكُ بِاللَّهِ شَيْئًا إِلاَّ رَجُلاً كَانَتْ بَيْنَهُ وَبَيْنَ أَخِيهِ شَحْنَاءُ، فَيُقَالُ: أَنْظِرُوا هَذَيْنِ حَتَّى يَصْطَلِحَا! أَنْظِرُوا هَذَيْنِ حَتَّى َصْطَلِحَا!)) مسلم وَفي رواية: ((تُعْرَضُ الأَعْماَلُ فِي كُلِّ يَوْمِ خَمِيسٍ واثْنِيْن)) وَذَكَرَ نَحْوَهُ
Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah(رضي الله عنه) kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Milango ya Jannah hufunguliwa kila siku ya Jumatatu na Alkhamiys, na ataghufuriwa kila mja asiyemshirikisha Allaah kwa chochote, isipokuwa mtu aliye na utesi baina yake na nduguye, hapo husemwa: “Waacheni hawa mpaka wapatane! Waacheni hawa mpaka wapatane!”)). [Muslim]
Katika Riwaayah nyingine: ((‘Amali hutandazwa kila siku ya Alkhamiys na Jumatatu)), na akataja kama hivyo. [Muslim]
Mafunzo Na Mwongozo:
1. Jannah imeharamishwa kwa ndugu waliokhasimiana.
2. Kukhasimiana ni maovu yaliyofananishwa na kumshirikisha Allaah (سبحانه وتعالى).
3. Muislamu anaweza kupoteza muda na nguvu zake kutenda ‘amali zisizopokelewa na Allaah (سبحانه وتعالى) kama Anavyosema:
وَقَدِمْنَا إِلَىٰ مَا عَمِلُوا مِنْ عَمَلٍ فَجَعَلْنَاهُ هَبَاءً مَّنثُورًا ﴿٢٣﴾
Na Tutayaendea yale waliyoyatenda ya ‘amali yoyote ile, Tutayafanya chembechembe za vumbi zinazoelea hewani zinazotawanyika. [Al-Furqaan (25: 23)].
4. Baadhi ya mas-alah watu wanayachukulia mepesi, lakini kumbe yana uzito mno mbele ya Allaah (سبحانه وتعالى), kama vile hali ilivyokuwa katika kisa cha ‘Ifk’ – kusingiziwa kashfa Mama wa Waumini ‘Aaisha (رضي الله عنها) Aliposema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَتَحْسَبُونَهُ هَيِّنًا وَهُوَ عِندَ اللَّـهِ عَظِيمٌ ﴿١٥﴾
na mnalidhania ni jambo jepesi; na hali hili mbele ya Allaah ni kubwa mno. [An-Nuwr: 15]
5. Wajibu wa Waislamu kusuluhisha waliokhasimiana ili wachume thawabu zake na wapate fadhila zake
Rejea An-Nisaa (4: 114), Al-Hujuraat (49: 10).
Rejea Hadiyth namba (24), (96).
6. Uislamu unasisitiza mno undugu, amani, na mapenzi baina ya Waislamu.