098-Lu-ulu-un-Manthuwrun: Dhana Mbaya Ni Mazungumzo Ya Uongo Kabisa
Lu-ulu-un-Manthuwrun
(Mkusanyiko Wa Hadiyth Mbali Mbali Na Mafunzo Yake)
Hadiyth Ya 98
Dhana Mbaya Ni Mazungumzo Ya Uongo Kabisa
عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ: ((إِيَّاكُمْ وَالظَّنَّ فَإِنَّ الظَّنَّ أَكْذَبُ الْحَدِيثِ)) متفق عليه
Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Tahadharini na dhana mbaya, kwani hakika dhana ni mazungumzo ya uongo kabisa)). [Al-Bukhaariy na Muslim]
Mafunzo Na Mwongozo:
1. Tahadharisho la kuwa na dhana mbaya ambayo inampeleka mtu kufikia maovu mengine ya kujasusi na ghiybah kama Anavyotahadharisha Allaah (سبحانه وتعالى):
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اجْتَنِبُوا كَثِيرًا مِّنَ الظَّنِّ إِنَّ بَعْضَ الظَّنِّ إِثْمٌ ۖ وَلَا تَجَسَّسُوا وَلَا يَغْتَب بَّعْضُكُم بَعْضًا ۚ أَيُحِبُّ أَحَدُكُمْ أَن يَأْكُلَ لَحْمَ أَخِيهِ مَيْتًا فَكَرِهْتُمُوهُ ۚ وَاتَّقُوا اللَّـهَ ۚ إِنَّ اللَّـهَ تَوَّابٌ رَّحِيمٌ﴿١٢﴾
Enyi walioamini! Jieupusheni sana na dhana kwani hakika baadhi ya dhana ni dhambi. Na wala msifanyiane ujasusi, na wala wasisengenyane baadhi yenu wengineo. Je, anapenda mmoja wenu kwamba ale nyama ya nduguye aliyekufa? Basi mmelichukia hilo! Na mcheni Allaah! Hakika Allaah ni Mwingi wa kupokea tawbah, Mwenye kurehemu. [Al-Hujuraat (59: 12)]
2. Dhana mbaya zinaweza kumfikisha mtu kuchuma dhambi kubwa inayoangamiza ya kusingizia uovu watu.
Rejea Hadiyth namba (87) (88), (89), (104).
3. Dhana mbaya imefananishwa na uongo wa hali ya juu kabisa, nayo ni aina ya maradhi ya moyo ya kufuata matamanio ya nafsi.
4. Shariy’ah za Kiislamu na adhabu zinahukumiwa kwa yakini na si kwa dhana tu. Na ndio maana wanatakiwa mashahidi wanne katika jambo la hadd (adhabu zilizowekwa katika Shariy’ah).
Rejea An-Nuwr (24: 4-9), An-Nisaa (4: 15).
5. Dhana mbaya inaleta vurugu na malumbano katika jamii, hivyo huchelewesha maendeleo.
6. Dhana mbaya pia huleta utesi baina ya watu.