118-Lu-ulu-un-Manthuwrun: Kutokuomboleza Kwa Kupiga Mashavu, Kupasua Mifuko Na Kuomba Maombi Ya Kijahilia
Lu-ulu-un-Manthuwrun
(Mkusanyiko Wa Hadiyth Mbali Mbali Na Mafunzo Yake)
Hadiyth Ya 118
Kutokuomboleza Kwa Kupiga Mashavu, Kupasua Mifuko Na Kuomba Maombi Ya Kijahilia
عَنْ عَبْد الله ابْن مَسْعُودٍ (رضي الله عنه) عَنْ النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ: ((لَيْسَ مِنَّا مَنْ ضَرَبَ الْخُدُودَ وَشَقَّ الْجُيُوبَ وَدَعَا بِدَعْوَى الْجَاهِلِيَّةِ)) متفق عليه
Imepokelewa kutoka kwa ‘Abdullaah bin Mas’uwd (رضي الله عنه) amesema: Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Si miongoni mwetu anayejipiga mashavu, akapasua mifuko na akaomba maombi ya kijahilia)). [Al-Bukhaariy na Muslim]
Mafunzo Na Mwongozo:
1. Makatazo ya kujipiga mashavu, kupasua mifuko au nguo, kuomboleza n.k.
2. Muislamu anapaswa aridhike na majaaliwa ya Rabb wake Anapomkidhia msiba, na si kuchukiwa, kwani huenda ikampeleka kukufuru. Aamini Qadhwaa na Qadar (Yaliyohukumiwa na Yaliyokadiriwa) na Allaah (سبحانه وتعالى) Yameshaandikwa katika Lawhum-Mahfuudhw [Ubao Uliohifadhiwa mbingu ya saba]. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
مَا أَصَابَ مِن مُّصِيبَةٍ فِي الْأَرْضِ وَلَا فِي أَنفُسِكُمْ إِلَّا فِي كِتَابٍ مِّن قَبْلِ أَن نَّبْرَأَهَا ۚ إِنَّ ذَٰلِكَ عَلَى اللَّـهِ يَسِيرٌ﴿٢٢﴾
Hausibu msiba wowote katika ardhi au katika nafsi zenu isipokuwa umo katika Kitabu kabla hatujautokezesha. Hakika hayo kwa Allaah ni mepesi.
لِّكَيْلَا تَأْسَوْا عَلَىٰ مَا فَاتَكُمْ وَلَا تَفْرَحُوا بِمَا آتَاكُمْ ۗ وَاللَّـهُ لَا يُحِبُّ كُلَّ مُخْتَالٍ فَخُورٍ ﴿٢٣﴾
Ili msisononeke juu ya yale yaliyokuondokeeni na wala msifurahie kwa yale Aliyokupeni (Allaah); na Allaah Hapendi kila mwenye kujinata, anayejifakharisha. [Al-Hadiyd (57: 22-23)]
3. Kuomboleza kwa sauti na kujipiga au kuchana nguo kunamuadhibisha maiti kaburini
Hadiyth: ((Maiti anaadhibika kaburini mwake kwa anayoombolezewa)). [Al-Bukhaariy na Muslim]
4. Anayeomboleza ataadhibiwa Siku ya Qiyaamah
Hadiyth: ((Mwombolezi asipotubia kabla ya kufa kwake, Siku ya Qiyaamah atavalishwa kanzu ya lami na deraya ya upele)). [Muslim]
5. Kuomboleza kwengine ni kunyoa kichwa kwa ajili ya msiba. Hii imekatazwa katika Hadiyth ifuatayo:
Wakati fulani Abuu Muwsaa aliugua na kuhisi maumivu makubwa, kwa maumivu hayo akazimia ilhali kichwa chake kipo chini ya uangalizi wa mwanamke mmoja katika jamaa zake, mwanamke yule baada ya kuona hali ya Abuu Muwsaa akapiga kelele kwa nguvu lakini Abuu Muwsaa hakuweza kusema kitu kwa hali aliyokuwa nayo, baada ya kuzindukana akasema, ‘Mimi najikosha kwa yale aliyojikosha Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) kwani Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alijikosha na haya yafuatayo (hakuyataka kabisa yatokee): Asw-Swaliqah; yaani mtu mwenye kunyanyua sauti yake kwa juu wakati wa msiba, na Al-Haaliqah; mwenye kunyoa nywele zake wakati wa msiba na Ash-Shaaqqah; anayerarua na kuchana nguo zake wakati wa kuomboleza.” [Al-Bukhaariy na Muslim]
6. Muislamu afuate mafunzo ya Sunnah katika msiba. Kulia kunaruhusiwa bila ya kutoa sauti na kuomboleza.