119-Lu-ulu-un-Manthuwrun: Anayemwendea Mtazamaji Ramli Akamsadiki Hatokubaliwa Swalaah Siku Arubaini

Lu-ulu-un-Manthuwrun

 

(Mkusanyiko Wa Hadiyth Mbali Mbali Na Mafunzo Yake)

 

Hadiyth Ya 119

 

Anayemwendea Mtazamaji Ramli Akamsadiki Hatokubaliwa Swalaah Siku Arubaini

 

 

 

عَنْ صَفِيَّةَ بِنْتِ أبِي عُبِيْدٍ عَنْ بَعْضِ أَزْوَاجِ النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ وَ (رضي الله عنهم) عَنْ النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ: ((مَنْ أَتَى عَرَّافًا فَسَأَلَهُ عَنْ شَيْءٍ لَمْ تُقْبَلْ لَهُ صَلاَةٌ أَرْبَعِينَ لَيْلَةً)) مسلم

Imepokelewa kutoka kwa Swafiyyah bint Abiy ‘Ubayd kutoka kwa baadhi ya wakeze Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) kwamba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Mwenye kumwendea mtazamiaji [mpiga ramli] akamwuliza jambo na akamsadiki, hatokubaliwa Swalaah yake siku arubaini)). [Muslim]

 

 

Mafunzo Na Mwongozo:

 

 

1. Haramisho la kuwaendea watabiri na makahini na kusadiki wayasemayo na kwamba Swalaah haitokubaliwa siku arubaini.

 

 

2. Kuna hatari kubwa ya kumsikiliza mtabiri au kahini na kumwamini, kwani kutamkosesha Muislamu thawabu za ‘amali njema kama Swalaah, kwani hiyo ni aina ya shirki kwa vile anaingilia elimu ya ghayb ya Allaah (سبحانه وتعالى) na hivyo humtoa mtu nje ya Uislamu kwa dalili ya Hadiyth zifuatazo:

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ رضي الله عنه عَنْ النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ : (( مَنْ أَتَى حَائِضًا أَوْ امْرَأَةً فِي دُبُرِهَا أَوْ كَاهِنًا فَقَدْ كَفَرَ بِمَا أُنْزِلَ عَلَى مُحَمَّدٍ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ))

((Mwenye kumuingia mwenye hedhi, au mwanamke kwa nyuma, au kumwendea mchawi na kumuamini kwa anayosema, basi amekufuru aliyoteremshiwa Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم)). [Abuu Daawuwd, At-Tirmidhiy, Ibn Maajah na isnaad yake ni Swahiyh]

 

Na pia:

 

مَنْ أَتَى كَاهِنًا أَوْ سَاحِرًا فَصَدَّقَهُ بِمَا يَقُولُ فَقَدْ كَفَر بِمَا أُنْزِلَ عَلى مُحَمَّدٍ صلى الله عليه وسلّم

Atakayemwendea kahini au mchawi akasadiki yale anayoyasema basi amekufuru ambayo Ameteremshiwa nayo Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم) [Tafsiyr Ibn Kathiyr; Hadiyth ina isnaad ya upokezi Swahiyh na kuna Hadiyth zinazokubaliana na hii].

 

 

3. Umuhimu wa kujifunza mas-alah ya hatari kama haya ambayo humtoa mtu katika Uislamu. Ni kwa kuwa, masuala haya ni dhambi Asizozisamehe Allaah (سبحانه وتعالى).

 

Rejea: An-Nisaa (4: 48, 116),  na kwamba anayemshirikisha Allaah (سبحانه وتعالى) ataharamishwa na kuingia katika Jannah, bali pia makazi yake yatakuwa ni ya motoni! Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 إِنَّهُ مَن يُشْرِكْ بِاللَّـهِ فَقَدْ حَرَّمَ اللَّـهُ عَلَيْهِ الْجَنَّةَ وَمَأْوَاهُ النَّارُ ۖ وَمَا لِلظَّالِمِينَ مِنْ أَنصَارٍ﴿٧٢﴾

Hakika mwenye kumshirikisha Allaah bila shaka Allaah Atamharamishia Jannah, na makazi yake yatakuwa ni motoni. Na madhalimu hawatopata yeyote mwenye kunusuru.” [Al-Maaidah (5: 72)]

 

Rejea pia Hadiyth namba (108), (136).

 

 

4. Wayasemayo watabiri yanayotokea kweli ni kwa kuwa wamepatiwa habari kutoka kwa majini wanaotega sikio, kisha kuyahamisha kwa wengine. Rejea: Al-Jinn (72: 6-10).

 

 

5. Ieleweke kuwa mbali na kutokubaliwa Swalaah siku arubaini, Muislamu aliyefanya kosa hilo ni lazima aswali. Kutoswali kwake ni dhambi nyingine kubwa.

 

 

Share