121-Lu-ulu-un-Manthuwrun: Misikiti Si Ya Kuchafuliwa Bali Ni Ya Kumdhukuru Allaah

Lu-ulu-un-Manthuwrun

 

(Mkusanyiko Wa Hadiyth Mbali Mbali Na Mafunzo Yake)

 

Hadiyth Ya 121  

 

Misikiti Si Ya Kuchafuliwa Bali Ni Ya Kumdhukuru Allaah

 

 

 

 

عَنْ أَنَس (رضي الله عنه) أَنَّ رَسُول اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قال: ((إِنَّ هَذِهِ الْمَسَاجِدَ لاَ تَصْلُحُ لِشَيْءٍ مِنْ هَذَا الْبَوْلِ وَلاَ الْقَذَرِ، إِنَّمَا هِيَ لِذِكْرِ اللَّهِ تَعَالى وَقِرَاءَةِ الْقُرْآنِ)) أوْ كَماَ قَالَ رَسُولُ الله  صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ -    مسلم

Imepokelewa kutoka kwa Anas (رضي الله عنه)  kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه  وآله وسلم ) amesema: ((Hakika hii Misikiti, haifai kukojoa wala kutia uchafu. Hakika imejengwa kwa ajili ya kumtaja Allaah na kusoma Qur-aan)) au kama alivyosema Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم).  [Muslim]

 

 

Mafunzo Na Mwongozo:

 

 

1. Haramisho la kukojoa Msikitini au kutupa uchafu wowote. Ikiwa ni wa najsi, basi haifai zaidi.

 

 

2. Ni wajibu kwa kila Muislamu kuhifadhi Misikiti, kwani ni sehemu inayofanywa ‘Ibaadah.

 

 

3. Kuhifadhi Misikiti kwa kila njia, usafi, amani na usalama baina ya watu n.k.

 

 

4. Haifai kupiga gumzo Msikitini wala kutenda lolote isipokuwa kuswali na kumdhukuru Allaah (سبحانه وتعالى) kwa usomaji wa Qur-aan, kumsabbih, kumhimidi Allaah (سبحانه وتعالى), kumtukuza n.k.

 

 

 

5. Kulinda Misikiti na kila ovu ni alama ya mapenzi ya Allaah (سبحانه وتعالى) na kuvitukuza vitukufu Vyake. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

 ذَٰلِكَ وَمَن يُعَظِّمْ حُرُمَاتِ اللَّـهِ فَهُوَ خَيْرٌ لَّهُ عِندَ رَبِّهِ

Ndio hivyo iwe na yeyote anayeadhimisha vitukufu vya Allaah basi hivyo ni kheri kwake mbele ya Rabb wake. [Al-Hajj (22: 30)]

 

Na pia Anasema (سبحانه وتعالى):

 

 ذَٰلِكَ وَمَن يُعَظِّمْ شَعَائِرَ اللَّـهِ فَإِنَّهَا مِن تَقْوَى الْقُلُوبِ ﴿٣٢﴾

 

Ndivyo hivyo, na yeyote anayeadhimisha Ishara za Allaah, basi hayo ni katika taqwa ya nyoyo. [Al-Hajj (22: 32)]

 

 

 

6. Kwa minajili hiyo, Muislamu anatakiwa awe ni mwenye kuondosha kohozi au uchafu wowote anaouona Msikitini pasi na kumngojea mtu maalumu kama mhudumu au msafishaji.

 

Hadiyth: Imepokewa kutoka kwa Abuu Dharr(رضي الله عنه)  kwamba Nabiy (صلى الله عليه  وآله وسلم) amesema: ((Nilionyeshwa ‘amali za Ummah wangu, nzuri na mbaya. Nikapata katika ‘amali zao nzuri ni udhia unaoondoshwa njiani. Na nikapata katika ‘amali zao mbaya kohozi linaloachwa Msikitini pasi na kuzikwa)). [Muslim]

 

 

 

 

Share