122-Lu-ulu-un-Manthuwrun: Haifai Kupandisha Sauti Za Mazungumzo Misikitini
Lu-ulu-un-Manthuwrun
(Mkusanyiko Wa Hadiyth Mbali Mbali Na Mafunzo Yake)
Hadiyth Ya 122
Haifai Kupandisha Sauti Za Mazungumzo Misikitini
عَنْ السَّائِبِ بْنِ يَزِيدَ الصَّحابيِّ (رضي الله عنه) قَالَ: كُنْتُ قَائِمًا فِي الْمَسْجِدِ، فَحَصَبَنِي رَجُلٌ، فَنَظَرْتُ فَإِذَا عُمَرُ بْنُ الْخَطَّابِ (رضي الله عنه)، فَقَالَ: اذْهَبْ فَأْتِنِي بِهَذَيْنِ، فَجِئْتُهُ بِهِمَا، قَالَ: مِنْ أَيْنَ أَنْتُمَا؟ قَالاَ: مِنْ أَهْلِ الطَّائِفِ. قَالَ: لَوْ كُنْتُمَا مِنْ أَهْلِ الْبَلَدِ لأوْجَعْتُكُمَا، تَرْفَعَانِ أَصْوَاتَكُمَا فِي مَسْجِدِ رَسُولِ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ! - البخاري
Imepokelewa kutoka kwa Swahaba, As-Saaib bin Yaziyd (رضي الله عنه) amesimulia: Nilikuwa Msikitini. Mtu mmoja akanirushia kijiwe. Nilipomtazama alikuwa ni ‘Umar bin Al-Khattwaab(رضي الله عنه) . Akaniambia: “Nenda ukaniletee watu wale wawili”. Nikaenda nikawaita. ‘Umar akawauliza: “Nyinyi mmekuja kutoka wapi?” Wakamjibu: “Tunakutoka Twaaif” Akawaambia: “Lau mngelikuwa ni wenyeji wa mji huu, ningaliwapiga! Mnazinyanyua sauti zenu katika Msikiti wa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم)?” [Al-Bukhaariy]
Mafunzo Na Mwongozo:
1. Makatazo ya kupandisha sauti Msikitini hata ikiwa ni kwa kusoma Qur-aan au kumdhukuru Allaah (سبحانه وتعالى). Na inakuwa haraam inapokuwa inaleta tashwishi au mabishano.
2. Muislamu anatakiwa aifanye sauti yake wastani katika ‘Ibaadah. Anaamrisha hivyo Allaah (سبحانه وتعالى):
وَلَا تَجْهَرْ بِصَلَاتِكَ وَلَا تُخَافِتْ بِهَا وَابْتَغِ بَيْنَ ذَٰلِكَ سَبِيلًا ﴿١١٠﴾
Na wala usisome kwa jahara Swalaah yako na wala usiifiche kimya kimya, bali shika njia (ya wastani) baina yake. [Al-Israa (17: 110)]
Na pia Rejea: Al-A’raaf (7: 55)
3. Inakuwa ni vizuri kumuashiria mtu Msikitini au kumtupia kitu kwa ajili ya kumtanabahisha jambo badala ya kutoa sauti.
4. Wajibu wa kutekeleza adabu za Msikitini zikiwemo kutokupandisha sauti, kutokuzozana, mijadala n.k.
5. Kuamrisha mema na kukataza maovu mahali popote khasa Msikitini ambako ni mahali patukufu kabisa wanapokusanyika Waislamu kwa ‘Ibaadah zao.
6. Inaruhusiwa kiongozi kumuadhibu kwa kumpiga mtu anayekwenda kinyume na shariy’ah za Dini.
7. Jukumu la kiongozi kuzuia maovu yanayotendwa popote.
Rejea Hadiyth namba (27).
8. Kutokuwaadhibu au kuwasamehe wageni wanaotenda maovu ambayo hayakuwekewa adhabu maalumu na shariy’ah katika mji usio wao bila ya kujua.
9. Nyumba za Allaah (سبحانه وتعالى) ni kwa ajili ya ‘Ibaadah na utiifu, hivyo inabidi kutekeleza humo yanayoamrishwa, kuepukana na yanayokatazwa kama yaliyotajwa juu, kufanya biashara n.k.
Rejea: An-Nuwr (24: 36-38).
10. Kutukuza vitukufu vya Allaah (سبحانه وتعالى) ni dalili ya taqwa na mapenzi ya Dini yetu hii ya Kiislamu tukufu.
Rejea: Al-Hajj (22: 30, 32).