128-Lu-ulu-un-Manthuwrun: Amelaaniwa Mke Anayemkatalia Mumewe Kujimai Bila Ya Sababu
Lu-ulu-un-Manthuwrun
(Mkusanyiko Wa Hadiyth Mbali Mbali Na Mafunzo Yake)
Hadiyth Ya 128
Amelaaniwa Mke Anayemkatalia Mumewe Kujimai Bila Ya Sababu
عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: ((إِذَا دَعَا الرَّجُلُ امْرَأَتَهُ إِلَى فِرَاشِهِ فَأَبَتْ فَبَاتَ غَضْبَانَ عَلَيْهَا لَعَنَتْهَا الْمَلآئِكَةُ حَتَّى تُصْبِحَ)) متفق عليه وَفي رواية: ((حَتَّى تَرْجِعَ))
Imepokelewa kutoka kwa Abu Hurayrah (رضي الله عنه) amesema: Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم ) amesema: ((Mwanamume atakapomwita mkewe kitandani [ili ajimae naye] akakataa, akalala [mume huyo] akiwa amemkasirikia [mkewe], Malaika watamlaani [mke huyo] mpaka apambaukiwe)). [Al-Bukhaariy na Muslim]. Na katika riwaayah: ((Mpaka arejee).
Mafunzo Na Mwongozo:
1. Mke anapaswa kutimiza haki ya mume kwa kumuitikia anapomhitaji kitandani. Isipokuwa tu anapokuwa katika hali ya hedhi, kwani hilo limekatazwa na Allaah (سبحانه وتعالى) kama Anavyosema:
وَيَسْأَلُونَكَ عَنِ الْمَحِيضِ ۖ قُلْ هُوَ أَذًى فَاعْتَزِلُوا النِّسَاءَ فِي الْمَحِيضِ ۖ وَلَا تَقْرَبُوهُنَّ حَتَّىٰ يَطْهُرْنَ ۖ فَإِذَا تَطَهَّرْنَ فَأْتُوهُنَّ مِنْ حَيْثُ أَمَرَكُمُ اللَّـهُ ۚ إِنَّ اللَّـهَ يُحِبُّ التَّوَّابِينَ وَيُحِبُّ الْمُتَطَهِّرِينَ ﴿٢٢٢﴾
Na wanakuuliza kuhusu hedhi. Sema: “Hiyo ni dhara; basi waepukeni wanawake katika hedhi. Wala msiwakaribie kujimai nao mpaka watwaharike. Watakapotwaharika basi waendeeni kupitia pale Alipokuamrisheni Allaah.” Hakika Allaah Anapenda wenye kutubia na Anapenda wenye kujitwaharisha [Al-Baqarah (2: 222)]
Na Hadiyth kadhaa zimekataza mume kujimai na mke mwenye hedhi; miongoni mwazo ni:
“Mwenye kumuingia mwenye hedhi au mwanamke kwenye dubur (uchi wa nyuma) au kumwendea mtabiri na kumuamini kwa anayosema basi amekufuru kwa aliyoteremshiwa Muhammad.” [Swahiyh At-Tirmidhiy (135), Swahiyh Ibn Maajah (528), As-Silsilah Asw-Swahiyhah (7/1130)].
Lakini mume anaruhusika kustarehe na mkewe isipokuwa kujimai kwa dalili ya Hadiyth:
عن أنس رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ أَنَّ الْيَهُودَ كَانُوا إِذَا حَاضَتِ الْمَرْأَةُ؛ لَمْ يُؤَاكِلُوهَا. فَقَالَ النَّبِيُّ -صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: ((اصْنَعُوا كُلَّ شَيْءٍ إِلاَّ النِّكَاحَ)) رَوَاهُ مُسْلِمٌ
Imepokelewa kutoka kwa Anas (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba Mayahudi walikuwa hawali na mwanamke anapokuwa katika hedhi. Lakini Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: ((Fanyeni naye kila jambo isipokuwa kujimai)) [Muslim]
Ama katika hali ya ugonjwa au machofu makali, mume anapaswa kumvumilia mkewe katika hali hiyo. Na mke anapokuwa katika Swawm ya Ramadhwaan, hapasi kumtii mumewe kumkubalia kujimai naye.
2. Mwanamke asipomkidhia mumewe haja yake ya kitendo cha ndoa, anastahiki adhabu ya kulaaniwa na Malaika mpaka akiamka asubuhi. Hii inadhihirisha jinsi gani umuhimu wa jambo hili, kwani litaweza kumzuia mume asitoke nje kutenda maasi ya zinaa.
3. Mwanamume kawaida ni mwenye matamanio zaidi ya kitendo cha ndoa kuliko mwanamke, na ni hikma ya Allaah (سبحانه وتعالى) kuwaumba kila mmoja kwa kutofautiana mwili, matamanio n.k. Na ndio maana akakatazwa mwanamke kufunga Swawm za Sunnah bila ya ruhusa ya mumewe.
Rejea Hadiyth namba (30).
4. Tahadharisho hili la mke kumkatalia mume kujimai naye bila ya sababu inayoruhusika ki-shariy’ah njia kubwa kwa Uislamu kufunga mlango wa shari, kwani kiubinaadamu, mtu akiwa ana hasira anaweza kutoa talaka na hivyo nyumba kuvunjika. Au pia ikiwa shauku ya mwanamme ni kubwa, anaweza kuzini, na hivyo kuvunja mahusiano mema na mkewe na hata pengine kumletea ugonjwa mbaya unaotokana na kuzini nje.