129-Lu-ulu-un-Manthuwrun: Haifai Kutia Chokaa Makaburi Au Kujengea Au Kukalia
Lu-ulu-un-Manthuwrun
(Mkusanyiko Wa Hadiyth Mbali Mbali Na Mafunzo Yake)
Hadiyth Ya 129
Haifai Kutia Chokaa Makaburi Au Kujengea Au Kukalia
عَنْ جَابِرٍ (رضي الله عنه) قَالَ: نَهَى رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ أَنْ يُجَصَّصَ الْقَبْرُ وَأَنْ يُقْعَدَ عَلَيْهِ وَأَنْ يُبْنَى عَلَيْهِ. مسلم
Imepokelewa kutoka kwa Jaabir (رضي الله عنه) amesema: Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amekataza kaburi kutiwa chokaa (liwe imara), kuketiwa juu yake na kujengewa. [Muslim]
Mafunzo Na Mwongozo:
1. Makatazo ya kupaka kaburi chokaa au kutia alama yoyote ile. Na kuzidisha inapovuka mipaka ya kulipamba huwa ni haraam.
2. Uharamisho wa kuketi juu ya kaburi, kwani hivyo ni utovu wa adabu juu ya maiti kama alivyosema Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) ((Msiswali juu ya makaburi wala msiketi juu yake)). [Muslim]
Rejea Hadiyth namba (83), (137).
3. Kuyajengea makaburi hatimaye kutapelekea watu kuyatukuza na kufanya mahali pa ‘Ibaadah, jambo liloharamishwa. Ni kama vile Aswhabul-Kahf (watu wa pangoni) walivyofanyiwa na watu baada ya kufariki kwao:
وَكَذَٰلِكَ أَعْثَرْنَا عَلَيْهِمْ لِيَعْلَمُوا أَنَّ وَعْدَ اللَّـهِ حَقٌّ وَأَنَّ السَّاعَةَ لَا رَيْبَ فِيهَا إِذْ يَتَنَازَعُونَ بَيْنَهُمْ أَمْرَهُمْ ۖ فَقَالُوا ابْنُوا عَلَيْهِم بُنْيَانًا ۖ رَّبُّهُمْ أَعْلَمُ بِهِمْ ۚ قَالَ الَّذِينَ غَلَبُوا عَلَىٰ أَمْرِهِمْ لَنَتَّخِذَنَّ عَلَيْهِم مَّسْجِدًا ﴿٢١﴾
Na hivyo ndivyo Tulivyowatambulisha kwa watu ili wajue kwamba ahadi ya Allaah ni haki. Na kwamba Saa haina shaka yoyote humo. Pale walipozozana baina yao kuhusu jambo lao. Wakasema: “Jengeni jengo juu yao; Rabb wao Anawajua vyema.” Wakasema wale walioshinda katika shauri lao: “Bila shaka tutajenga msikiti juu yao.” [Al-Kahf 18: 21)]
Makatazo ya Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) pia katika Hadiyth kadhaa zikiwemo:
((Hakika watu waovu kabisa watakaokutana na alama za Qiyaamah ni wale wanaofanya makaburi kuwa ni Misikiti [mahali pa ‘Ibaadah])). [Ahmad na amesimulia Abu Haatim katika Swahiyh yake]
Na pia Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Allaah Awalaani Mayahudi na Manasara, kwani wamefanya makaburi ya Manabii wao kuwa ni sehemu za ‘ibaadah.)) [Imesimuliwa na Al-Bukhaariy na Muslim].
4. Makatazo ya kujengea kaburi kwa vile ni mila za kikafiri na upotezaji wa mali kwa jambo lisilopasa. Na kujengewa pia kutasababisha watu wengine kutopata nafasi ya kuzikwa makaburini.
5. Muislamu anapaswa kupewa heshima yake hata baada ya kufariki kwake na kutomfanyia mambo yanayokatazwa katika Shariy’ah.