Naombeni Ushauri Wa Kuinusuru Na Kuimarisha Ndoa Yangu

SWALI

Mimi ni mwanamke mwenye umri wa miaka 30 ninaeishi Mombasa mjini Zanzibar, bado sijaolewa kwa muda huu, Allah akipenda natarajia kufunga ndoa mfunguo sita mwaka huu (2006) sasa ninachokiomba unipe elimu kupitia kwenye Qur-aan na Hadith za mtume ili niweze kuinusuru ndoa yangu na nia yangu nataka kufanya yote kwa mume kwa ajili ya Allah


 

JIBU:

AlhamduliLLaah - Himdi Na Sifa Zote Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

Kwanza kabisa ukitaka nyumba yako iimarike, inakulazimu uzifahamu haki zako kwa mume wako, na mume wako nae analazimika kuzifahamu haki zake kwako.

Baadhi ya haki za Mume kwa Mke:

1. Unatakiwa mwanamke wa Kiislamu umtii mume wako kwa kila anachokuamrisha

Uzindushi: huo utiifu unatakiwa usiambatane na aina yoyote ya kumuasi Allaah ndani yake, kama vile mume kumuamuru mke wake avue hijabu, au aache kuswali, au kutaka kumjamii akiwa ndani ya siku zake, au akataka kumlawiti, n.k

Amesema Mtume (Swalla Allahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) "Si ruhusa kufanya utiifu katika jambo la kumuasi Allaah, Hakika ya utiifu unatakiwa ufanyike katika mambo yaliyo mema pekee" Al- Bukhaariy na Muslim

 

2. Mwanamke wa Kiislamu unatakiwa ukae nyumbani, na usitoke ila kwa ruhusa ya mume

Allaah Anasema: "Na kaeni majumbani mwenu, wala msioneshe mapambo yenu kama walivyokuwa wakionesha mapambo yao wanawake wa zama za ujinga" Al-Ahzaab: 33

 

3. Mwanamke wa Kiislamu unatakiwa umtii mumeo pindi anapokuita kitandani

 

4. Usimruhusu yeyote kuingia ndani ya nyumba ya mumeo ila kwa ruhusa yake

 

5. Usifunge Swawm ya Sunnah wakati mumeo yupo mjini ila kwa ruhusa yake

Anasema Mtume (Swalla Allahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), "Si halali kwa mwanamke kufunga (Swawm ya Sunnah) na mumewe akiwa yupo mjini ila kwa ruhusa yake, na wala asiruhusu kuingia ndani ya nyumba ya mume wake ila kwa ruhusa yake

 

6. Usitoe chochote katika miliki ya mumeo illa kwa ruhusa yake:

Anasema Mtume (Swalla Allahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), "Hana ruhusa mwanamke yeyote kutoa kitu chochote kutoka kwenye nyumba ya mume wake ila kwa idhini yake" Abu Dawuud  na Tirmidhiy

 

7. Unatakiwa umuhudumie mumeo pamoja na watoto wake kwa kutoa huduma za nyumbani

 

8. Unatakiwa umuhifadhi mumeo kwa kumlindia heshima yake, mali yake na watoto wake

 

9. Unatakiwa umshukuru mumeo na wala usiukanushe wema wake, na utangamane nae kwa wema

 

Anasema Mtume (Swalla Allahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) " Allaah Hatomuangalia mwanamke asiye mshukuru mumewe na kutoridhika nae" An-Nasaaiy

 

10. Ujipodoe na ujirembe kwa ajili ya mumeo

 

11. Usijikweze endapo utamsaidia yeye na watoto wake kutoka katika mali yako

 

12. Unatakiwa uridhike na kidogo, na utosheke nacho, na wala usimlazimishe zaidi ya uwezo wake

 

Anasema Allaah Subhaanahu wa Ta'ala: "Na atoe mwenye wasaa kwa kadiri ya wasaa wake; na yule ambae amepungikiwa riziki yake, atoe katika kile alichopewa na Allaah. Allaah Hamkalifishi mtu yoyote ila kwa kadiri ya alichompa atajaalia Allaah baada ya dhiki faraja." At-Twalaaq :7

 

13. Usifanye jambo litakalomuudhi na kumkasirisha

 

14. Unatakiwa uishi na wazazi na ndugu wa mume kwa wema

 

15. Ujitahidi udumu na mumeo, wala usiombe talaka pasi na sababu za kisheria

 

16. Unatakiwa ujiepushe na mapambo pindi utakapofiwa na mumeo kwa muda wa miezi minne na siku kumi

 

Baadhi ya haki za mke kwa mume: 

1. Kuishi na mke kwa wema

 

Anasema Allaah Subhaanahu wa Ta'ala, "Naishini nao kwa wema…" An-Nisaa: 19

 

Na anasema tena Allaah Subhaanahu wa Ta'ala: "Na Wanawake nao wanayo haki ya kufanyiwa wema na waume zao"  Al-Baqarah: 228

 

2, 3, 4 -  Kumlisha, kumvisha, na kumpa makazi mnasaba

 

5. Kuwa mpole kwa mke, kucheza nae na kuutilia maanani udogo wa umri wake

 

6. Akeshe pamoja na mke wake wakisimuliana khabari mbalimbali.

 

7. Amuelimishe mambo yanayoihusu dini yake na amuhimize katika utiifu

 

8. Ayafumbie macho baadhi ya makosa yake iwapo hayaikiuki sheria ya Allaah.

 

9. Wala asimkere kwa kumpiga usoni au kumkashifu

 

10. Asimuhame pindi anapomuhama-ila iwe ndani ya nyumba yake

 

11. Amuhifadhi kwa maneno na vitendo

 

12. Endapo utaombwa ruhusa kwenda kuwatembelea ndugu na jamaa na ukawa na uhakika wa usalama wa huko aendako, unatakiwa umruhusu

 

13. Hutakiwi kutaja siri za mkeo na kuenenza dosari zake

 

14. Mume nae anatakiwa ajipambe kwa ajili ya mke wake, kama ambavyo mke hutakiwa kujipamba kwa ajili mume wake

 

15. Anatakiwa awe na dhana njema juu ya mke wake

 

16. Endapo mume ana mke zaidi ya mmoja, anatakiwa awe muadilifu katika kugawanya chakula, mavazi, makazi, malazi, n.k

 

Haya na mengineyo mkiyatimiza nyumba yenu itaimarika In Shaa Allaah.

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share