Kumuoa Mkristo Atakayesilimu Siku Ya Ndoa
SWALI:
Je inakubalika kumuoa Mkiristo atakaesilimu siku ya ndoa?
JIBU:
Sifa zote njema anastahiki Allah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.
Hakuna tatizo lolote endapo atasilimu kidhati, Imepokewa kutoka kwa Anas amesema: Abu Twalha alipomuoa Ummu Sulaym, mahari yao ilikuwa ni kusilimu, Ummu Sulaym alisilimu mwanzo kabla ya Abu Twalha, alipomchumbia, akasema kwa hakika mimi nimeshasilimu, ikiwa utasilimu utanioa, akasilimu na ikawa kusilimu ndiyo mahari yao" (An-Nasaaiy 6/114).
Lakini Muislamu mwanamume awe makini na mwanamke mwenye kutaka kusilimu siku ya ndoa, isijekuwa ni mwenye kumdanganya akawa anasubiri siku hiyo wakati ameshatayrisha mambo ya harusi kisha amgeukie. Ikiwa hili ndilo sharti aliloliweka huyo mwanamke basi nasiha yetu ni kuwa uwe makini na ujaribu kuchunguza kwanza dhamira yake.
Na Allaah Anajua zaidi