Amemuoa Mkristo Bila Kufuata Sheria Za Kiislamu Hataki Kuingia Katika Uislamu Nini Hukmu Yake Na Watoto Watakaozaa?

SWALI:

 

kama mtu atakuwa kaowa mwanamke wa kinasara nakuowa yenyewe sio kwa kiislam ni kwa kupitia marage regester office, kwa mfano kama hapa England. Swali langu ni hili je mke kama huyu inafaa mtu kusema au kuhisabiwa kaowa? Na kama utazaa nae hukumu yake itakuwaje kidini? Na vile vile kama kakataa kuufata uislam anataka kubakia na unasara wake mwanamke kama huyu je inafaa kuendelea kukaanae? Nitashukuru nikipata majibu kutoka kwenu ndugu zangu. Asalam alaikum warahmatullah wabarakatu.

 


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu swali lako la kuoa mwanamke wa kinasara. Uislamu umemruhusu mwanamme kumuoa mwanamke wa kinasara. Hii ni kwa mujibu wa kauli ya Aliyetukuka:

 

"Na mmehalalishiwa kuwaoa wanawake wema wa Kiislamu na wanawake wema katika wale waliopewa Kitabu kabla yenu. Ni halali kwenu kuwaoa mtakapowapa mahari yao, mkafunga nao ndoa, bila kufanya uzinzi wala kuwaweka kinyumba" (5: 5).

 

Katika Aayah iliyo juu tunapata mafunzo mazuri na mema katika kuoa wanawake waliopewa Kitabu. Miongoni mwayo ni:

  1. Wanawake hao ni lazima wawe ni wema, waliojihifadhi ambao hawana tabia ya uzinifu wala kuzungunga zunguka.

  2. Mfunge nao ndoa kwa njia ya Kiislamu.

  3. Msifanye nao uzinzi kabla ya kuwaoa.

  4. Msiwaweke kinyumba kabla ya ndoa.

Ikiwa mwanamke atakuwa na sifa hiyo ya kujihifadhi na kuwa mwema basi itaruhusiwa kwako kisheria kumuoa. Ikiwa hatakuwa na sifa hiyo basi hujapatiwa idhini ya kumuoa bali inafaa utafute Muislamu.

 

Nukta ya pili ndio ni jibu la swali lako, haifai kwa Muislamu kufunga ndoa na Mnasara Kanisani au kwa Marriage Register Office kwani ndoa hiyo haitambulikani kisheria. Bali inafaa ufunge kwa njia ya Kiislamu ambayo inakuamuru wewe umfanyie wema wa hali ya juu wala usimlazimishe kuingia katika Uislamu na umpatie mahari yake.

 

Ikiwa haikufungwa kwa njia ya Kiislamu aliyeoa kwa Ofisi ya Registrar, hatakuwa ni mkewe kisheria, hivyo watoto atakaozaa naye hawatambulikana kisheria kuwa ni wake. Hapa tungependa kuwatanabahisha ndugu zetu wasiwe ni wenye kuoa wanawake wa Kinasara au Kiyahudi kwani tukifanya hivyo, mwanzo wasichana wetu wataolewa na nani? Je, tunataka waolewe na John na Joseph au ni vipi? Kisha yapo matatizo mengi ambayo tunakumbana nayo pindi kunapotokea talaka kwa sababu tuko katika nchi ambazo sheria zake si za Kiislamu watoto ima anapewa mama au wanachukuliwa na serikali hivyo kuongeza idadi ya wasiokuwa Waislamu kwa nguvu na juhudi zetu.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share