Binti Mwenye Kufanya Maasi Ya Zinaa

SWALI:

Asalaam alaykum warahmatullah wabarakatuh,

JE NI SAWA HUYU NDUGU YANGU WA KIISLAM ANAVYOFANYA?ALINIJIA RAFIKI YANGU KUNIOMBA USHAURI AFANYAJE ILI AWEZE KUEPUKANA  NA JAMBO HILO.'' ALISEMA YEYE KILA MWENZI ANAHISI KUFANYA TENDO LA NDOA NA BADO BINTI HAJAOLEWA ANAMIAKA 24 ,HAWEZI KUMUASI ALLAH( S.W) KWA KUFANYA ZINAA ILA INAMPELEKEA KUFANYA KITENDO KIBAYA NA ANAHISI NI KAMA AMEKARIBIA ZINAA"Mimi nilimwambia aswali rakaa mbili amuombe ALLAH(S.W) msaada ila alisema kashafanya na bado hali ilimrudia je kunafatwa gani iliaweze kuepukana na hali hiyo?

 

 

 


 

 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukran ndugu yetu kwa swali lake nyeti na tatizo sugu katika jamii yetu. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anatuelezea kuwa zipo aina nyingi ya zinaa ila kile kitendo cha mwisho cha kufanya jimai ndicho chenye kuyakinisha. Macho yanazini kutazama maasiya, miguu kwa kutembea kwenye maasiya hayo, mikono kwa kushika, ulimi kwa kuzungumza na kadhalika. Allah Aliyetukuka Naye Anatuambia: “Wala msikaribie zinaa. Hakika hiyo zinaa ni uchafu na ni njia mbaya kabisa” (17: 32). Hii ina maana kuwa kitu chochote kinachokupeleka karibu na zinaa ni zinaa.

Kutamani kufanya tendo la zinaa au kumtamani mtu wa jinsia nyingine huwa mtu amekaribia zinaa na anapata dhambi kwa hilo. Japokuwa mwenye kutamani hivyo huwa hana adhabu ya kisheria mpaka afanye kitendo chenyewe lakini hiyo ni hatari kwani inaweza kumuingiza katika jimai kisha ikawa ni hasara kubwa hapa duniani kwa pengine kuambukizwa ukimwi, kuvunja heshima yake, kuharibu jamii, kubomoa maadili, na kesho Akhera adhabu kali zaidi.

Tunataka kutanabahisha hapa kuwa hakuna Swalah maalumu ya mtu kujikinga na madhambi ya zinaa au madhambi mengine. Hakika ni kuwa Swalah za faradhi na za Sunnah nyengine zikiswaliwa sawasawa inavyotakikana zinamkinga mtu na maasiya hayo. Hili ni kwa mujibu wa kauli ya Aliyetukuka: “Na simamisha Swalah. Bila shaka Swalah (ikiswaliwa vilivyo) humzuiliya na machafu na maovu” (29: 45). Machafu ni amali mbaya kabisa ikiwemo uasherati na zinaa.

Nasaha ambayo tunaweza kukupatia ni kumshauri aolewe haraka ili aepukane na tatizo hilo. Ikiwa hatafanya hivyo basi ataingia katika shimo la zinaa na hataweza kutoka kirahisi. Mshauri atumie muda wake vizuri kwa kusoma Qur-aan pamoja na maana yake na kujaribu kuzingatia mafunzo ndani yake na kutekeleza amri zilizomo ndani. Ajaribu kumdhukuru Allah kwa wingi, aongeze Ibadah za Sunnah kama Swalah na funga, amuombe Allah (Subhaanahu wa Ta’ala) Amuepushie balaa hiyo. Swalah ya usiku mja anakuwa karibu zake na Mola wake Mlezi, hivyo ajaribu kuinuka na kulia kwa Allah (Subhaanahu wa Ta’ala) Amuondoshee tatizo hilo na InshaAllah litamuondokea kabisa.

Pia ajiepushe na yale yote ambayo yanamkurubisha na hali hiyo ya matamanio, kama kutazama sinema zenye uchafu, kutazama picha za uchi na sinema zake kwenye mtandao (internet), kuzungumzia mambo hayo na mtu/watu, aku kwenye simu n.k.

Nasi hapa tunakuombea tawfiyq wewe na yeye katika ‘amali hiyo ya kumnasihi huyo dada yetu na pia yeye kuepukana na maasiya hayo.

Na Allaah Anajua zaidi.

 

 

 

Share