015 - Al-Hijr

 

الْحِجْر

 

015-Al-Hijr

 

015-Al-Hijr: Utangulizi Wa Suwrah

 

Alhidaaya.com

 

 

بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرّحِيمِ

 

 

الر ۚ تِلْكَ آيَاتُ الْكِتَابِ وَقُرْآنٍ مُّبِينٍ ﴿١﴾

1. Alif Laam Raa.[1] Hizi ni Aayaat za Kitabu na Qur-aan iliyo bayana.

 

 

 

رُّبَمَا يَوَدُّ الَّذِينَ كَفَرُوا لَوْ كَانُوا مُسْلِمِينَ ﴿٢﴾

2. Watatamani wale waliokufuru lau wangelikuwa Waislamu.

 

 

 

ذَرْهُمْ يَأْكُلُوا وَيَتَمَتَّعُوا وَيُلْهِهِمُ الْأَمَلُ ۖ فَسَوْفَ يَعْلَمُونَ ﴿٣﴾

3. Waache wale na wastarehe na yawashughulishe matumaini (ya uongo), basi watakuja kujua.

 

 

 

وَمَا أَهْلَكْنَا مِن قَرْيَةٍ إِلَّا وَلَهَا كِتَابٌ مَّعْلُومٌ ﴿٤﴾

4. Na Hatukuangamiza mji wowote isipokuwa ulikuwa na majaaliwa yaliyokadiriwa maalumu.

 

 

 

مَّا تَسْبِقُ مِنْ أُمَّةٍ أَجَلَهَا وَمَا يَسْتَأْخِرُونَ ﴿٥﴾

5. Ummah wowote hauwezi kutangulia muda wake (wa kuangamizwa) wala hauwezi kuakhirisha.

 

 

 

وَقَالُوا يَا أَيُّهَا الَّذِي نُزِّلَ عَلَيْهِ الذِّكْرُ إِنَّكَ لَمَجْنُونٌ ﴿٦﴾

6. Na wakasema: Ee ambaye umeteremshiwa Adh-Dhikru (Qur-aan)! Hakika wewe ni majnuni tu.

 

 

 

لَّوْ مَا تَأْتِينَا بِالْمَلَائِكَةِ إِن كُنتَ مِنَ الصَّادِقِينَ ﴿٧﴾

7. Mbona basi usituletee Malaika ikiwa wewe ni miongoni mwa wakweli?

 

 

 

مَا نُنَزِّلُ الْمَلَائِكَةَ إِلَّا بِالْحَقِّ وَمَا كَانُوا إِذًا مُّنظَرِينَ ﴿٨﴾

8. Hatuteremshi Malaika isipokuwa kwa jambo la haki, na hawatokuwa hapo wenye kupewa muhula.

 

 

 

إِنَّا نَحْنُ نَزَّلْنَا الذِّكْرَ وَإِنَّا لَهُ لَحَافِظُونَ ﴿٩﴾

9. Hakika Sisi Tumeteremsha Adh-Dhikra (Qur-aan) na hakika Sisi bila shaka Ndio Wenye Kuihifadhi.[2]

 

 

 

وَلَقَدْ أَرْسَلْنَا مِن قَبْلِكَ فِي شِيَعِ الْأَوَّلِينَ ﴿١٠﴾

10. Na kwa yakini Tulipeleka (Rusuli) kabla yako (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) katika makundi ya (nyumati za) awali.

 

 

 

وَمَا يَأْتِيهِم مِّن رَّسُولٍ إِلَّا كَانُوا بِهِ يَسْتَهْزِئُونَ ﴿١١﴾

11. Na hakuwafikia Rasuli yeyote ila walikuwa wakimfanyia istihzai.

 

 

 

كَذَٰلِكَ نَسْلُكُهُ فِي قُلُوبِ الْمُجْرِمِينَ ﴿١٢﴾

12. Hivyo ndivyo Tunavyoingiza hilo (istihzai, kadhibisho) katika nyoyo za wahalifu.  

 

 

 

لَا يُؤْمِنُونَ بِهِ ۖ وَقَدْ خَلَتْ سُنَّةُ الْأَوَّلِينَ ﴿١٣﴾

13. Hawaiamini (Qur-aan), na hali imekwishapita ada ya (kuadhibiwa) watu wa awali. 

 

 

 

وَلَوْ فَتَحْنَا عَلَيْهِم بَابًا مِّنَ السَّمَاءِ فَظَلُّوا فِيهِ يَعْرُجُونَ ﴿١٤﴾

14. Na hata kama Tungeliwafungulia mlango wa mbingu wakabakia kupanda huko.

 

 

 

لَقَالُوا إِنَّمَا سُكِّرَتْ أَبْصَارُنَا بَلْ نَحْنُ قَوْمٌ مَّسْحُورُونَ ﴿١٥﴾

15. Wangelisema: Hapana ila macho yetu yamelevywa, bali sisi ni watu tuliorogwa.

 

 

 

وَلَقَدْ جَعَلْنَا فِي السَّمَاءِ بُرُوجًا وَزَيَّنَّاهَا لِلنَّاظِرِينَ﴿١٦﴾

16. Na kwa yakini Tumejaalia katika mbingu buruji[3] na Tumeipamba kwa wenye kutazama.

 

 

 

وَحَفِظْنَاهَا مِن كُلِّ شَيْطَانٍ رَّجِيمٍ﴿١٧﴾

17. Na Tumeilinda na kila shaytwaan aliyetokomezwa mbali na kulaaniwa.

 

 

 

إِلَّا مَنِ اسْتَرَقَ السَّمْعَ فَأَتْبَعَهُ شِهَابٌ مُّبِينٌ﴿١٨﴾

18. Isipokuwa mdukizi basi huyo humfuatia kimondo kinachoonekana bayana.

 

 

 

وَالْأَرْضَ مَدَدْنَاهَا وَأَلْقَيْنَا فِيهَا رَوَاسِيَ وَأَنبَتْنَا فِيهَا مِن كُلِّ شَيْءٍ مَّوْزُونٍ﴿١٩﴾

19. Na ardhi Tumeitandaza na Tukatupa humo milima iliyosimama thabiti, na Tukaotesha humo kila kitu kwa uwiano. 

 

 

 

وَجَعَلْنَا لَكُمْ فِيهَا مَعَايِشَ وَمَن لَّسْتُمْ لَهُ بِرَازِقِينَ﴿٢٠﴾

20. Na Tukakuwekeeni humo njia na mbinu za maisha, na ya hao ambao nyinyi si wenye kuwaruzuku.

 

 

 

وَإِن مِّن شَيْءٍ إِلَّا عِندَنَا خَزَائِنُهُ وَمَا نُنَزِّلُهُ إِلَّا بِقَدَرٍ مَّعْلُومٍ﴿٢١﴾

21. Na hakuna kitu chochote isipokuwa Tuna hazina zake, na Hatukiteremshi isipokuwa kwa kadiri maalumu.

 

 

 

وَأَرْسَلْنَا الرِّيَاحَ لَوَاقِحَ فَأَنزَلْنَا مِنَ السَّمَاءِ مَاءً فَأَسْقَيْنَاكُمُوهُ وَمَا أَنتُمْ لَهُ بِخَازِنِينَ﴿٢٢﴾

22. Na Tukatuma pepo za rehma zikibeba umande, na Tukateremsha kutoka mbinguni maji kisha Tukakunywesheni kwayo, wala nyinyi si wenye kuyahifadhi.

 

 

 

وَإِنَّا لَنَحْنُ نُحْيِي وَنُمِيتُ وَنَحْنُ الْوَارِثُونَ﴿٢٣﴾

23. Na hakika Sisi Tunahuisha na Tunafisha, na Sisi Ndio Warithi.

 

 

 

وَلَقَدْ عَلِمْنَا الْمُسْتَقْدِمِينَ مِنكُمْ وَلَقَدْ عَلِمْنَا الْمُسْتَأْخِرِينَ﴿٢٤﴾

24. Na Tumekwishajua (vizazi) waliotangulia miongoni mwenu, na Tumekwishajua wenye kutaakhari.

 

 

 

وَإِنَّ رَبَّكَ هُوَ يَحْشُرُهُمْ ۚ إِنَّهُ حَكِيمٌ عَلِيمٌ﴿٢٥﴾

25. Na hakika Rabb wako Ndiye Atakayewakusanya. Na hakika Yeye Ni Mwenye Hikmah wa yote, Mjuzi wa yote.

 

 

 

وَلَقَدْ خَلَقْنَا الْإِنسَانَ مِن صَلْصَالٍ مِّنْ حَمَإٍ مَّسْنُونٍ﴿٢٦﴾

26. Na kwa yakini Tumemuumba binaadam kutokana na udongo wa mfinyanzi mkavu, unaotoa sauti, unaotokana na tope nyeusi iliyotaghayari.

 

 

 

وَالْجَانَّ خَلَقْنَاهُ مِن قَبْلُ مِن نَّارِ السَّمُومِ﴿٢٧﴾

27. Na majini Tuliwaumba kabla kutokana na moto ulio mkali mno.

 

 

 

وَإِذْ قَالَ رَبُّكَ لِلْمَلَائِكَةِ إِنِّي خَالِقٌ بَشَرًا مِّن صَلْصَالٍ مِّنْ حَمَإٍ مَّسْنُونٍ﴿٢٨﴾

28. Na pindi Rabb wako Alipowaambia Malaika: Hakika Mimi Namuumba mtu kutokana na udongo wa mfinyanzi mkavu, unaotoa sauti, unaotokana na tope nyeusi iliyotaghayari.

 

 

 

فَإِذَا سَوَّيْتُهُ وَنَفَخْتُ فِيهِ مِن رُّوحِي فَقَعُوا لَهُ سَاجِدِينَ﴿٢٩﴾

29. Basi Nitakapomsawazisha na Nikampuliza Roho Niliyomuumbia, muangukieni kumsujudia.

 

 

 

فَسَجَدَ الْمَلَائِكَةُ كُلُّهُمْ أَجْمَعُونَ﴿٣٠﴾

30. Basi wakasujudu Malaika wote pamoja.

 

 

 

إِلَّا إِبْلِيسَ أَبَىٰ أَن يَكُونَ مَعَ السَّاجِدِينَ﴿٣١﴾

31. Isipokuwa Ibliys, alikataa kuwa pamoja na waliosujudu.

 

 

 

قَالَ يَا إِبْلِيسُ مَا لَكَ أَلَّا تَكُونَ مَعَ السَّاجِدِينَ﴿٣٢﴾

32. (Allaah) Akasema: Ee Ibliys! Una nini hata hukuwa pamoja na waliosujudu?

 

 

 

قَالَ لَمْ أَكُن لِّأَسْجُدَ لِبَشَرٍ خَلَقْتَهُ مِن صَلْصَالٍ مِّنْ حَمَإٍ مَّسْنُونٍ﴿٣٣﴾

33. (Ibliys) akasema: Haiwi mimi nimsujudie mtu Uliyemuumba kutokana na udongo mkavu unaotoa sauti, unaotokana na tope nyeusi iliyotaghayari.

 

 

 

قَالَ فَاخْرُجْ مِنْهَا فَإِنَّكَ رَجِيمٌ﴿٣٤﴾

34. (Allaah) Akasema: Basi toka humo, kwani hakika wewe umetokomezwa mbali na kulaaniwa.

 

 

 

وَإِنَّ عَلَيْكَ اللَّعْنَةَ إِلَىٰ يَوْمِ الدِّينِ﴿٣٥﴾

35. Na hakika juu yako ipo laana mpaka Siku ya Malipo.

 

 

 

قَالَ رَبِّ فَأَنظِرْنِي إِلَىٰ يَوْمِ يُبْعَثُونَ﴿٣٦﴾

36.  Akasema: Rabb wangu! Nipe muhula mpaka Siku watakayofufuliwa.

 

 

 

قَالَ فَإِنَّكَ مِنَ الْمُنظَرِينَ﴿٣٧﴾

37. (Allaah) Akasema: Basi hakika wewe ni miongoni mwa waliopewa muhula.

 

 

 

إِلَىٰ يَوْمِ الْوَقْتِ الْمَعْلُومِ﴿٣٨﴾

38. Mpaka siku ya wakati maalumu.

 

 

 

قَالَ رَبِّ بِمَا أَغْوَيْتَنِي لَأُزَيِّنَنَّ لَهُمْ فِي الْأَرْضِ وَلَأُغْوِيَنَّهُمْ أَجْمَعِينَ﴿٣٩﴾

39. (Ibliys) akasema: Rabb wangu! Kwa vile Umenihukumia kupotoka, basi bila shaka nitawapambia (maasi) katika ardhi na nitawapotoa wote.

 

 

 

إِلَّا عِبَادَكَ مِنْهُمُ الْمُخْلَصِينَ﴿٤٠﴾

40. Isipokuwa Waja Wako miongoni mwao waliokhitariwa kwa ikhlaasw zao.

 

 

 

قَالَ هَـٰذَا صِرَاطٌ عَلَيَّ مُسْتَقِيمٌ﴿٤١﴾

41. (Allaah) Akasema: Hii ni njia ya kufikia Kwangu iliyonyooka.

 

 

 

إِنَّ عِبَادِي لَيْسَ لَكَ عَلَيْهِمْ سُلْطَانٌ إِلَّا مَنِ اتَّبَعَكَ مِنَ الْغَاوِينَ﴿٤٢﴾

42. Hakika Waja Wangu huna mamlaka nao isipokuwa ambaye atakufuata miongoni mwa waliopotoka.

 

 

 

وَإِنَّ جَهَنَّمَ لَمَوْعِدُهُمْ أَجْمَعِينَ﴿٤٣﴾

43. Na hakika Jahannam ni miadi yao wote pamoja.

 

 

 

لَهَا سَبْعَةُ أَبْوَابٍ لِّكُلِّ بَابٍ مِّنْهُمْ جُزْءٌ مَّقْسُومٌ﴿٤٤﴾

44. Ina milango saba, na kwa kila mlango iko sehemu (makhsusi) iliyogawanywa kwao wao.[4]

 

 

 

 

إِنَّ الْمُتَّقِينَ فِي جَنَّاتٍ وَعُيُونٍ﴿٤٥﴾

45. Hakika wenye taqwa watakuwa katika Jannaat na chemchemu.

 

 

 

ادْخُلُوهَا بِسَلَامٍ آمِنِينَ﴿٤٦﴾

46. (Wataambiwa): Ingieni humo kwa salama mkiwa katika amani.

 

 

 

وَنَزَعْنَا مَا فِي صُدُورِهِم مِّنْ غِلٍّ إِخْوَانًا عَلَىٰ سُرُرٍ مُّتَقَابِلِينَ﴿٤٧﴾

47. Na Tutaondosha mafundo ya kinyongo yaliyomo vifuani mwao,[5] wakiwa ndugu, juu ya makochi yaliyoinuliwa wakikabiliana.

 

 

 

لَا يَمَسُّهُمْ فِيهَا نَصَبٌ وَمَا هُم مِّنْهَا بِمُخْرَجِينَ﴿٤٨﴾

48. Hautowagusa humo uchovu nao humo hawatotolewa.

 

 

 

نَبِّئْ عِبَادِي أَنِّي أَنَا الْغَفُورُ الرَّحِيمُ﴿٤٩﴾

49. (Ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم)! Wajulishe Waja Wangu, kwamba: Hakika Mimi Ni Mwingi wa Kughufuria, Mwenye Kurehemu.

 

 

 

وَأَنَّ عَذَابِي هُوَ الْعَذَابُ الْأَلِيمُ﴿٥٠﴾

50. Na kwamba Adhabu Yangu, ndiyo adhabu iumizayo.

 

 

 

وَنَبِّئْهُمْ عَن ضَيْفِ إِبْرَاهِيمَ﴿٥١﴾

51. Na wajulishe kuhusu wageni wa Ibraahiym.

 

 

 

إِذْ دَخَلُوا عَلَيْهِ فَقَالُوا سَلَامًا قَالَ إِنَّا مِنكُمْ وَجِلُونَ﴿٥٢﴾

52. Pale walipoingia kwake, wakasema: Salaama! (Ibraahiym) akasema: Hakika sisi tunakuogopeni.

 

 

 

قَالُوا لَا تَوْجَلْ إِنَّا نُبَشِّرُكَ بِغُلَامٍ عَلِيمٍ﴿٥٣﴾

53. (Malaika) wakasema: Usiogope! Hakika sisi tunakubashiria ghulamu mjuzi.

 

 

 

قَالَ أَبَشَّرْتُمُونِي عَلَىٰ أَن مَّسَّنِيَ الْكِبَرُ فَبِمَ تُبَشِّرُونَ﴿٥٤﴾

54. (Ibraahiym) akasema: Je, mnanibashiria (mwana) na hali uzee umeshanishika, basi kwa njia gani mnanibashiria?

 

 

 

قَالُوا بَشَّرْنَاكَ بِالْحَقِّ فَلَا تَكُن مِّنَ الْقَانِطِينَ﴿٥٥﴾

55. Wakasema: Tunakubashiria kwa haki, basi usiwe miongoni mwa wakatao tamaa.

 

 

 

قَالَ وَمَن يَقْنَطُ مِن رَّحْمَةِ رَبِّهِ إِلَّا الضَّالُّونَ﴿٥٦﴾

56. Akasema: Na nani anayekata tamaa na Rehma ya Rabb wake isipokuwa wapotofu?

 

 

 

قَالَ فَمَا خَطْبُكُمْ أَيُّهَا الْمُرْسَلُونَ﴿٥٧﴾

57.  Akasema: Basi nini jambo lenu muhimu enyi Wajumbe?  

 

 

 

 

قَالُوا إِنَّا أُرْسِلْنَا إِلَىٰ قَوْمٍ مُّجْرِمِينَ﴿٥٨﴾

58. Wakasema: Hakika sisi tumetumwa kwa watu wahalifu.

 

 

 

إِلَّا آلَ لُوطٍ إِنَّا لَمُنَجُّوهُمْ أَجْمَعِينَ﴿٥٩﴾

59. Isipokuwa familia ya Luutw, hakika Sisi Tutawaokoa wote.

 

 

 

إِلَّا امْرَأَتَهُ قَدَّرْنَا ۙ إِنَّهَا لَمِنَ الْغَابِرِينَ﴿٦٠﴾

60. Isipokuwa mkewe. Tumehukumu kwamba yeye bila shaka ni miongoni mwa watakaobakia nyuma (kuangamizwa).

 

 

 

 

فَلَمَّا جَاءَ آلَ لُوطٍ الْمُرْسَلُونَ﴿٦١﴾

61. Basi Wajumbe walipokuja kwa familia ya Luutw.

 

 

 

قَالَ إِنَّكُمْ قَوْمٌ مُّنكَرُونَ﴿٦٢﴾

62. (Luutw) akasema: Hakika nyinyi ni watu msiojulikana.

 

 

 

قَالُوا بَلْ جِئْنَاكَ بِمَا كَانُوا فِيهِ يَمْتَرُونَ﴿٦٣﴾

63. (Malaika) wakasema: Bali tumekujia kwa yale waliyokuwa wanatilia shaka.

 

 

 

وَأَتَيْنَاكَ بِالْحَقِّ وَإِنَّا لَصَادِقُونَ﴿٦٤﴾

64. Na tumekujia kwa haki na hakika sisi ni wakweli.

 

 

 

فَأَسْرِ بِأَهْلِكَ بِقِطْعٍ مِّنَ اللَّيْلِ وَاتَّبِعْ أَدْبَارَهُمْ وَلَا يَلْتَفِتْ مِنكُمْ أَحَدٌ وَامْضُوا حَيْثُ تُؤْمَرُونَ﴿٦٥﴾

65. Basi toka usiku (huu) na ahli wako sehemu iliyobakia ya usiku na ufuate nyuma yao, wala asigeuke nyuma yeyote miongoni mwenu, na endeleeni kwenda mnakoamrishwa.

 

 

 

وَقَضَيْنَا إِلَيْهِ ذَٰلِكَ الْأَمْرَ أَنَّ دَابِرَ هَـٰؤُلَاءِ مَقْطُوعٌ مُّصْبِحِينَ﴿٦٦﴾

66. Na Tukamjulisha hukumu ya jambo hilo, kwamba: Mtu wa mwisho wa hawa (watendaji uliwati) atakuwa amemalizwa wakipambaukiwa asubuhi.

 

 

 

وَجَاءَ أَهْلُ الْمَدِينَةِ يَسْتَبْشِرُونَ﴿٦٧﴾

67. Na wakaja watu wa mji ule wakifurahia.

 

 

 

قَالَ إِنَّ هَـٰؤُلَاءِ ضَيْفِي فَلَا تَفْضَحُونِ﴿٦٨﴾

68. (Luutw) akasema: Hakika hawa ni wageni wangu, basi msinifedheheshe.

 

 

 

وَاتَّقُوا اللَّـهَ وَلَا تُخْزُونِ﴿٦٩﴾

69. Na mcheni Allaah wala msinihizi.

 

 

 

قَالُوا أَوَلَمْ نَنْهَكَ عَنِ الْعَالَمِينَ﴿٧٠﴾

70.  Wakasema: Je, hatujakukataza kukaribisha (au kuwalinda) watu wowote?

 

 

 

قَالَ هَـٰؤُلَاءِ بَنَاتِي إِن كُنتُمْ فَاعِلِينَ﴿٧١﴾

71. Akasema: Hawa hapa mabinti zangu (wa kuwaoa kihalali) ikiwa nyinyi ni wafanyaji.

 

 

 

لَعَمْرُكَ إِنَّهُمْ لَفِي سَكْرَتِهِمْ يَعْمَهُونَ﴿٧٢﴾

72. Naapa kwa uhai wako (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم)![6] Hakika wao (washirikina wa Makkah) wako katika ulevi wao wanatangatanga kwa upofu.

 

 

 

فَأَخَذَتْهُمُ الصَّيْحَةُ مُشْرِقِينَ﴿٧٣﴾

73. Basi uliwachukua ukelele angamizi wakati wanapambaukiwa.

 

 

 

فَجَعَلْنَا عَالِيَهَا سَافِلَهَا وَأَمْطَرْنَا عَلَيْهِمْ حِجَارَةً مِّن سِجِّيلٍ﴿٧٤﴾

74. Tukaupindua (mji huo) juu chini, na Tukawanyeshea mvua ya mawe ya udongo uliookwa (motoni).

 

 

 

إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَاتٍ لِّلْمُتَوَسِّمِينَ﴿٧٥﴾

75. Hakika katika hayo mna Aayaat (Ishara, Mawaidha, Mazingatio) kwa watambuzi.

 

 

 

وَإِنَّهَا لَبِسَبِيلٍ مُّقِيمٍ﴿٧٦﴾

76. Na hakika hiyo (miji) iko katika barabara kuu inayopitwa. 

 

 

إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَةً لِّلْمُؤْمِنِينَ﴿٧٧﴾

77. Hakika katika hayo ipo Aayah (Ishara, Dalili) [za wazi] kwa Waumini.

 

 

 

وَإِن كَانَ أَصْحَابُ الْأَيْكَةِ لَظَالِمِينَ﴿٧٨﴾

78. Na hakika watu wa Al-Aykah[7] walikuwa madhalimu.

 

 

 

 

فَانتَقَمْنَا مِنْهُمْ وَإِنَّهُمَا لَبِإِمَامٍ مُّبِينٍ﴿٧٩﴾

79. Tukawalipiza (kuwaadhibu) na miji yote miwili hiyo iko katika njia kuu mashuhuri.

 

 

 

وَلَقَدْ كَذَّبَ أَصْحَابُ الْحِجْرِ الْمُرْسَلِينَ﴿٨٠﴾

80. Na kwa yakini watu wa Al-Hijr (kina Thamuwd) waliwakadhibisha Rusuli.[8]

 

 

 

وَآتَيْنَاهُمْ آيَاتِنَا فَكَانُوا عَنْهَا مُعْرِضِينَ﴿٨١﴾

81. Na Tuliwapa Aayaat (Ishara, Dalili) Zetu wakawa wenye kuzipuuza.

 

 

 

وَكَانُوا يَنْحِتُونَ مِنَ الْجِبَالِ بُيُوتًا آمِنِينَ﴿٨٢﴾

82. Na walikuwa wanachonga majumba katika majabali wakiwa katika amani.

 

 

 

فَأَخَذَتْهُمُ الصَّيْحَةُ مُصْبِحِينَ﴿٨٣﴾

83. Ukawachukua ukelele angamizi wakipambaukiwa asubuhi.

 

 

 

فَمَا أَغْنَىٰ عَنْهُم مَّا كَانُوا يَكْسِبُونَ﴿٨٤﴾

84. Basi hayakuwasaidia yale waliyokuwa wakichuma.

 

 

 

وَمَا خَلَقْنَا السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ وَمَا بَيْنَهُمَا إِلَّا بِالْحَقِّ ۗ وَإِنَّ السَّاعَةَ لَآتِيَةٌ ۖ فَاصْفَحِ الصَّفْحَ الْجَمِيلَ﴿٨٥﴾

85. Na Hatukuumba mbingu na ardhi na vilivyo baina yake isipokuwa kwa haki. Na hakika Saa bila shaka itafika. Basi samehe msamaha mzuri.

 

 

 

إِنَّ رَبَّكَ هُوَ الْخَلَّاقُ الْعَلِيمُ﴿٨٦﴾

86. Hakika Rabb wako Ndiye Mwingi wa Kuumba Atakavyo, Mjuzi wa yote.

 

 

 

وَلَقَدْ آتَيْنَاكَ سَبْعًا مِّنَ الْمَثَانِي وَالْقُرْآنَ الْعَظِيمَ﴿٨٧﴾

87. Na kwa yakini Tumekupa (Suwrah au Aayaat) Saba zinazokaririwa (kusomwa) na Qur-aan Adhimu.[9]

 

 

 

لَا تَمُدَّنَّ عَيْنَيْكَ إِلَىٰ مَا مَتَّعْنَا بِهِ أَزْوَاجًا مِّنْهُمْ وَلَا تَحْزَنْ عَلَيْهِمْ وَاخْفِضْ جَنَاحَكَ لِلْمُؤْمِنِينَ﴿٨٨﴾

88. Usikodoe kabisa macho yako kwa yale ya starehe Tuliyowaneemesha baadhi ya makundi (ya kikafiri) miongoni mwao, wala usiwahuzunikie. Na inamisha bawa lako kwa Waumini (kuwahurumia).

 

 

 

وَقُلْ إِنِّي أَنَا النَّذِيرُ الْمُبِينُ﴿٨٩﴾

89. Na sema (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم): Hakika mimi ni mwonyaji mwenye kubainisha.

 

 

 

كَمَا أَنزَلْنَا عَلَى الْمُقْتَسِمِينَ﴿٩٠﴾

90. Kama Tulivyowateremshia (adhabu) waliojigawanya.

 

 

 

الَّذِينَ جَعَلُوا الْقُرْآنَ عِضِينَ﴿٩١﴾

91. Ambao wameifanya Qur-aan sehemu mbali mbali.[10] 

 

 

 

فَوَرَبِّكَ لَنَسْأَلَنَّهُمْ أَجْمَعِينَ﴿٩٢﴾

92. Basi Naapa kwa Rabb wako (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم)! Bila shaka Tutawauliza wote.

 

 

 

عَمَّا كَانُوا يَعْمَلُونَ﴿٩٣﴾

93. Kuhusu yale waliyokuwa wakitenda.

 

 

 

فَاصْدَعْ بِمَا تُؤْمَرُ وَأَعْرِضْ عَنِ الْمُشْرِكِينَ﴿٩٤﴾

94. Basi tangaza wazi yale unayoamrishwa na jitenge na washirikina.

 

 

 

إِنَّا كَفَيْنَاكَ الْمُسْتَهْزِئِينَ﴿٩٥﴾

95. Hakika sisi Tunakutosheleza dhidi ya wafanyao istihzai.

 

 

 

الَّذِينَ يَجْعَلُونَ مَعَ اللَّـهِ إِلَـٰهًا آخَرَ ۚ فَسَوْفَ يَعْلَمُونَ﴿٩٦﴾

96. Ambao wanafanya pamoja na Allaah mwabudiwa mwengine, basi watakuja kujua.

 

 

 

وَلَقَدْ نَعْلَمُ أَنَّكَ يَضِيقُ صَدْرُكَ بِمَا يَقُولُونَ﴿٩٧﴾

97. Na kwa yakini Tunajua kwamba kifua chako kinadhikika kwa yale wanayoyasema.

 

 

 

فَسَبِّحْ بِحَمْدِ رَبِّكَ وَكُن مِّنَ السَّاجِدِينَ﴿٩٨﴾

98. Basi Msabbih Rabb wako kwa Himdi Zake na uwe miongoni mwa wanaosujudu.

 

 

 

وَاعْبُدْ رَبَّكَ حَتَّىٰ يَأْتِيَكَ الْيَقِينُ﴿٩٩﴾

99. Na mwabudu Rabb wako mpaka ikufikie yakini (mauti).

 

 

 

 

 

[1] الحروف المقطعة  (Al-Huruwf Al-Muqatw-twa’ah):

 

Hizi ni herufi zinazojulikana kama الحروف المقطعة  (Al-Huruwf Al-Muqatw-twa’ah), ambazo hakuna ajuaye maana zake isipokuwa Allaah (سبحانه وتعالى). Rejea Tanbihi ya Al-Baqarah (2:1).

 

[2] Qur-aan Imehifadhiwa:

 

Ni Ahadi ya Allaah (سبحانه وتعالى) Kuihifadhi Qur-aan, na Ahadi Yake kamwe haiendi kinyume! Wala haiwezekani Qur-aan kubadilishwa au kuitia pogo au kuitowesha ipotee kabisa kwa sababu Allaah (سبحانه وتعالى) Aliiteremsha kwanza katika kifua cha Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم), kisha Swahaba zake (رضي الله عنهم)  wakaihifadhi nyoyoni mwao, kisha Waumini waliofuatia, na inaendelea kuhifadhika katika vifua vya Waislamu, na itaendelea hivyo hadi Siku ya Qiyaamah. Na hii ni muujiza, kwa sababu imedhihirika wazi kuwa Waislamu wengi ulimwenguni wamehifadhi Qur-aan katika vifua vyao. Bali hata wale ambao hawajui lugha ya kiarabu, Allaah (سبحانه وتعالى) Amewawezesha waihifadhi Qur-aan vifuani mwao. Na maadui wa Uislamu waliochoma Miswahafu wamefeli! Kwani hata wakichoma Miswahafu yote waliyonayo, Qur-aan bado itabakia vifuani vya Waislamu!

 

Imaam As-Sa’diy (رحمه الله)  amesema: Yaani wakati inateremshwa na baada ya kuteremshwa. Wakati inateremshwa, ilihifadhiwa isidukuliwe na kila shaytwaan aliyelaaniwa na kubaidishwa na Rehma ya Allaah. Kisha baada ya kuteremshwa, Allaah (عزّ وجلّ) Aliihifadhi katika moyo wa Rasuli Wake (صلى الله عليه وآله وسلم), kisha kwenye nyoyo za ummah wake. Halafu Allaah (سبحانه وتعالى) Akayahifadhi maneno yake yasibadilishwe ndani yake, yasiongezwe, wala yasipunguzwe, na maana zake zisibadilishwe. Na kwa hifadhi kama hii, hawezi mpotoshaji kupotosha maana zake zozote zile isipokuwa Allaah (عزّ وجلّ) Atamuibulia mtu wa kubainisha haki waziwazi. Na hii ni katika Dalili Kubwa kabisa za Allaah pamoja na Neema Zake kwa Waja Wake Waumini. Ama Hifadhi nyingine, ni kwamba Allaah Anawalinda wenye kushikamana na Qur-aan kutokana na maadui zao, na Hawapi kabisa nafasi maadui hao ya kuweza kuwadhuru kama watawavamia. [Tafsiyr As-Sa’diy]

 

[3] Buruji:

 

Rejea Suwrah Al-Burujw (85:1) kulikotajwa maana zake kadhaa kutokana na kauli za ‘Ulamaa.

 

[4] Milango Ya Jahannam:

 

Jahnnam ina milango saba. Kila mlango uko chini ya mwengine. Kila mlango utakuwa na fungu na sehemu la wafuasi wa Ibliys kulingana na matendo yao. [Tafsiyr Al-Muyassar na As-Sa’diy]

 

[5] Waumini Wataondoshewa Mafundo, Vinyongo Kabla Ya Kuingia Peponi: Rejea Al-A’raaf (7:43).

 

[6] Kuapia Kwa Asiyekuwa Allaah Ni Haramu Na Ni Shirk:

 

Allaah (سبحانه وتعالى) Ambaye ni Muumba wa kila kitu, Anaapia kwa chochote Atakacho. Ama viumbe, haijuzu kuapia kwa chochote isipokuwa kuapia kwa Allaah. Na Allaah (عزّ وجلّ) Anaapia hapa kwa uhai wa Nabiy Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم) kama ni taadhima. [Tafsiyr Al-Muyassar]

 

Na tunaona kuwa Allaah (سبحانه وتعالى) Anaapia vitu mbalimbali katika Suwrah kadhaa. Anaapia kwa mbingu na ardhi, Anaapia pia kwa tini na zaytuni, jua na mwezi, usiku na mchana, alasiri n.k. Yeye Allaah (سبحانه وتعالى) Ana haki ya kuapia chochote Anachotaka. Ama sisi viumbe Vyake, ni haramu kuapia kwa chochote isipokuwa kwa Allaah (سبحانه وتعالى) tu. Na kuapia huku ni kutumia herufi tatu tu. Rejea An-Nahl (16:56).

 

Wengi kati ya Waislamu wanaapia vitu vitukufu vya Allaah (سبحانه وتعالى) wakidhania kuwa inafaa, kama kuapia Mswahafu, Al-Ka’bah, kuapia kwa kumtaja Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم). Basi hivi na vinginevyo vyovyote haijuzu kabisa kuapia!

 

Na Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) ameharamisha kuapia kwa Asiyekuwa Allaah (سبحانه وتعالى). Hadiyth kadhaa zimegusia hili, na mojawapo ni ifuatayo: Amesimulia Ibn ‘Umar (رضي الله عنهما)  kwamba alimsikia mtu mmoja akisema:  Laa, naapa kwa Al-Ka’bah.  Ibn ‘Umar akamwambia: Haapiwi asiye Allaah, kwani hakika mimi nimemsikia Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akisema: “Mwenye kuapa kwa asiye Allaah, basi hakika amefanya shirki.”  [Hadiyth Hasan. Imekharijiwa na At-Tirmidhiy (1535) na Abu Daawuwd (3251)]

 

[7] Watu Wa Al-Aykah ni watu wa kichakani katika mji wa Madyan. Ni watu wa Nabiy Shu’ayb (عليه السّلام). Rejea Ash-Shu’araa (26:176) kupata maelezo bayana.

 

[8] Watu Wa Al-Hijr (Thamuwd):

 

Watu wa Al-Hijr ni kina Thamuwd ambao walitumiwa Nabiy Swaalih (عليه السّلام) kuwalingania Tawhiyd ya Allaah. Wameitwa Al-Hijr kwa sababu waliishi Al-Hijr; eneo lilioko baina ya Sham na Hijaaz. Rejea Ash-Shams (91:11-15) kwenye maelezo kuhusu kisa chao. Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم)  alipokuwa anaelekea katika Vita vya Tabuwk alipita na Swahaba wake (رضي الله عنهم)  katika masikani zao walizokua wakiishi. Akawatahadharisha Swahaba kwa kauli yake (صلى الله عليه وآله وسلم): “Msiingie masikani za waliodhulumu nafsi zao isipokuwa muingie huku mnalia ili isije kukusibuni yaliyowasibu wao.” Kisha akafunika kichwa chake na kuharakiza mwendo wa kasi mpaka akavuka bonde.  [Al-Bukhaari, Muslim na wengineo]

 

[9] Suwrah Au Aayah Saba Zinazokaririwa.

 

Wafasiri wa Qur-aan wamekhitilafiana kuhusu Suwrah au Aayaat. Kuna waliosema ni Suwrah saba ndefu: (i) Al-Baqarah (ii) Aal-‘Imraan (iii) An-Nisaa (iv) Al-Maaidah (v) Al-An’aam (vi) Al-A’raaf (vii) Al-Anfaal, (viii) At-Tawbah ambayo haina BismiLLaah. Na rai nyengine ni Aayaat Saba za Suwrah Al-Faatihah kwa kuwa zinakaririwa katika kila Swalaah. [Tafsiyr As-Sa’diy, Tafsiyr Ibn Kathiyr]

 

[10] Makafiri Kuifanya Qur-aan Katika Sehemu Mbalimbali:

 

Waliosema ni sihri (uchawi), imetungwa, mashairi, ukuhani, hekaya za awali,  n.k. ili wawazuie watu kufuata uongofu. [Tafsiyr Al-Muyassar, As-Sa’diy, Imaam Ibn Kathiyr] Na Imaam Ibn Kathiyr ameongezea kunukuu Hadiyth ya Ibn ‘Abaas  (رضي الله عنهما) “Hao waloifanya Qur-aan sehemu mbalimbali ni Watu wa Kitabu (Mayahudi na Manaswaara), wameamini baadhi yake na wamekanusha baadhi yake.”  [Al-Bukaariy]

 

Na pia rejea Al-Furqaan (25:4) kwenye uchambuzi na maelezo bayana kuhusu makafiri na kuikanusha kwao Qur-aan, na kuipa sifa ovu mbali mbali, pamoja na kumpachika sifa ovu mbali mbali Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم).

 

Share