085 - Al-Buruwj

 

الْبُرُوج

 

 

085-Al-Buruwj

 

 

085-Al-Buruwj: Utangulizi Wa Suwrah

 

Alhidaaya.com

 

 

 

بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ

 

 

 

وَالسَّمَاءِ ذَاتِ الْبُرُوجِ ﴿١﴾

1. Naapa kwa mbingu yenye buruji [1]  

 

 

 

 

وَالْيَوْمِ الْمَوْعُودِ ﴿٢﴾

2. Na Naapa kwa Siku iliyoahidiwa (ya Qiyaamah).

 

 

 

وَشَاهِدٍ وَمَشْهُودٍ ﴿٣﴾

3. Na Naapa kwa shahidi na kinachoshuhudiwa.[2]

 

 

 

 

قُتِلَ أَصْحَابُ الْأُخْدُودِ ﴿٤﴾

4. Wamelaaniwa na kuangamia watu wa mahandaki.[3]

 

 

النَّارِ ذَاتِ الْوَقُودِ ﴿٥﴾

5.  Yenye moto uliojaa kuni na mafuta.

 

 

 

إِذْ هُمْ عَلَيْهَا قُعُودٌ ﴿٦﴾

6.  Pale walipokuwa wamekaa hapo.

 

 

 

وَهُمْ عَلَىٰ مَا يَفْعَلُونَ بِالْمُؤْمِنِينَ شُهُودٌ ﴿٧﴾

7.  Nao ni wenye kushuhudia juu ya yale wanayowafanyia Waumini.

 

 

 

 

وَمَا نَقَمُوا مِنْهُمْ إِلَّا أَن يُؤْمِنُوا بِاللَّـهِ الْعَزِيزِ الْحَمِيدِ ﴿٨﴾

8. Na hawakuwachukia isipokuwa kwa vile wamemwamini Allaah Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika, Mwenye Kustahiki Kuhimidiwa kwa yote.

 

 

 

 

الَّذِي لَهُ مُلْكُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِۚ وَاللَّـهُ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ شَهِيدٌ ﴿٩﴾

9. Ambaye Pekee Ana ufalme wa mbingu na ardhi. Na Allaah juu ya kila kitu Ni Shahidi.  

 

 

 

 

إِنَّ الَّذِينَ فَتَنُوا الْمُؤْمِنِينَ وَالْمُؤْمِنَاتِ ثُمَّ لَمْ يَتُوبُوا فَلَهُمْ عَذَابُ جَهَنَّمَ وَلَهُمْ عَذَابُ الْحَرِيقِ ﴿١٠﴾

10. Hakika wale waliowatesa motoni Waumini wa kiume na Waumini wa kike kisha hawakutubu, watapata adhabu ya Jahannam, na watapata adhabu ya kuunguza.

 

 

 

 

إِنَّ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ لَهُمْ جَنَّاتٌ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُۚ ذَٰلِكَ الْفَوْزُ الْكَبِيرُ ﴿١١﴾

11. Hakika wale walioamini na wakatenda mema watapata Jannaat zipitazo chini yake mito. Huko ndiko kufuzu kukubwa.

 

 

 

 

إِنَّ بَطْشَ رَبِّكَ لَشَدِيدٌ ﴿١٢﴾

12. Hakika mkamato wa kuadhibu wa Rabb wako bila shaka ni mkali.

 

 

 

 

إِنَّهُ هُوَ يُبْدِئُ وَيُعِيدُ ﴿١٣﴾

13. Hakika Yeye Ndiye Anayeanzisha asili (ya uumbaji) na Anayerudisha.

 

 

 

 

وَهُوَ الْغَفُورُ الْوَدُودُ ﴿١٤﴾

14. Naye Ni Mwingi wa Kughufuria, Mwenye Upendo halisi.

 

 

 

 

ذُو الْعَرْشِ الْمَجِيدُ ﴿١٥﴾

15. Mwenye ‘Arsh, Al-Majiyd.[4]

 

 

 

 

فَعَّالٌ لِّمَا يُرِيدُ ﴿١٦﴾

16. Mwingi wa Kufanya Atakalo, hakuna wa kumzuia.

 

 

 

 

هَلْ أَتَاكَ حَدِيثُ الْجُنُودِ ﴿١٧﴾

17. Je, imekujia hadithi ya majeshi?

 

 

 

 

فِرْعَوْنَ وَثَمُودَ ﴿١٨﴾

18.  Ya Firawni na kina Thamuwd?

 

 

 

 

بَلِ الَّذِينَ كَفَرُوا فِي تَكْذِيبٍ ﴿١٩﴾

19. Bali wale waliokufuru wamo katika kukadhibisha.

 

 

 

 

وَاللَّـهُ مِن وَرَائِهِم مُّحِيطٌ ﴿٢٠﴾

20. Na Allaah Amewazunguka (kwa Ujuzi Wake) nyuma yao.

 

 

 

 

 

بَلْ هُوَ قُرْآنٌ مَّجِيدٌ ﴿٢١﴾

21. Bali hii ni Qur-aan Majiyd[5].     

 

 

 

فِي لَوْحٍ مَّحْفُوظٍ ﴿٢٢﴾

22. Katika Ubao Uliohifadhiwa.[6]

 

 

 

[1] Buruji:

 

‘Ulamaa wametaja maana ya buruji katika kauli zifuatazo: (i) Ibn ‘Abbaas, Mujaahid, Adhw-Dhwahaak, Al-Hasan, Qataadah, As-Suddy wamesema ni nyota (ii) Mujaahid kanukuliwa kwenye kauli nyingine akisema ni nyota zenye walinzi (iii) Yahyaa bin Raafi’ amesema ni maqasri mbinguni (iv) Al-Minhaal bin ‘Amr amesema ni uumbaji mzuri (v) Ibn Jariyr yeye anaona ni vituo au njia za kupitia jua na mwezi, nazo ni buruji kumi na mbili ambazo jua hutembea na kupita katika kila moja ya hizi burj (umoja wa buruji) katika mwezi mmoja. Mwezi nao pia hutembea na kupita katika kila moja ya burj hizi katika siku mbili na theluthi, na hivyo ni vituo ishirini na nane, na hufichika kwa nyusiku mbili. [Tafsiyr Ibn Kathiyr]

 

Rejea pia Al-Furqaan (25:61)]

 

[2] Shahidi Na Kinachoshuhudiwa:

 

Inajumuisha kila mtu anayekidhi maelezo haya. Yaani: Mwenye kuona na anayeonekana, na mwenye kuwepo na mwenye kuhudhurishwa. Kinachoshuhudiwa hapa ni ishara dhahiri zinazong'aa za Allaah (سبحانه وتعالى) na Hikma iliyodhahiri, na Rehma Yake pana. [Tafsiyr As-Sa’diy] Na imesemwa pia yanayofuatia ya Aayah namba (4). 

 

[3] Kisa Cha Watu Wa Mahandaki:

 

Allaah (سبحانه وتعالى) Ameapia kuanzia mwanzo wa Suwrah. Na jawabu la kiapo hicho  (جَوَابُ القَسَمِ) ni kama alivyotafsiri Imaam As-Sa’diy (رحمه الله):

Ni Kauli Yake:

قُتِلَ أَصْحَابُ الْأُخْدُودِ ﴿٤﴾

Wamelaaniwa na kuangamia watu wa mahandaki.

 

Hii ni duaa  ya kuangamizwa kwao. Na mahandaki ni mashimo yanayochimbwa ardhini. Na hawa watu wa mahandaki walikuwa ni makafiri, na walikuwa wakiishi pamoja nao Waislamu.  Wakajaribu kuwarai Waislamu ili waingie katika dini yao,  lakini Waumini hawa walikataa kufanya hivyo. Basi makafiri wakachimba mahandaki ardhini na kuwasha moto ndani yake, kisha wakaketi kuyazunguka na wakawatesa Waumini na kuwasogeza karibu na moto huo. Wale waliowakubalia kuingia ukafirini waliwaachia, ama wale walioshikamana na imaan yao waliwatupa motoni.  Huu ulikuwa ni mfano wa uadui mkubwa juu ya Allaah na Waumini, kwa hiyo Allaah Akawalaani, Akawaangamiza na Akawaahidi adhabu ndio Akasema:

قُتِلَ أَصْحَابُ الْأُخْدُودِ ﴿٤﴾

Wamelaaniwa na kuangamia watu wa mahandaki.

[Tafsiyr As-Sa’diy]

 

Aayah zinazofuatia zinaelezea hali ilivyo ya kisa hicho cha watu wa mahandaki na Adhabu Alizowaahidi Allaah.

 

[4] Mwenye ‘Arsh Al-Majiyd

 

Tafsiyr:

 

Yaani Mwenye Kumiliki ‘Arsh Adhimu Ambaye kutokana na Utukufu Wake, Ametandaza mbingi na ardhi na Kursiyy ambayo ni kipimo cha (udogo wa) pete katika jangwa, kulinganisha na ‘Arsh.  Allaah Ameitaja ‘Arsh makhsusi  kutokana na uadhimu wake, na kwamba ni makhsusi kati ya vitu Alivyoviuma vilivyokuuwa karibu Naye (سبحانه وتعالى). AL-Majiyd inaweza kuwa imekusudiwa ni ‘Arsh. Na huenda Al-Majiyd imekusudiwa ni Allaah ambayo ni Sifa yeye maana pana ya Utukufu. [Tafsiyr As-Sa’diy]

 

Na katika Majina Mazuri ya Allaah (سبحانه وتعالى) na Sifa Zake maana ya Al-Majiyd  ni: Mwingi Mno Wa Vipawa Na Ukarimu.

 

Ikiwa imekusudiwa Qur-aan, basi ni: Adhimu, Karimu, yenye kheri, Baraka na ilimu tele.  Rejea Qaaf (50:1).

 

[5] Qur-aan Majiyd:

 

Qur-aan Adhimu, Karimu, yenye kheri, hikmah, baraka na ilmu tele.  Rejea Qaaf (50:1)

 

[6] Al-Lawh Al-Mahfuwdhw:

 

Al-Lawh Al-Mahfuwdhw ni Ubao Uliohifadhiwa mbinguni. Umehifadhika kutokana na mabadiliko, kuongozeka na kupunguka na umehifadhiwa na mashaytwaan. Nao ni Ubao ambao Allaah (سبحانه وتعالى)  Amethibitisha kila kitu ndani yake [Tafsiyr As-Sa’diy]

 

Na pia imetajwa kuwa ni Ummul-Kitaab (Mama wa Kitabu) Rejea pia Ar-Ra’d  (13:39).

 

 

Share