086 - Atw-Twaariq

 

الطَّارِق

 

086-At-Twaariq

 

086-Atw-Twaariq: Utangulizi Wa Suwrah

 

Alhidaaya.com

 

 

بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ

 

 

 

وَالسَّمَاءِ وَالطَّارِقِ ﴿١﴾

1. Naapa kwa mbingu na kinachogonga kinapotoka usiku[1].

 

 

 

وَمَا أَدْرَاكَ مَا الطَّارِقُ ﴿٢﴾

2. Na kipi kitakachokujulisha kinachogonga na kutoka usiku?

 

 

 

النَّجْمُ الثَّاقِبُ ﴿٣﴾

3.  Ni nyota yenye mwanga mkali mno inayopenya kwa nguvu.  

 

 

 

إِن كُلُّ نَفْسٍ لَّمَّا عَلَيْهَا حَافِظٌ ﴿٤﴾

4. Hakuna nafsi yeyote isipokuwa inayo (Malaika) mhifadhi juu yake. 

 

 

 

فَلْيَنظُرِ الْإِنسَانُ مِمَّ خُلِقَ ﴿٥﴾

5. Basi na atazame binaadamu ameumbwa kutokana na kitu gani?

 

 

 

خُلِقَ مِن مَّاءٍ دَافِقٍ ﴿٦﴾

6. Ameumbwa kutokana na maji yatokayo kwa mchupo (manii).

 

 

 

يَخْرُجُ مِن بَيْنِ الصُّلْبِ وَالتَّرَائِبِ ﴿٧﴾

7. Yanatoka baina ya uti wa mgongo na mbavu za kifua.

 

 

 

إِنَّهُ عَلَىٰ رَجْعِهِ لَقَادِرٌ ﴿٨﴾

8. Hakika Yeye (Allaah) bila shaka Ni Muweza[2] wa Kumrudisha (hai).

 

 

 

يَوْمَ تُبْلَى السَّرَائِرُ ﴿٩﴾

9. Siku siri zitakapopekuliwa (na kufichuka).

 

 

 

فَمَا لَهُ مِن قُوَّةٍ وَلَا نَاصِرٍ ﴿١٠﴾

10. Basi hatakuwa na nguvu yoyote wala mwenye kunusuru yeyote.

 

 

 

وَالسَّمَاءِ ذَاتِ الرَّجْعِ ﴿١١﴾

11. Naapa kwa mbingu yenye marejeo (ya kuleta mvua).

 

 

 

وَالْأَرْضِ ذَاتِ الصَّدْعِ ﴿١٢﴾

12. Na Naapa kwa ardhi yenye kupasuka (kutoa mimea).

 

 

 

إِنَّهُ لَقَوْلٌ فَصْلٌ ﴿١٣﴾

13. Hakika hii (Qur-aan) ni kauli pambanushi[3] (bayana na ukweli mtupu)

 

 

 

وَمَا هُوَ بِالْهَزْلِ ﴿١٤﴾

14. Nayo si mzaha.

 

 

إِنَّهُمْ يَكِيدُونَ كَيْدًا ﴿١٥﴾

15. Hakika wao wanapanga hila.

 

 

 

وَأَكِيدُ كَيْدًا ﴿١٦﴾

16. Nami Natibua hila (zao).

 

 

 

فَمَهِّلِ الْكَافِرِينَ أَمْهِلْهُمْ رُوَيْدًا ﴿١٧﴾

17. Basi wape makafiri muhula, wape muhula taratibu.

 

 

 

[1] Atw-Twaariq (Nyota Angavu Inayotoka Usiku Huku Ikigonga)   

 

At-Twaariq ni nyota inayotoka usiku yenye mwanga mkali, na mwanga wake unapenya katika mbingu hadi unaonekana ardhini. Rai iliyo sahihi ni nyota zote zenye mwanga mkali unaopenya. [Tafsiyr As-Sa’diy]

 

Na kauli nyengineyo ni anayegonga usiku kama alivyotafsiri Imaam Ibn Kathiyr:

 

Imeitwa At-Twaariq kwa sababu inaonekana usiku na inapotea mchana. Na inatilia nguvu Hadiyth Swahiyh ya kukatazwa mtu kuwafikia ahli wake kwa ghafla usiku kama ilivyothibiti katika Hadiyth ifuatayo:

 

عَنْ جَابِرٍ، قَالَ نَهَى رَسُولُ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم أَنْ يَطْرُقَ الرَّجُلُ أَهْلَهُ لَيْلاً يَتَخَوَّنُهُمْ أَوْ يَلْتَمِسُ عَثَرَاتِهِمْ ‏.‏

 

Amesimulia Jaabir (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amekataza mtu kuwafikia ahli wake (bila ya kuwapasha habari) usiku kwa kujenga dhana kwamba wanamkhini, au kupeleleza na kufumania makosa yao.  [Muslim]

 

Na Hadiyth nyengine (ni duaa ya kujikinga na viumbe vya shari vinavyoingia majumbani usiku:

 

ومِنْ شَرِّ كُلِّ طارِقٍ إِلَّا طَارِقاً يَطْرُقُ بخَيْرٍ يَا رَحْمَنُ.

 

Na shari ya kila anayegonga usiku ila anayegonga kwa kheri Ee Mwingi wa Rehma. [Tafsiyr Ibn Kathiyr]

 

Bonyeza kiungo kifuatacho kupata duaa hiyo:

 

128-Hiswnul-Muslim: Duaa Ya Kuzuia Vitimbi Vya Mashaytwaan

 

[2] Kuthibitisha Sifa Ya Allaah (سبحانه وتعالى) Ya  Uwezo Wake:

 

Rejea Adh-Dhaariyaat (51:58)  

 

[3] Qur-aan Ni Kauli Pambanushi:

 

Kauli Pambanushi: Ina uwazi na ukweli mtupu. [Tafsiyr As-Sa’diy]

 

Kauli Pambanushi: Inapambanua baina ya haki na baatwil.  [Tafsiyr Al-Muyassar]

 

Kauli Pambanushi: Ya haki. [Tafsiyr Ibn Kathiyr]

 

Kauli Pambanushi: Inapambanua baina ya haki na baatwil na imaamuru sharia kali kwa mwanaadam ili kukata mizizi ya uovu. [The Noble Qur-aan]

 

 

 

 

Share