087 - Al-A'laa
الْأَعْلَى
087-Al-A’laa
087-Al-A’laa: Utangulizi Wa Suwrah
بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ
سَبِّحِ اسْمَ رَبِّكَ الْأَعْلَى ﴿١﴾
1. Sabbih Jina la Rabb wako Mwenye ‘Uluwa Aliyetukuka kabisa kuliko vyote.[1]
الَّذِي خَلَقَ فَسَوَّىٰ ﴿٢﴾
2. Ambaye Ameumba (kila kitu) kisha Akasawazisha.
وَالَّذِي قَدَّرَ فَهَدَىٰ ﴿٣﴾
3. Na Ambaye Amekadiria na Akaongoza.[2]
وَالَّذِي أَخْرَجَ الْمَرْعَىٰ ﴿٤﴾
4. Na Ambaye Ametoa malisho.
فَجَعَلَهُ غُثَاءً أَحْوَىٰ ﴿٥﴾
5. Kisha Akayafanya majani makavu, meusi.
سَنُقْرِئُكَ فَلَا تَنسَىٰ ﴿٦﴾
6. Tutakufanya uisome (Qur-aan ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) kisha hutoisahau.
إِلَّا مَا شَاءَ اللَّـهُۚ إِنَّهُ يَعْلَمُ الْجَهْرَ وَمَا يَخْفَىٰ ﴿٧﴾
7. Isipokuwa yale Ayatakayo Allaah. Hakika Yeye Anayajua ya jahara na yale yanayofichikana.
وَنُيَسِّرُكَ لِلْيُسْرَىٰ ﴿٨﴾
8. Na Tutakuwepesishia kwa yaliyo mepesi.
فَذَكِّرْ إِن نَّفَعَتِ الذِّكْرَىٰ ﴿٩﴾
9. Basi kumbusha ikiwa unafaa ukumbusho.
سَيَذَّكَّرُ مَن يَخْشَىٰ ﴿١٠﴾
10. Atakumbuka yule anayeogopa.
وَيَتَجَنَّبُهَا الْأَشْقَى ﴿١١﴾
11. Na atajiepusha nao fedhuli.
الَّذِي يَصْلَى النَّارَ الْكُبْرَىٰ ﴿١٢﴾
12. Ambaye atauingia moto mkubwa kabisa na kuungua.
ثُمَّ لَا يَمُوتُ فِيهَا وَلَا يَحْيَىٰ ﴿١٣﴾
13. Kisha hatokufa humo, na wala hatokuwa na uhai (wa raha).[3]
قَدْ أَفْلَحَ مَن تَزَكَّىٰ ﴿١٤﴾
14. Hakika amefaulu ambaye amejitakasa.
وَذَكَرَ اسْمَ رَبِّهِ فَصَلَّىٰ ﴿١٥﴾
15. Na akadhukuru Jina la Rabb wake na akaswali.
بَلْ تُؤْثِرُونَ الْحَيَاةَ الدُّنْيَا ﴿١٦﴾
16. Bali mnahiari zaidi uhai wa dunia.[4]
وَالْآخِرَةُ خَيْرٌ وَأَبْقَىٰ ﴿١٧﴾
17. Na hali Aakhirah ni bora zaidi na ya kudumu zaidi.
إِنَّ هَـٰذَا لَفِي الصُّحُفِ الْأُولَىٰ ﴿١٨﴾
18. Hakika haya bila shaka yamo katika Suhuf (Maandiko Matukufu) ya awali.[5]
صُحُفِ إِبْرَاهِيمَ وَمُوسَىٰ ﴿١٩﴾
19. Suhuf ya Ibraahiym na Muwsaa.
[1] Al-A’laa:
Mwenye ‘Uluwa, Ametukuka, Ana Uadhama Kuliko wote kuliko vyote, Yuko juu Kabisa juu ya viumbe Vyake vyote.
[2] Allaah (سبحانه وتعالى) Amekadiria Kila Alichokiumba Akakiongoza:
Kauli Ya Allaah (سبحانه وتعالى):
قَالَ رَبُّنَا الَّذِي أَعْطَىٰ كُلَّ شَيْءٍ خَلْقَهُ ثُمَّ هَدَىٰ ﴿٥٠﴾
(Muwsaa) akasema: Rabb wetu ni Yule Aliyekipa kila kitu umbo lake, kisha Akakiongoza. [Twaahaa (20:50)]
Na kauli ya Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) kuhusu Allaah (سبحانه وتعالى) Kukadiria kila Alichokiumba ni Hadiyth ifuatayo:
عَنْ عَبْدِ اللَّهِ بْنِ عَمْرِو، بْنِ الْعَاصِ قَالَ سَمِعْتُ رَسُولَ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم يَقُولُ " كَتَبَ اللَّهُ مَقَادِيرَ الْخَلاَئِقِ قَبْلَ أَنْ يَخْلُقَ السَّمَوَاتِ وَالأَرْضَ بِخَمْسِينَ أَلْفَ سَنَةٍ - قَالَ - وَعَرْشُهُ عَلَى الْمَاءِ " .
Amesimulia ‘Abdullaah bin ‘Amr bin Al-‘Aasw (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Hakika Allaah Aliandika (kwenye Al-Lawh Al-Mahfuwdh) makadirio na hatima ya viumbe wote kabla ya kuumba mbingu na ardhi kwa miaka elfu khamsini, - akasema- 'Arsh Yake ilikuwa juu ya maji." [Muslim]
Rejea pia Huwd (11:7) kwenye faida nyenginezo.
[3] Makafiri Motoni Hawatakufa Wala Hawatakuwa Hai:
Rejea Faatwir (35:36) kwenye faida ya maudhui hii.
[4] Tahadharisho La Kupendelea Dunia Badala Ya Aakhirah:
Rejea Ash-Shuwraa (42:20) na Al-Hadiyd (57:20) kwenye maelezo bayana na faida tele pamoja na rejea mbalimbali za maudhui.
[5] Suhuf (Maandiko Matukufu) Na Tofauti Baina Yake Na Vitabu Vinginenvyo Vya Mbinguni:
Kila Rasuli ameteremshiwa Kitabu lakini hatuvijui Vitabu hivyo isipokuwa Tawraat (ya Nabiy Muwsaa (عليه السّلام), Injiyl (ya Nabiy ‘Iysaa (عليه السّلام), Zabuwr (ya Nabiy Daawuwd (عليه السّلام), na Suhuf ya Nabiy Ibraahiym na Muwsaa (عليهما السلام). Rejea An-Najm (53:36-37).
Na ‘Ulamaa wamekhitilafiana kuhusu Suhuf ya Muwsaa kama hiyo ndio Tawraah au laa! Na Allaah Ndiye Mjuzi zaidi [Imaam Ibn ‘Uthaymiyn – Fataawa Nuwr Alad-Darb Kaseti (278)]
‘Ulamaa wengineo wamekhitilafiana katika kauli mbili:
Kauli ya kwanza: Suhuf na Vitabu ni kitu kimoja na kwamba Suhuf ya Muwsaa (عليه السّلام) ndio hiyo hiyo Tawraat ambayo Allaah (عزّ وجلّ) Ameiandika kwa Mkono Wake katika Al-Alwaah (Mbao) kama ilivyotajwa katika Qur-aan. Lakini Allaah (سبحانه وتعالى) Ameziita (Al-Alwaah) Mbao katika baadhi ya Aayah na Ameziita Tawraat katika Aayah nyenginezo na Ameziita Suhuf katika Aayah nyenginezo.
Kauli ya pili: Suhuf za mbinguni zinatofautiana na Vitabu vya Mbinguni na kwamba Tawraat inatofautiana na Suhuf. Tawraat ni Kitabu ambacho Allaah (سبحانه وتعالى) Alikiandika kwa Mkono Wake. Ama Suhuf ni Suhuf Alizoteremsha Allaah (سبحانه وتعالى) kwa Nabiy Muwsaa (عليه السّلام) ambayo ndani yake inabainishwa na kufafanuliwa wazi Sharia ya Tawraat kama vile Sunnah (Hadiyth) Anazoteremshiwa Nabiy Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم).
Rejea pia Al-Bayyinah (98:2).
Na Allaah Mjuzi zaidi