088- Al-Ghaashiyah
الْغَاشِيَة
088-Al-Ghaashiyah
088-Al-Ghaashiyah: Utangulizi Wa Suwrah
بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ
هَلْ أَتَاكَ حَدِيثُ الْغَاشِيَةِ ﴿١﴾
1. Je, imekujia habari ya tukio la kufunikiza (na kutoa fahamu)?
وُجُوهٌ يَوْمَئِذٍ خَاشِعَةٌ ﴿٢﴾
2. Nyuso siku hiyo zitadhalilika.[1]
عَامِلَةٌ نَّاصِبَةٌ ﴿٣﴾
3. Zifanye kazi ngumu na zichoke mno.
تَصْلَىٰ نَارًا حَامِيَةً ﴿٤﴾
4. Zitaingia moto uwakao vikali na kuungua.
تُسْقَىٰ مِنْ عَيْنٍ آنِيَةٍ ﴿٥﴾
5. Zitanyweshwa kutoka chemchem yenye kutokota.
لَّيْسَ لَهُمْ طَعَامٌ إِلَّا مِن ضَرِيعٍ ﴿٦﴾
6. Hawatokuwa na chakula isipokuwa kutokana na mti wenye miba, wenye kunuka na mchungu mno.
لَّا يُسْمِنُ وَلَا يُغْنِي مِن جُوعٍ ﴿٧﴾
7. Hakinenepeshi, na wala hakisaidii kuondoa njaa.
وُجُوهٌ يَوْمَئِذٍ نَّاعِمَةٌ ﴿٨﴾
8. Na nyuso (nyingine) Siku hiyo zitakuwa zenye kuneemeka.[2]
لِّسَعْيِهَا رَاضِيَةٌ ﴿٩﴾
9. Zitafarijika kwa juhudi zake.
فِي جَنَّةٍ عَالِيَةٍ ﴿١٠﴾
10. Kwenye Jannah ya juu.
لَّا تَسْمَعُ فِيهَا لَاغِيَةً ﴿١١﴾
11. Hazitosikia humo upuuzi wala ubatilifu.
فِيهَا عَيْنٌ جَارِيَةٌ ﴿١٢﴾
12. Humo mna chemchem inayobubujika.
فِيهَا سُرُرٌ مَّرْفُوعَةٌ ﴿١٣﴾
13. Humo mna makochi yaliyoinuliwa.
وَأَكْوَابٌ مَّوْضُوعَةٌ ﴿١٤﴾
14. Na bilauri zilizopangwa tayari.
وَنَمَارِقُ مَصْفُوفَةٌ ﴿١٥﴾
15. Na matakia yaliyopangwa safusafu.
وَزَرَابِيُّ مَبْثُوثَةٌ ﴿١٦﴾
16. Na mazulia yaliyopambwa na ya fahari yaliyotandazwa.
أَفَلَا يَنظُرُونَ إِلَى الْإِبِلِ كَيْفَ خُلِقَتْ ﴿١٧﴾
17. Je, hawawataamuli ngamia namna walivyoumbwa?[3]
وَإِلَى السَّمَاءِ كَيْفَ رُفِعَتْ ﴿١٨﴾
18. Na mbingu vipi zilivyonyanyuliwa?[4]
وَإِلَى الْجِبَالِ كَيْفَ نُصِبَتْ ﴿١٩﴾
19. Na milima vipi imekongomewa imara kabisa?
وَإِلَى الْأَرْضِ كَيْفَ سُطِحَتْ ﴿٢٠﴾
20. Na ardhi vipi ilivyotandazwa?
فَذَكِّرْ إِنَّمَا أَنتَ مُذَكِّرٌ ﴿٢١﴾
21. Basi kumbusha (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم). Hakika wewe ni mkumbushaji tu.
لَّسْتَ عَلَيْهِم بِمُصَيْطِرٍ ﴿٢٢﴾
22. Wewe si mwenye kuwadhibiti.
إِلَّا مَن تَوَلَّىٰ وَكَفَرَ ﴿٢٣﴾
23. Isipokuwa yule atayegeuka na akakufuru.
فَيُعَذِّبُهُ اللَّـهُ الْعَذَابَ الْأَكْبَرَ ﴿٢٤﴾
24. Basi huyo Allaah Atamuadhibu adhabu kubwa kabisa.
إِنَّ إِلَيْنَا إِيَابَهُمْ ﴿٢٥﴾
25. Hakika Kwetu ndio marejeo yao.
ثُمَّ إِنَّ عَلَيْنَا حِسَابَهُم ﴿٢٦﴾
26. Kisha bila shaka ni juu Yetu hesabu yao.
[1] Nyuso Za Makafiri Zitadhalilika:
Rejea ‘Abasa (80:38) kwenye kubainisha nyuso za makafiri na nyuso za Waumini zitakavyokuwa Siku ya Qiyaamah.
[2] Nyuso Za Waumini Zitang’ara Siku Ya Qiyaamah Kwa Furaha Na Kufuzu Kwake:
Rejea ‘Abasa (80:38) kwenye kubainisha nyuso za makafiri na nyuso za Waumini zitakavyokuwa Siku ya Qiyaamah.
[3] Uumbwaji Wa Ajabu Wa Ngamia Na Manufaa Yake:
Allaah (عزّ وجلّ) Anawaamrisha Waja Wake kuvitazama viumbe Vyake vinavyoashiria Uwezo na Uadhwamah (Utukufu) Wake, kwani ngamia ni kiumbe cha ajabu, na uundwaji wake ni wa ajabu kwa kuwa ana nguvu kubwa mno, lakini juu ya hivyo, anabeba mizigo mizito bila matata yoyote, na anaongozwa hata na kijana mdogo tu. Nyama yake inaliwa, maziwa yake yananywewa, na manyoya yake hutumika kwa manufaa mbalimbali. Basi Waarabu wametanabahishwa hayo kwa sababu aghlabu wa wanyama wao walikuwa ni ngamia. Na Shariyh Al-Qaadhwiy alikuwa akisema: “Tutoe nje ili tuangalie ngamia jinsi walivyoumbwa.” [Tafsiyr Ibn Kathiyr]
[4] Mbingu Zimeumbwa Bila Ya Nguzo:
Anasema Allaah (سبحانه وتعالى) katika Kauli Yake:
اللَّـهُ الَّذِي رَفَعَ السَّمَاوَاتِ بِغَيْرِ عَمَدٍ تَرَوْنَهَا ۖ
Allaah Ambaye Ameinua mbingu bila ya nguzo mnaziona. [Ar-Ra’d (13:2)]
Na pia:
خَلَقَ السَّمَاوَاتِ بِغَيْرِ عَمَدٍ تَرَوْنَهَا ۖ
(Allaah) Ameumba mbingu bila ya nguzo mnazoziona. [Luqmaan (31:10)]