Imaam Ibn 'Uthaymiyn: Mwanamke Kufanya Kazi
Mwanamke Kufanya Kazi
Imaam Ibn 'Uthaymiyn (Rahimahu Allaah)
SWALI:
“Ni zipi sehemu za kazi ya halali ambayo inawezekana mwanamke kufanya kazi hapo bila ya kwenda kinyume na mafundisho ya Dini yake?”
JIBU:
“Maeneo ya kazi kwa mwanamke ni kufanya pale mahala panapohusiana na wanawake, kwa mfano afanye kazi ya kufundisha mabinti, sawa iwe ni kazi ya idara au ni fani maalumu, au afanye nyumbani kwake kazi za kushona nguo za wanawake na mambo yanayofanana na hayo.
Ama kufanya kazi katika maeneo yanayohusiana na wanaume, hilo halijuzu kwake kufanya hivyo; kwa namna ya kwamba inamlazimu yeye kuchanganyika na wanaume, na hiyo ni fitnah kubwa sana ambayo ni wajibu kujihadhari nayo.
Na inapasa ijulikane kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) zimwendee katika yale yaliyothibiti kutoka kwake kwamba alisema:
“Sijaacha baada yangu fitnah yenye kudhuru wanaume zaidi kuliko (fitnah ya) wanawake, na kwamba baniy Israaiyl walifitiniwa na wanawake.”
[Hadiyth ya kutoka kwa Usaamah bin Zayd (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa) iliyopo katika Al-Bukhaariy na Muslim]
Ni juu ya mwanamme kumuepusha Ahli wake (mkewe) na sehemu za fitnah na kumuepusha na sababu zake (sababu za fitnah) kwa kila hali.
[Silsilat Fataawa Nuwr ‘Alaa Ad-Darb, kanda namba 94]