Kijana Kaunga Swalaah Pembeni Ya Mwanamke Kwenye Chumba Wakiwa Wawili Peke Yao

SWALI:
Naombeni kuuliza wiki iliyopita nilikuwa sehemu ambayo ina chumba kimoja cha sala kwa wanawake na wanaume. Kwahiyo wakiwahi wanawake wanaume wanasubiri. Mie wakati naswali akaja kijana mmoja labda alikuwa na haraka akaingia na kusimama safwu moja na mie akaswali. Mie alinikuta katikati ya swala khiyo sikuweza kuikata. Je hapo swala zetu ziliswihi?

 

Ufafanuzi:
Muulizaji ni mwanamke. Na inavyoonekana, siyo kwamba aliunga swala ya mwanamke, bali alikuja akasimama usawa mmoja na mwanamke

 


JIBU:
Kwa hali hiyo kama ulivyofafanua hilo swali, jambo hilo halifai kishariy'ah,
Ni haraam mwanamke kuwa faragha na mwanamme asiye Mahram (Maharimu) yake. Na kinyume chake vilevile mwanamme haifai kuwa faragha na mwanamke asiye Mahram wake. Iwe kwenye Swalaah au kwenye mazingira mengine.
Wanachuoni wanaeleza kanuni kuwa, kile kinachopelekea kwenye haraam nacho ni haraam.

 

Ziko Ahaadith nyingi zenye kuharamisha faragha baina ya jinsiya mbili zisizo na mahusiano ya damu au mke na mume, kuwa faragha.

 

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

'Mwenye kumuamini Allaah na siku ya mwisho basi asikae peke yake na mwanamke asiyekuwa na maharimu wake pamoja naye, kwani watatu wao ni Shaytwaan' [Ahmad]

 

“Hakai mwanamme na mwanamke peke yao (faragha) ila watatu wao ni Shaytwaan”. [At-Tirmidhiy]

 

Na akasema tena:
“Shaytwaan hutembea kwenye mwili wa binaadamu kama damu (inavyotembea kwenye mishipa)”.

 

Na akasema tena:
"Asikae faragha mmoja wenu na mwanamke isipokuwa awe pamoja na maharimu wake." [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Na akasema tena:
"Tahadharini na kuingia kwa wanawake'. Akasema mmoja katika Answaar, 'Ee Mtume wa Allaah, unaonaje jamaa zake mume (shemeji)?' Akajibu: 'shemeji ni mauti." [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Na akasema tena akiwa kwenye Minbari siku moja:
"Baada ya leo, hapaswi mwanamme yeyote kuingia kwa siri kwa mwanamke ambaye mume wake hayupo, ila isipokuwa awepo mwanamme mwengine au wanaume wawili pamoja naye." [Muslim]

 

Makusudio hapo, ni kuwa, mwanamme asiingine nyumba ya mwanamke yeyote ambaye ni mke wa mtu, au yule mwanamke ambaye hajaolewa lakini si Mahram yake, ila kuwepo na watu wengine pamoja naye au pamoja na huyo mwanamke. Vilevile mwanamme asiingie mahali wako wanawake watupu ambao si Mahram zake.

 

Kwa dalili zote hizo, kunaonesha ubaya na uharamu wa mwanamme na mwanamke kuwa faragha peke yao kwenye eneo lolote lile na hata kwenye Swalaah.

 

Maimaam na Wanachuoni wametoa ufafanuzi zaidi kuhusu hilo, kwa kueleza kuwa, ikiwa wanawake watakuwa wengi na mwanamme ndiye mwenye kuongoza Swalaah, hilo linawezekana lakini ni makruuh. Linawezekana kwa sababu wanaona uwezekano wa kuwepo fitnah wakiwa wengi, si mkubwa kama ilivyo wawili peke yao. Na wanaona makatazo na uharamu ni pale wanapokuwa wawili faragha. Lakini wakiwa wengi, na mwanamme mwenye kuongoza Swalaah ni mtu mwenye kuaminika, basi inakubalika japo kuna karaha ndani yake. Likiepukika pia hilo, basi ni bora zaidi ili kufunga milango na penyo zote za fitnah.

 

Ama tukirejea kwenye qadhwiyyah hiyo ya muulizaji, ni kuwa kitendo kile kilikuwa hakifai kishariy'ah na wanapaswa wafanye tawbah kwa hilo na kama walikuwa hawajui hukmu basi wajihadhari mbeleni na huyo kijana aelimishwe kwani anaonekana ni Jaahil wa shariy'ah za Dini.

 

Na Allaah ni Mjuzi zaidi.

 

 

Share