Swalaah Karibu Na Makaburi Inafaa?

 

SWALI: 

Assallam Allaykum

 

Kwanza kabisa namuomba Mwenyezi Mungu awajalie kila lilo jeme na awazidishie nguvu katika kutangaza Uislam ktk website hii.   

 

Swali:
Je inaswihi kuswali katika msikiti uliojengwa katika maeneo ya makaburi, wengine wanasema alimradi makaburi yasiwe sehemu ya Qibla, wengine husema alimradi kuna kizuizi mbele inaswihi, pia wapo wanabisha wakataka wapewe AYA inayokataza kuswali mababurini. Naomba mnisaidi ili niweze kupata kauli ilodhati.

 

Ni ndugu yenu katika Uislam,  

 


 

 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allah Aliyetukuka Mola  wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ahli zake, Sahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum jamiy'an) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani kwa swali lako hili ambalo tayari limetupatia sisi muelekeo au kutuongoza kwa mambo ambayo umesema ni rai za watu katika suala hilo. Inataka ifahamike kabla ya sisi kulijibu swali hili kuwa si kila kitu utapata utajo wake moja kwa moja kutoka kwa Qur-aan. Ndio tukawa na nyenzo za sheria katika Dini yetu, nazo ni:

1.    Qur-aan.

2.   Sunnah au Hadithi za Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).

3.    Ijmaa' ya Maswahaba na wanavyuoni.

4.    Qiyasi.

Vipo vitu kama sigara au mirungi havijatajwa katika Qur-aan moja kwa moja wala idadi ya rakaa ya Swalah za Faradhi pia hazijatajwa katika Qur-aan. Lakini hivi ni vitu ambavyo vinapatikana katika nyenzo nyengine za sheria ya Kiislamu. Aayah ya moja kwa moja inayokataza hakuna lakini ipo aayah inayotuamuru hivi: ((Na anachokupeni Mtume chukueni, na anachokukatazeni jiepusheni nacho. Na mcheni Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mkali wa kuadhibu)) (59: 7).

 

Katika suala hili wenye Fataawaa Islaamiyyah (shaykh ‘Abdul-‘Aziz ibn Baaz, Shaykh Muhammad al-‘Uthaymin na Shaykh ‘Abdillah al-Jibriin) wamesema: “Ikiwa misikiti haikujengwa kwa sababu ya makaburi na Swalah haikuandaliwa karibu na makaburi hayo kwa ajili ya makaburi na kuwatukuza wafu au kupata thawabu zaidi kwa kuswali na kujileta karibu na Allah ndani yake, kunaruhusiwa na Swalah hapo ipo katika sheria.

 

Sehemu hizi zinaweza kutazamwa vyema kwa ajili ya kutekeleza Swalah ndani yake na amali nyengine za kujikurubisha kwa Allah, na hili ni jambo linalopendeza kidini. Ikiwa upo ukuta unaotenganisha makaburi na msikiti hiyo itatosha na ile sehemu ambayo haikuzungukwa na ukuta, inatakiwa ujengwe (ukuta au boma) kutenganisha hivyo vitu viwili. Ikiwa ni rahisi kuacha nafasi baina ya ukuta wa msikiti na pia kuweka ukuta wa makaburi, hiyo itakuwa ni vizuri zaidi. Hata hivyo, ikiwa kujengwa kwa msikiti karibu na makaburi ni kwa ajili ya kuyatukuza hayo makaburi, hivyo itakuwa haifai kuswali ndani yake na italazimu kuuvunja msikiti huo. Kwa sababu kuijenga kwa aina hii ni njia ya kuwapelekea watu katika shirki.

 

Hakika imethibiti kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa amesema: “Msiswali kuyaelekea makaburi wala musikae juu yake” (Muslim).

 

Pia amesema: “Jueni ya kwamba wale waliokuwa kabla yenu walikuwa wakiyachukua makaburi ya Manabii wao na watu wao wema kuwa Misikiti. Jueni, musiyafanye makaburi kuwa Misikiti, hakika mimi nimewakataza nyote hilo” (Muslim)”.

Lakini kaburi likiwa ndani ya Msikiti itakuwa haifai kabisa kwa Muislamu kuswali ndani yake na inabidi ima Msikiti uvunjwe au kaburi lichimbwe na mabaki ya maiti ihamishwe sehemu nyengine. Na hili litafanyika ikiwa kaburi likuwa hapo mbeleni itabidi Msikiti uvunjwe na ikiwa Msikiti ulikuwa hapo mwanzo itabidi mabaki ya maiti yahamishwe na yazikwe sehemu ya makaburi baada ya kufukuliwa. 

Na Maulamaa wanaona ikiwa kaburi/makaburi na Msikiti yapo katika kiwanja kimoja na mbele ya Qiblah itakuwa haifai

Na rai ya Shaykhul Islaam Ibn Taymiyah katika Fataawa yake amesema ikiwa hali ni hiyo ni kuwa makaburi yalikuwa pale mwanzo basi Msikiti utavunjwa au ikiwa Msikiti ulikuwa mwanzo basi makaburi yatahamishwa. Na Shaykh Shanqiitwiy katika tafsiri yake Adhwaa' ul Bayaan amesema haifai.

Kwa tahadhari ni vizuri zaidi makaburi yawe mbali na Misikiti ili isiwapelekee Waumini kidogo kidogo katika shirki ya kuyatukuza hayo makaburi au waliozikwa ndani yake.

Lakini ni bora kuzuia kumpeleka mtu katika shirki au kutukuza waliozikwa katika makaburi hayo (Sadu-dh-Dharia) kutoswali katika msikiti huo. 

Na Allah Anajua zaidi.

Share