Ummu 'Atwiyyah: Nusaybah Bint Al-Haarith Al-Answaariyyah (رضي الله عنها)
Ummu ‘Atwiyyah Nusaybah Bint Al-Haarith Al-Answaariyyah (رضي الله عنها)
Ummu ‘Atwiyyah ni mmoja katika wanawake wa kiislaamu ambao historia haitowasahau kwa mchango wao mkubwa walioutoa katika Jihaad, elimu ya Fiq-h na pia kupokea Hadiyth. Mara nyingi jina lake huchanganywa na la Nusaybah bint Ka’ab ambaye alikuwa kinga ya Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika vita vya Uhud.
Ummu ‘Atwiyyah alitokea Madiynah na alisilimu mapema ulipofika Uislaam katika mji wa Madiynah pale Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipomtuma Mus’ab ibn ‘Umayr kwenda kuwafundisha na kuwalingania dini.
Hatuna haja ya kuutaja wasifu wake lakini tuutathmini mchango hasa katika vita vya Jihaad kama anavyosimulia mwenyewe.
عن أم عطية رضي الله عنها قالت: غزوت مع النبي صلى الله عليه وسلم سبع غزوات أخلفهم في رحالهم، فأصنع لهم الطعام، وأداوي الجرحى، وأقوم على المرضى
Kutoka kwa Ummu ‘Atwiyyah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa): Nilikuwa nikipigana vita pamoja na Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika vita saba nikibaki nyuma kwenye mizigo yao nikiwapikia chakula na kuwatibu majeruhi na kuwahudumia wagonjwa.
Haya ndiyo yalikuwa majukumu ya mwanamama shujaa aliyediriki kushiriki takriban vita vyote alivyopigana Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Kwani katika vita vya Khaybar, Ummu ‘Atwiyyah pia alikuwa ni miongoni mwa wanawake ishirini walioshiriki kwa ajili ya kupata ujira wa Jihaad.
Ama katika majala ya Fiq-h, Ummu Atwiyyah alikuwa ndiye mkoshaji mkubwa wa maiti za akinamama katika mji wa Madiynah enzi za Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Ni yeye aliemuosha Zaynab bint Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipofariki kama anavyosimulia katika moja ya hadiyth zake:
Kutoka kwa Ummu ‘Atwiyyah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa):
لما ماتت زينب بنت رسول الله صلى الله عليه قال: (اغسلنها وتراً ، ثلاثاً أو خمساً ، واجعلن في الآخرة كافوراً أو شيئاً من كافور ، فإذا غسلتنها فأعلمنني) فلما غسلناها أعطانا حقوه ، فقال: (أشعرنها إياه)
Alipokufa Zaynab bint wa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Akasema: “Mkosheni witr – mara tatu au mara tano na jaalieni katika josho la mwisho Kaafur au kitu kidogo katika Kaafuur na mkishamaliza niiteni”. Tulipomaliza tulimuita na akaturushia shuka yake anayovaa kiunoni na kusema iwekeni jirani yake.
Ni kutokana na maneno ya Ummu ‘Atwiyyah ndivyo tulivyojua kwamba tunapoanza kuosha mayyit wetu tuanze upande wake wa kulia na katika sehemu tunazoziosha wakati wa kutia wudhuu kama ilivyosimuliwa na Al-Bukhaary na Muslim.
Ni kutokana na hadiyth ya Ummu ‘Atwiyyah ndivyo tulivyojuwa kwamba akinamama wamekatazwa kusindikiza jeneza kama anavyosimulia:
نهينا عن اتباع الجنازة ، ولم يعزم علينا
Tulikatazwa kulifuata Jeneza ingawa haikuwajibishwa juu yetu.
Ummu ‘Atwiyyah hakuwa mpokezi wa hadiyth tu bali pia alikuwa ni mwenye kuuliza na kutaka ufafanuzi katika masaail mengi kutoka kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).
Aliwahi kumuuliza Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) pale alipowaamrisha akinamama na wanawake kutoka kwenda kuswali Swala ya ‘Iyd kwamba: Je, asiyekuwa na nguo ya kujistiri anaweza kuruhusiwa kubaki nyumbani asiende kuswali? Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: “Na amuazime mwenzake”
Na hapa tunapata maelekezo ya kielimu jinsi Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alivyowaamrisha wanawake kutoka kwenda kuswali hata watoto wadogo, wanawari na wenye hedhwi na walitakiwa kubaki nyuma na wanaoswali wakileta Takbiyr (za ‘Iyd) na wao huleta na wakiomba du’aah pia huitikia kama ilivyosimuliwa na A-Bukhaariy na Muslim.
Na katika upande wa hadiyth, Ummu ‘Atwiyyah ni miongoni mwa kinamama waliobahatika kusimulia hadiyth nyingi kutoka kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Inasemekana alikuwa na hadiyth zinazofika arubaini na sita kati ya hizo zimo kwenye Swahihi A-Bukhariy na Muslim. Pia hadiyth zake hupatikana katika vitabu vyengine vinavyotegemewa.
Miongoni mwa Maswahaba wakubwa kama Anas Ibn Maalik (Radhiya Allaahu ‘anhu) pia alipokea baadhi ya hadiyth kupitia kwake. Kama walivyopokea Taabi’iyn kama kina Muhammad ibn Siriyn na dada yake Hafswah bint Siriyn na wengineo.
Baadae alihamia Baswrah ambapo alisifika kwa ‘ilmu yake na waislaamu wengi walifaidika na kunufaika kupitia kwake. Baadhi ya Maswahaba na hata Taabi’iyn walidiriki kufanya safari kwenda Baswra kwenda kumsikiliza Ummu ‘Atwiyyah katika masaail mengi ya kifiq-h na uoshaji wa mayyit.
Alifariki Baswrah akiwa na takriban miaka 70 katika umri wake (Radhwiya Allaahu ‘anhu)