Kubusiana Au Kukumbatiana Hadharani Na Mbele Ya Watoto Inajuzu?

SWALI:

 QUESTION: is it wrong in ISLAM 4 a couple (husband and wife, ofcourse) 2 show affection 4 each other in public or infront of their kids????

i mean nothing VULGAR.... for example if they hold hands in public OR kiss each other OR one leans on the other OR if they feed each other.... that kind of stuff.

AND if its not wrong THEN what is the limit bcoz our society keeps saying everything is "3eib" but is it REALLY wrong in islam?

please can u answer that 4 me coz its bothering me coz i don't see any show of affection btwn muslims in this world and i want 2 know if we r making things haram when they aren't!!!

 




JIBU:

AlhamduliLLah,  Waswalaatu Was-salaam 'alaa Rasuli-Llah  صلى الله عليه وآله وسلم Amma ba'ad,

Ingawa swali la ndugu yetu limekuja kwa lugha ya kiingereza, sisi tutalijibu kwa kiswahili kama ilivyo tovuti hii. Na kama tulivyosema awali, hatubadilishi swali la mtu au kulirekebisha, bali tunaliweka kama lilivyo.

 

1.     Kuonyesha mapenzi hadharani.

Jambo hili halifai kabisa, kwani ni mambo ya kuiga makafiri ambao tabia zao kama za wanyama khaswa katika mambo haya, kwani unaweza kuwaona njiani wakifanya mapenzi bila ya kuwa na haya. Dini yetu imekamilika kwa kutupa kila aina ya mafunzo. Na katika mafunzo ya mapenzi baina ya mume na mke, Mtume صلى الله عليه وآله وسلم amekataza mume au mke hata kuelezea nje yale wanayofanya baina yao. Sasa vipi mume na mke wa Kiislamu waonyeshe mapenzi yao hadharani? Bila shaka ni jambo la fedheha na lisilopendeza. Inatupasa tujiweke katika stara na tutunze heshima zetu, kwani kuonyeshana mapenzi njiani wengi wanaona ni fakhari, wakati khaswa ni ujinga wa kutaka kuiga tabia za makafiri na kuacha mafundisho yetu yaliyo mema na yenye faida kubwa ndani yake. 

Na wala haiwi kuonyesha penzi hadharani ndio kielelezo cha kuwa watu wanapendana hivyo, wengi hufanya kutaka kujionyesha tu kwa watu na hali huenda ikawa nyumbani kwao ni kinyume na hivyo.   

Ikiwa mwanamke hatakiwi atoke nje bila ya sababu muhimu kama anavyosema Allaah سبحانه وتعالى :  

((وَقَرْنَ فِي بُيُوتِكُنَّ وَلَا تَبَرَّجْنَ تَبَرُّجَ الْجَاهِلِيَّةِ الْأُولَى))

((Na kaeni majumbani kwenu, wala msijishauwe kwa majishauwo ya kijahilia ya kizamani)).[Al-Ahzaab:33]

Seuze mwanamke awe nje kisha ajishauwe kwa mambo kama hayo? 

 

2.     Kuonyesha mapenzi mbele ya watoto:

Inaweza kufaa ikiwa ni kukumkumbatia bila ya matamanio na kumbusu mke kwenye kipaji, kwani Mtume صلى الله عليه وآله وسلم alikuwa akimbusu 'Aishah ndio maana wengi wa Maulamaa wamechukulia kuwa udhuu wa mtu hauvunjiki kwa kuguswa na mume au kubusiwa kama hivyo bila ya matamanio. Lakini kama ni kukumbatiana  au kubusiana ambako mume na mke wanafanyiana wakiwa peke yao, yaani kwa matamanio, basi haifai kufanya mbele ya watoto.

Allaah سبحانه وتعالى Ametupa mafundisho ya tabia nzuri za watoto wanapotaka kuingia vyumbani kwa wazazi wao, na Ametoa mafundisho tofauti kwa wasio beleghe (yaani watoto wadogo) kuwa wao wanaweza kuingia wakati wowote bila ya kupiga hodi ila nyakati tatu tu. Hii inatufahamisha kuwa nyakati hizo tatu ndizo nyakati za kupumzika na kustarehe  baba na mama na  ambazo aghlabu huwa katika hali ya mapenzi kwa hiyo hata hao watoto wadogo hawafai kuwaona wazazi wao wakifanya mapenzi japokuwa ni mapenzi ya kubusiana tu lakini yenye matamanio.

Na Walio baleghe nao pia wana mafundisho khaswa yao kuwa wao WAKATI WOTE wanapotaka kuingia kwa wazazi wao lazima wapige hodi. Kwa hiyo hii inatupa fundisho kuwa kuna mipaka na heshima kubwa inayotakiwa iweko baina ya wazazi na watoto wao khaswa wakubwa. Allaah سبحانه وتعالى Anasema:

((يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لِيَسْتَأْذِنكُمُ الَّذِينَ مَلَكَتْ أَيْمَانُكُمْ وَالَّذِينَ لَمْ يَبْلُغُوا الْحُلُمَ مِنكُمْ ثَلَاثَ مَرَّاتٍ مِن قَبْلِ صَلَاةِ الْفَجْرِ وَحِينَ تَضَعُونَ ثِيَابَكُم مِّنَ الظَّهِيرَةِ وَمِن بَعْدِ صَلَاةِ الْعِشَاء ثَلَاثُ عَوْرَاتٍ لَّكُمْ لَيْسَ عَلَيْكُمْ وَلَا عَلَيْهِمْ جُنَاحٌ بَعْدَهُنَّ طَوَّافُونَ عَلَيْكُم بَعْضُكُمْ عَلَى بَعْضٍ كَذَلِكَ يُبَيِّنُ اللَّهُ لَكُمُ الْآيَاتِ وَاللَّهُ عَلِيمٌ حَكِيمٌ))   

((Enyi mlio amini! Nawakutakeni idhini iliyowamiliki mikono yenu ya kulia na walio bado kubaalighi miongoni mwenu mara tatu - kabla ya Swalah ya alfajiri, na wakati mnapovua nguo zenu adhuhuri, na baada ya Sala ya 'ishaa. Hizi ni nyakati tatu za faragha kwenu. Si vibaya kwenu wala kwao baada ya nyakati hizi, kuzungukiana nyinyi kwa nyinyi. Hivyo ndivyo Mwenyezi Mungu  anavyokuelezeni Aya zake, na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi    Mwenye hikima))[An Nuur:58]

Ibn Kathiyr amesema: Hapa watumishi na watoto wameamrishwa wasiingie tu kwa wazazi wao vyumbani nyakati hizi isijekuwa wako katika hali ya mapenzi na kadhalika [3/401]

((وَإِذَا بَلَغَ الْأَطْفَالُ مِنكُمُ الْحُلُمَ فَلْيَسْتَأْذِنُوا كَمَا اسْتَأْذَنَ الَّذِينَ مِن قَبْلِهِمْ كَذَلِكَ يُبَيِّنُ اللَّهُ لَكُمْ آيَاتِهِ وَاللَّهُ عَلِيمٌ حَكِيمٌ ((

((Na watoto wanapofikilia umri wa kubaalighi basi na watake ruhusa, kama walivyotaka ruhusa wa kabla yao. Hivyo ndivyo anavyokubainishieni Mwenyezi Mungu Aya zake, na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi Mwenye hikima)) [An-Nuur:59]

Kwa hiyo ikiwa watoto wamekatazwa kuingia kwa wazazi wao ili wasije kuwaona wanapofanya mapenzi, vipi wazazi wafanye mapenzi mbele ya watoto wao, kama kubusiana (midomo, kunyonyana) na kadhalika?

Hatukupata mafundisho kutoka kwa Mtume صلى الله عليه وآله وسلم au Maswahaba kuwa walikuwa wakifanya hivyo, kwa hiyo na sisi ni wajibu wetu kufuata nyendo zao. 

Mume au mke wanaweza kulala pamoja mbele ya aila zao bila ya kuwa katika hali ya mapenzi kama ilivyothibiti katika Hadiyth ifuatayo:

Imepokelewa kutoka Kurayb, mtumwa wa 'Abdullah bin 'Abbaas aliyeachwa huru kwamba, 'Abdullah bin 'Abbaas alimwambia kuwa alikaa usiku mmoja na Maymuunah, mke wa Mtume صلى الله عليه وآله وسلم ambaye ni ndugu wa mama yake.  Amesema: Niliweka kichwa changu mwisho wa mto na Mtume صلى الله عليه وآله وسلم na mkewe waliweka vichwa vyao pembezoni mwake. Mtume صلى الله عليه وآله وسلم alilala mpaka usiku wa manane, au karibu na usiku wa manane, kisha Mtume صلى الله عليه وآله وسلم akaamka na kuanza kufikicha macho yake kwa mikono yake kujitoa usingizi, kisha akasoma aya za kumi za mwisho katika Suratul-'Imraan)) [Al-Bukhaariy na Muslim]  


An-Nawawy (r.a) amesema, hii inaonyesha kuwa inaruhusiwa kwa mume kulala karibu na mkewe bila ya kuwa katika hali ya mapenzi mbele ya Mahram wao hata
kama kafikia umri wa kubaleghe. 

Tabia hiyo ya kufanya mapenzi mbele ya watoto huenda ikaleta athari mbaya kwa watoto, kwani na wao wataiga hivyo hivyo, kwani msingi wa tabia njema au mbaya unatokana na wazazi wenyewe na mafunzo yao.   

Ama kama tulivyosema hapo juu kuwa kubusiana na kukumbatiana bila ya matamanio inafaa mbele ya watoto khaswa kama siku za 'Iyd na kadhalika ili watoto wawe na matumaini ya kuona wazazi wao wako katika maisha ya masikilizano, yenye furaha na mapenzi, madamu tu hawatovuka mipaka katika kuonyesha mapenzi hayo.

 3.    Kuonyesha mapenzi baina ya Waislamu

Kuna njia nyingi za kuonyeshana hisia au upendo baina ya Waislamu, na sio lazima ziwe kama njia hizi zisizokuwa za heshima ambazo tu si kuvuta macho ya watu kuwatazama, bali pia inaingia na hali ya kujionyesha.

Miongoni mwa njia za kuonyeshana mapenzi baina ya Waislamu ni  kujuliana hali kwa kutembeleana au kwa simu, kusaidiana katika shida, kualikana, kununuliana zawadi na kadhalika. Pia kushikana mikono hadharani hakukatazwi.

Wa Allaahu A'alam

 

Share