Kumwita Mtoto Jina La Maulaana

Kumwita Mtoto Jina La Maulaana

 

www.alhidaaya.com

 

 

SWALI:

 

Je naweza kumwita mtoto wangu jina lake "Mulana" bin fulani?

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Kama tunavyokariri kusema kila wakati kuwa Uislaam ni Dini kamili inayokidhi mahitaji yote ya mwanaadamu. Uislaam ni mfumo kamili wa maisha katika kila nyanja katika masaa 24 ya kila siku yetu. Uislaam umetupatia muongozo katika mas-ala ya kiuchumi, kijamii, kisiasa, kiafya na mengineo mengi. 

 

 

Katika mfumo huu kamili Uislaam umetupatia muongozo kuhusu kupeana majina. Hii ni ada ya kijamii ya mtoto kupatiwa jina azaliwapo. Uislaam umetilia maanani sana jambo hili na kuliwekea hukumu zake. Kwa hilo.  

 

 

Na Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  ametuwekea mfumo ambao tunaupata katika dondoo zifuatazo:

 

 

1-Inafaa mzazi amchagulie jina zuri mtoto wake kama alivyosisitiza hilo Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  "Kwa yakini siku ya Qiyaama mtaitwa kwa majina yenu na kwa majina ya baba zenu. Basi yaboresheni majina yenu" [Abu Daawuwd].

 

2-Amesema pia Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): “Majina yaliyo bora kuitwa mtoto ni 'Abdullaah na Abdur-Rahmaan [Muslim].

 

3-Haifai kwa mzazi kumpatia mtoto wake jina baya. Hilo limekatazwa na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  mpaka akawa anayabadilisha majina hayo. 'Aaishah (Radhiya Allaahu 'anhas) amesema: "Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akilibadilisha jina baya" [[at-Tirmidhiy].

 

Hadiyth nyengine pia imethibiti:

 

Binti fulani wa Ibn 'Umar alikuwa akiitwa  Aaswiyah (muasi), Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akambadilisha na kumuita Jamiylah (mzuri) [at-Tirmidhiy na Ibn Maajah].

 

5-Mzazi asimuite mtoto jina linaloashiria ukorofi na kisirani. Babu yake Sa'iyd bin Muswayyib amesema: "Nilimwendea Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akaniuliza: 'Nani jina lako?' Nikamwambia: 'Naitwa Hazn (gumu)'. Akasema: 'Wewe ni Sahl (wepesi)'" [al-Bukhaariy].

 

6-Haifai kumuita mtoto jina ambalo ni maalum kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)   kama vile Al-Ahad (Mmoja pekee), Asw-Swamad (Mwenye kukusudiwa kwa haja zote),   Al-Khaaliq (Muumbaji), Ar-Razzaaq (Mwenye kuruzuku), na kadhalika. Yupo mtu ambaye alipewa lakabu na kaumu yake ya Abal Hakam (baba wa hukumu) lakini Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  akambadilisha na kumuita Abuu Shurayh (baba wa mtoto wake mkubwa Shurayh). Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Aliye khabithi mno siku ya Qiyaama ni yule aliyejiita Malikul-Al-Amlaak (mfalme wa wafalme) kwani hakuna mfalme ila Allaah. [Al-Bukhaariy]

 

7-Mzazi anafaa ajiepushe na majina yenye baraka au fali njema ili isije ikaleta karaha kujibu hayupo wakati aitwapo. Majina hayo ni kama Aflah (aliyefaulu), Naafi (mwenye manufaa), Yasaar (usahali). Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Maneno yapendezayo zaidi kwa Allaah ni manne: Subhaana-Allaah, Alhamdullillah, laa ilaaha illa-Allaah, na Allaahu Akbar. Usimuite mwanao Yasaar, wala Rabaah wala Najiyh wala Aflah. Kwani utauliza: 'Yuko huko?' Halafu mtu aseme: 'Laa (hayuko)'. Hayo ni manne, msinizidishie" [Muslim, Abu Daawuwd na at-Tirmidhiy].

 

8-Haifai kumwita mtoto majina yanayoabudishwa asiyekuwa Allaah kama vile 'Abdul'uzza (mja wa 'uzza   (jina la sanamu), 'Abdulka’bah (mja wa Ka'bah), 'Abdunabiy (mja wa Nabiy), ‘Abdurasul (mja wa Rasuli) na kadhalika.

Hizi ni baadhi ya kanuni ambazo zipo katika Uislaam lau tutazifuata basi hatutapata shida katika kuwachagulia watoto wetu majina yaliyo mazuri.

 

Ama kuhusu swali lako ikiwa tutakuwa tumekuelewa vyema unaposema Mulana labda unamaanisha Mawlaanah (lenye maana ya Mola au bwana, mtukufu), hivyo haifai kumwita mtoto kwa makusudio ya maana hizo.

 

Neno Mawlaanah kwa lugha nyengine kama Ki-Urdu lina maana tofauti. Maana yake ni Shaykh kwa huku kwetu, yaani mtu mwenye ilimu ndio utapata katika vitabu vilivyoandikwa na Wananzuoni wa Pakistan au India kwa mfano Mawlana Abulhasan 'Aliy Nadwi, na kadhalika.

 

Na Allah Anajua zaidi

 

Share