Njia Gani Inayopasa Katika Shari'ah; Kuzuia Au Kupanga Uzazi?

SWALI:

 

Asalam Aleikum, Inshallah natumai mpo wazima.

I have two questions: Inshallah am planning to get do my nikah in August and I want to know which ways are safe for family planning. I have read a lot of books about family planning and Islam but they all don’t agree with family planning. I want to have kids but I can’t have kids each and every year. So I want to know which way is permissible in Islam. Massallam


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu uzazi wa mpango. Uislamu ni mfumo kamili wa maisha na hivyo hakuna lolote isipokuwa umetuelezea kinaganaga.

 

Mwanzo inatakiwa tufahamu kuwa miongoni mwa malengo ya kuoa au kuolewa ni kuongeza jinsi ya mwanadamu hapa duniani. Kwa ajili hiyo, Uislamu ukapiga marufuku kabisa kufunga kizazi ili wanandoa wasiweze kuzaa. Hiyo ilitokea pale 'Uthmaan bin Madh'uwn (Radhiya Allaahu 'anhu) alipotaka kujihanithisha, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimkataza. Na pia (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: "Hakuna utawa katika Uislamu". Utawa ni mwanaume kukaa bila ya kuoa na mwanamke bila kuolewa kama wanavyofanya watu wa Dini nyinginezo.

 

Ni kwa ajili hiyo ndio al-Bukhaariy na Muslim wanatuelezea kuwa walikwenda watu watatu katika nyumba ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kuulizia kuhusu ‘Ibaadah ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Walipoelezewa waliiona kuwa ni kidogo sana. Mmoja wao aliamua kutolala usiku awe anaswali tu, mwengine kutooa na wa mwisho kufunga kila siku. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwakataza na akawataka wafuate mfumo wake kamili wa maisha. Akamalizia Hadiyth kwa kusema: "Yeyote anayekengeuka na Sunnah yangu si katika mimi".

 

Ama kupanga kizazi kwa muda haina tatizo katika Uislamu lakini isiwe kwa kisingizio cha kuwa sina cha kuwalisha watoto. Allaah Aliyetukuka Anasema:

"Wala msiwaue watoto wenu kwa kuogopa umasikini. Sisi ndio Tunaowaruzuku wao na nyinyi. Kwa yakini kuwaua ni hatia kubwa mno" (17: 31).

Katika njia zisizo na madhara ziliyoidhinishwa na Uislamu ni kama zifuatavyo:

 

  1. ‘Azl, nayo ni kumwaga maji ya uzazi nje ya utupu wa mkeo unapohisi ya kuwa uko tayari kutoa mbegu za uzazi. Njia hii ni lazima mume na mke waridhiane.
  2. Kunyonyesha baada ya kuzaa kwa miaka miwili.
  3. Mbali na hizo mbili pia kuna kufuata kalenda kwa kuelezewa kuhusu ada yako na daktari aliyebobea katika masuala hayo. Siku ambayo si salama mkajiepusha kujamiiana ili kuondosha uwezekano wa kushika mimba.

 

Ama mbali na hizo, njia za kuzuia uzazi kama zile za kupiga sindano, kula vidonge na nyingine zina hatari sana kwa siha ya mwanamke tu kama wanavyosema madaktari. Ikiwa hakutakuwa na budi ila kuzuia kwa muda kwa sababu ya afya au sababu nyingine yoyote inayokubaliwa kisheria inabidi upate daktari Muislamu, Mchaji aliyebobea akupe ushauri kuhusu dawa ambayo itakuwa na madhara kidogo zaidi kuliko nyingine. Pia upate kutoka kwake ushauri kuhusu hilo. Ikiwa hayo yatazingatiwa utaweza kutumia njia nyingine. Lakini njia ambayo ni salama zaidi ni hizo tatu tulizoziorodhesha.

 

Ingia pia katika viungo vifuatavyo upate faida zaidi:

 

Utumiaji Wa Mpira (Condom)

 

Utumiaji Kondom Kwa Mke Anaedai Kuwa Ni Mgonjwa

 

Kupanga Uzazi Na Sio Kuzuia Uzazi

 

Uzazi Wa Kupanga Unafaa?

 

Kuzuia Mimba Na Madhara Yake

 

20 Kuhalalishwa ‘Azl (Kuchopoa Kabla Ya Kushusha)

 

21 Kutofanya ‘Azl Ni Bora Zaidi

 

Vilevile ndugu yetu tunakunasihi na kukuzindua kuwa kabla hujaanza kufikiria kufunga uzazi au kupanga uzazi, na hali hujaolewa wala kuruzukiwa mtoto, kwanza omba ndoa yako ikamilike na muombe sana Allaah Akuruzuku mwana/wana, tena wa kheri. Unaweza kuwa unafikiria na kupanga ya mbele ambayo hayako kwenye uwezo wako, bali jitahidi umuombe Allaah Akuwafikishe katika hayo.

 

Tunakutakia Arusi njema na mtangamane na mumeo kwa njia nzuri na mdumu katika mapenzi yenu na wala msigombane kwa njia yoyote ile.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share