Kutamani Mtoto Na Kufanya Juhudi Za Kujua Jinsia Yake

SWALI:

 

Salaam a.w.w.mimi ni msichana mwenye miaka 22, nakaa na mume wangu na baada ya kujaribu sana kupata mtoto mwenyezi mungu ametujaalia na sasa nina mimba ya miezi mi5, ALHMDLILLAH. Swali langu nataka kujua kama ukitamani mtoto wa kiume na kumwomba mungu akupe mtoto wa kiume ni dhambi yaani unakosea? Na pia kujua jinsia ya mtoto kabla ya kuzaliwa ni haram? JAZAKUM ALLAH KHEYR

 


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukran kwa swali lako kuhusu kutamani mtoto wa jinsia fulani.

Hakuna kosa la mtu kutamani mtoto wa aina ya jinsia fulani – ima msichana au mvulana lakini ni makosa kabisa mtu aliye Muislamu kuomba kuwa mimi nataka mtoto wa kiume au wa kike.

Hii ni kinyume na du’aa za watu wema wakiwemo Mitume (‘Alayhimus Salaam). Bali inatakiwa uombe huyo umtakaye lakini awe mwema kwani ukipata mtoto wa kiume wa aina yoyote akija kuwa mkorofi utakuja juta katika maisha yako na hamu yote ya huyo mtoto itakuishia.

 

Tazama Nabii Ibraahiym (‘Alayhis Salaam) alivyomuomba Muumba wake Aliyetukuka:

Ewe Mola wangu! Nitunukie aliye miongoni mwa watenda mema” (asw-Swafaat [37]: 100).

 

Naye Nabii Zakariyyaa (‘Alayhis Salaam) alivyoomba:

Pale pale Zakariyyaa akamwomba Mola wake, akasema: Mola wangu! Nipe kutoka kwako uzao mwema. Wewe ndiye unayesikia maombi” (al-‘Imraan [3]: 38).

 

Na watu wema wanaomba:

Na wale wanaosema: Mola wetu! Tupe katika wake zetu na wenetu yaburudishayo macho” (al-Furqaan [25]: 74).

 

Na hivyo ndivyo unavyotakiwa kuomba mtoto mwema ewe ndugu yetu mpendwa.

 

 

Tafadhali bonyeza kiungo kifuatacho upate maelezo zaidi:

 

Kujua Aina Ya Mtoto Aliyeko Tumboni Kwa Ultra Sound Kabla Hajazaliwa

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share