Kodi Ya Serikali Ni Lazima Kuilipia?
SWALI:
Asalaam Alaikum W. W.
Suala langu linahusika na kodi za kulipia katika serikali zetu, kuna kodi ambazo tunatakiwa kulipa kama za taka na karo na kuna kama hizo ambazo kwa kweli gharama zake ni kubwa kwa kutokana na uwezo wetu ni mdogo kwa kulipia gharama zote kutokana na kipato chetu, na utakuta wasimamizi na wapokeaji hawatuelewi tukiwaeleza masuala kama hayo, wanatulazimisha kulipa sasa suala langu lipo hapa kuwa kweli katika dini yetu nini tunachotakiwa kufanaya wakati tunakutana na matatizo kama haya tujilazimishe ki vipi hata tuweze kukabiliana na tatizo hili ninaomba mafanikio ya jibu kwa wote mimi na waislamu kwa ujumla Salam Alaikum
JIBU:
Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.
Shukrani zetu za dhati kwa muulizaji wa swali hili kuhusu kodi ambayo wafanyakazi wanafaa kulipa kwa serikali
Hakika ni kuwa kodi hizi zinafaa zitekeleze majukumu muhimu sana ya kijamii kama kujenga barabara, zahanati, utoaji wa maji na umeme, kutizama usafi wa miji, matibabu na mengineyo mengi. Lakini huduma hizi hazipatikani kabisa. Wanazuoni wa Kiislamu wamelibaini suala hili kwa kusema kuwa ni jukumu na kila Muislamu aliye na uwezo wa kutoa Zakah afanye hivyo na ni hatia kwake kutotoa kwani lengo kubwa ni kuwasaidia masikini nao waweze kujimudu kimaisha. Kwa hiyo, ikiwa Waislamu hawatatoa kutakuwa na tatizo kubwa katika jamii kama ilivyo sasa.
Katika kodi nyengine yoyote inategemea dharura ambayo ipo na ikiwepo ni wajibu wa kiongozi kuweza kuwatangazia Waislamu waweze kuchangia. Hili lilionekana wazi wakati wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika mnasaba wa matayarisho ya Vita vya Taabuk. Wakati huo dola haikuwa na uwezo wa kulidhamini jeshi, hivyo kumlazimu Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kutangaza watu wachangie katika hilo. Nao Maswahaba (Radhiya Allaahu ‘Anhum) kwa moyo mmoja na mkunjufu wakawa ni wenye kuchangia kila mmoja kwa uwezo wake.
Ama kodi ambazo zinatozwa katika nchi zetu nyingi zake ni za dhulma na hazitekelezi malengo yaliyowekwa. Muislamu anatakiwa atetee haki yake kwa njia anazoweza. Kuhusu dhulma Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Anatufahamisha:
“Msidhulumu wa msidhulumiwe” (2: 279).
Hii ni kanuni ya msingi katika Uislamu na Muislamu anafaa aitetee haki yake kwa hali na mali.
Imepokewa kwa Abu Dharr al-Ghifaariy (Radhiya Allaahu ‘Anhu) kutokana na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika aliyoyapokea kutoka kwa Mola wake Aliyetukuka kuwa Alisema: “Enyi waja Wangu, Mimi Nimejiharamishia dhulma juu ya Nafsi Yangu na nikaifanya ni haramu baina yenu basi msidhulumiane” (Muslim).
Hadiyth kuhusu mas-ala ya dhulma ni nyingi, hivyo tunatakiwa sisi tusidhulumu na serikali zifahamishwe hivyo.
Ikiwa dhulma bado inaendelea basi ni haki ya wafanyakazi kutumia mbinu zote za kuweza kuishurutisha serikali kusikia kilio chao. Miongoni mwa njia ni kama kuvieleza vyombo vya habari kuhusu suala hilo, kufanya migomo, kwenda mahakamani na njia nyingine zozote za kisheria mpaka malalamishi yenu yasikilizwe. Mara nyingi serikali hizi za dhulma huwa hazisikii yote hayo lakini ni wajibu wetu kufanya juhudi za ziada katika suala
Tukija katika suala nyeti la kuwa, je, tunafaa kuzilipa hizo kodi au hatufai? Hili ni suala ambalo inatakiwa tulitazame kwa makini. Je, kutatokea nini ikiwa hatutalipa? Jawabu yake ni kuwa ni lazima tuangalie hasara ya kutolipa na faida yake. Katika nchi hizi zetu hatua inakuwa ni kali
Kwa hiyo, ikiwa mtu anaweza kuzikwepa kodi hizo bila ya kufikiwa na mafsada (madhara) hayo tuliyoyataja atakuwa hana dhambi yoyote.
Na Allaah Anajua zaidi