Kutumia Pesa Za Riba Kulipia Kodi (tax)

SWALI:

Salaamu-llah-alaykum. Al-hamdulilaah wasalaatu wasalaam ala-ashrafil ambiyaa. Swali langu ni kuwa ribaa inajulikana wazi kuwa ni HARAAM lakini baadhi ya marafiki zangu wamedai kuwa wameulizia na kujibiwa kuwa tunaweza kujihusisha katika ribaa bila ya kula, kuvaa,kujitibia au kutumia kwa matumizi yetu ya kila siku. Je!, hayo kweli kama naishi nchi ambayo sio ya kiislamu ki-hukumu na kiuchumi wake na ninafanya biashara au ninakipato changu katika nchi hiyo na kinabidi kukatwa kodi kama ya mapato, mauzo nk. Hivyo naweza kufungua na kuweka pesa katika Saving account yenye kuzalisha ribaa ili ribaa hiyo nitakayopata niitumie tu kulipia kodi za serikali ambayo sio ya kiislamu?. Majibu katika suala hili nadhani ni neema kwa jamii ya kiislamu zinazoishi katika nchi zisizo za kiislamu

Wabillahi taufiiq

Ndugu yenu katika Uislamu

 


JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Tunashukuru kwa swali lako hilo kuhusu mas-alah haya ya ribaa ambayo yanajitokeza kila wakati japokuwa kulingana na maelezo yako ni kuwa unajua ni haramu kuzitumia pesa hizo. Kabla hatujakuja katika hilo ni vyema mwanzo tujue hukumu ya ribaa kwa uwazi zaidi.

 

Hakika ni kuwa Allaah Aliyetukuka Ameharamisha kuchukua na kutoa ribaa katika njia zake zote. Allaah Aliyetukuka Anasema: “Allaah Amehalalisha biashara na kuiharamisha ribaa” [2: 275].

 

Na Amesema tena Aliyetukuka: “Enyi Mlioamini! Mcheni Allaah, na acheni yaliyobakia katika ribaa, ikiwa mmeamini. Na kama hamtafanya hivyo, basi fahamuni mtakuwa mmetanganza vita na Allaah na Mtume Wake” [2: 278-279].

 

Na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametuambia kuwa: “Allaah Amemlaani mwenye kula ribaa, mwenye kuitoa na mashahidi wake na mwandishi wake” [Ahmad, Abu Daawuud, At-Tirmidhiy, An-Nasaaiy na Ibn Maajah].

 

Na amesema tena (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusu uovu wa ribaa: “Dirhamu ya riba anayokula mtu na huku anajua ni mbaya zaidi kuliko kuzini mara thelathini na sita” [Ahmad].

 

Amesema tena: “Ribaa ina milango 73 iliyo nyepesi na sahali ni mtu kumuoa mamake” [Al-Haakim].

Pia, “Jiepusheni na maangamivu saba… kula riba” [Al-Bukhaariy na Muslim].

 

Tufahamu kuwa Allaah Aliyetukuka Anatutaka tusisaidiane katika uovu na uadui kama Alivyosema: “Na saidianeni katika wema na taqwa, wala msisaidiane katika dhambi na uadui” [5: 2].

 

Ni ajabu kuwa ikiwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) na Mtume Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wametukataza kula ribaa kwa njia yoyote ile vipi sisi tutatoa vipengele wa kuonyesha kuwa ni halali. Watu wengi wanaishi katika nchi za kikafiri na ni ajabu kuwa wengine walikuwa wanaishi katika nchi za Waislamu lakini kwa kuona manufaa yanayopatikana ya kifedha katika nchi za kikafiri wamehamia huko.

 

Serikali hata ya Kiislamu mia kwa mia inaweza kutoza ushuru fulani ili kukidhi mahitaji ya wananchi wao. Kwa hiyo, kukataa kutoa ushuru wa kufanya biashara au kukaa kulipa kodi unaweza kukuingiza wewe katika matatizo na serikali, ima ukafungwa au ukakatazwa kufanya biashara. Hapo utakosa maslahi yako yote katika nchi hiyo. Allaah Aliyetukuka Ametukataza kujitia katika maangamivu ya aina yoyote yale. Nina hakika kuwa ikiwa wewe unaishi nchi ya Ulaya au Marekani upo wakati kabla ya ufanisi wako na kupata uraia ulikuwa unasaidiwa na serikali ili kukukimu kimaisha katika nchi hiyo ngeni nawe.

 

Kwa hiyo, ni makosa kwa Muislamu akiwa katika nchi ya Waislamu au kikafiri kuitumia ribaa kwa njia yoyote ile kama kulipa kodi ya serikali na mambo mengineyo ambayo ni faida kwako mwenyewe.

 

Tunamuomba Allaah Aliyetukuka Atuepushe kula haramu kwa njia zote zile na Atutolee badali njema zaidi katika mambo yetu, kwani yeye ni muweza wa hilo.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share