Kusaidiana Katika Kufanya Kazi Pamoja

 

SWALI

Nini hukmu ya watu kusaidiana katika kufanya kazi pamoja, na imetajwa wapi katika Qur'an ama Hadith


JIBU:

 Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola  wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Uislamu ni dini iliyokamilika kwa kila upande ikiwa ni uhusiano baina ya mja na Mola wake, au baina ya mja na familia yake, au baina ya mja na wenzake. Na umekuja na kubadilisha maovu mengi yaliyokuwa yakitendeka katika ujahiliyah (ujinga kabla ya Uislamu) na pia umerekebisha hali za watu na kuwafanya Waislamu wawe ndugu katika Uislamu, lao liwe moja katika kushirikiana, kupendana na kuoneana huruma na kusaidiana kwa hali na mali.

 

Kushikamana na kuwa na umoja katika Uislamu ni jambo ambalo Allaah سبحانه وتعالى Amelipendekeza katika Quraan na Sunnah. Anasema Allaah سبحانه وتعالى  

((وَاعْتَصِمُواْ بِحَبْلِ اللّهِ جَمِيعًا وَلاَ تَفَرَّقُوا))

((Na shikamaneni kwa Kamba ya Allaah nyote pamoja, wala msifarikiane)) [Al-'Imraan: 103]

 

Na katika Sunnah vile vile Mtume صلى الله عليه وآله وسلم amehimiza jambo la kushikamana na kushirikiana kwani Mtume

صلى الله عليه وآله وسلم amesema:

 ((Shikameni na jamaa na hadharini na kutengana. Shaytwaan yuko pamoja na aliye mpweke, naye (shaytwaan) hujitenga mbali na watu wawili. Kwa hiyo yeyote anayetaka kustarehe na raha kubwa za Peponi basi ashikilie jamaa)) [At-Trimidhiy ikiwa hadiyth hasan, sahiyh – Sunan At-Tirmidhiy 2254]

Na katika Siyrah  ya Mtume صلى الله عليه وآله وسلم  tunapata mafundisho mengi kujua jinsi Mtume صلى الله عليه وآله وسلم  na Maswahaba zake walivyokuwa wakiungana kwa hali na mali katika kutekeleza misheni au kazi fulani. Mfano katika vita vya khandaq (handaki) au kwa jina lingine vita vya Ahzaab (makundi), Maswahaba walichimba handaki kuzunguka mji wa Madiynah kutoka upande wa Mashariki. Lengo lilikuwa ni kuzuia jeshi la makafiri wasivuke kuja kupigana nao. Wote walifanya kazi mkono kwa mkono pamoja na Mtume صلى الله عليه وآله وسلم alishiriki pamoja nao katika kuchimba handaki hilo. Hii ilikuwa ni  rai aliyoitoa  Salmaan Al-Faarisiy رضي الله عنه   

Na katika kushirikiana huko, Allaah Ametuamrisha kuwa tuwe makini katika aina ya ushirikiano wetu; uwe ni ushirikiano katika mambo ya kheri na yanayomridhisha, na yasiwe ni mambo maovu ya shari na uasi. Allaah سبحانه وتعالى Anatuamrisha hivyo katika Qur-aan  

((وَتَعَاوَنُواْ عَلَى الْبرِّ وَالتَّقْوَى))  

 

((Na saidianeni katika wema na ucha Mungu)) [Al-Maaidah:2]

 

Na bila shaka kushirikiana katika kazi huleta manufaaa katika hiyo kazi kama kuimaliza kazi kwa haraka zaidi kuliko atakapoifanya mtu mmoja pekee.  Vile vile wanaposhirikiana watu katika kazi hupeana ushauri hasa panapotokea utata katika hiyo kazi na kuweza kuipanga ifanyike kwa ukamilifu na kwa umadhubuti zaidi.

 

Na Allaah Anajua zaidi.

 

Share