Khatwiyb Kukamata Fimbo Katika Khutbah Ya Ijumaa Akiwa Kwenye Minbar Imethibiti?
Je, Imethibiti Khatwiyb Kukamata Fimbo Katika Khutbah Ya Ijumaa Akiwa Kwenye Minbar?
SWALI:
Nini hukmu ya Khatibu kutegemea/kukamatia fimbo/gongo?
JIBU:
AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.
Suala hili la kubeba au kushikilia fimbo au upinde au upanga wakati Khatwiyb wa Ijumaa anatoa khutbah wamekhitalifiana Wanachuoni. Na ikhtilaaf imekuja kwa sababu Ahaadiyth zilizokuja kuhusu suala hilo, wametofautiana usahihi wake. Wengi wanakubali kuwa Ahaadiyth zake hazijathibiti. Wanaoona inafaa jambo hilo, wamesema Ahaadiyth zake zimetiliwa nguvu na zingine hadi kukubalika.
Kuna wanaoona kuwa ni jambo lenye kupendeza, nao ni Wanachuoni wa ki-Maalik, ki-Shaafi'y na ki-Hanbaliy. Na Wanachuoni wa ki-Hanafiy wanaoona ni jambo lenye kuchukiza.
Nao wanaounga mkono wametoa dalili ya Hadiyth ifuatayo:
Kutoka kwa Al-Hakam bin Hazn kuwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alisimama siku ya Ijumaa (kwenye Minbar) akiegemea fimbo au upinde, na kisha akamhimidi Allaah na kumsifu..."
[Abuu Daawuwd. Amesema An-Nawawiy katika "Al-Majmuw'" kuwa ni Hadiyth Hasan, na vilevile kasema hivyo hivyo Al-Albaaniy kwenye "Swahiyh Abiy Daawuwd", lakini Wanachuoni wengine wameidhoofisha na kusema ni Hadiyth dhaifu, na Ibn Kathiyr katika "Irshaad Al-Faqiyh" kasema isnaad yake haina nguvu.]
Anasema Imaam Ibn Al-Qayyim (Rahimahu Allaah):
"Alikuwa hachukui mkononi mwake upanga wala kisicho hicho, bali alikuwa akiegemea upinde au fimbo kabla hajaingia kwenye Minbar. Na alikuwa vitani akiegemea upinde. Na katika Ijumaa akiegemea fimbo, na hakuna kilichohifadhiwa kutoka kwake kuwa akiegemea upanga, na wanayodhania baadhi ya wajinga kuwa alikuwa daima akiegemea upanga, na kwamba hiyo ni ishara kuwa Dini ilisimama kwa upanga. Huo ni ujahili uliopindukia (kwa anayedhania hivyo.
Na hakujahifadhiwa kutoka kwake kuwa baada ya kutoka Minbarini, alikuwa akipanda kwa kutegemea upanga au upinde, au chochote kingine, na wala kabla ya kupanda Minbarini hakuwa akichukua upanga katu. Bali alikuwa akiegemea juu ya fimbo au upinde (katika nyakati zingine)."
[Zaadu Al-Ma'aad, mj. 1, uk. 429]
Katika maneno ya Imaam Ibn Al-Qayyim (Rahimahu Allaah), anaonyesha kuwa haukuwa mwenendo wa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuegemea juu ya fimbo au chochote kwenye Khutbah ya Ijumaa akiwa Minbarini.
Na amesema Imaam Ibn 'Uthaymiyn (Rahimahu Allaah) akisherehesha:
"Kauli yake: "Akiegemea juu ya upanga au upinde au fimbo", maana yake: inasuniwa kuegemea wakati wa Khutbah juu ya upanga au upinde au fimbo. Na wakatolea dalili ya Hadiyth inayosimuliwa kutoka kwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ambayo usahihi wake una walakini. Na tukikadiria usahihi wake, amesema Ibn Al-Qayyim: Hakujahifadhiwa kutoka kwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) baada ya kupanda kwake Minbar kuwa alikuwa akiegemea juu ya chochote.
Na katika wajihi wa hilo, kwamba kuegemea kunakuwa kwa ajili ya mahitajio; ikiwa Khatwiyb atahitajia kuegemea juu ya kitu, mfano ni mtu dhaifu anahitaji fimbo kuegemea juu yake, basi itakuwa ni Sunnah, kwa sababu hiyo inamsaidia yeye kusimama ambako huko kusimama ni Sunnah. Na kinachosaidia katika Sunnah nacho ni Sunnah.
Ama ikiwa hakuna mahitajio ya hilo, basi hakuna haja ya kubeba fimbo."
[Ash-Sharh Al-Mumti', mj. 5, uk. 62-63]
Na ameliunga mkono Imaam Al-Albaaniy (Rahimahu Allaah) maneno ya Imaam Ibn Al-Qayyim (Rahimahu Allaah), na amekataa kuwa kumethibiti katika Ahaadiyth lenye kujulisha kuwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipokuwa akikhutubu juu ya Minbar alikuwa akiegemea upinde au fimbo. Kayaeleza hayo kwenye "As-Silsilatu Al-Ahaadiyth Adhw-Dhwa'iyfah, Hadiyth namba 964]
Kadhalika katika Fatwa nyingine ya Imaam Ibn 'Uthaymiyn (Rahimahu Allaah) amesema:
"Akihitaji kufanya hivyo kutokana na kuwa yeye ni dhaifu (anahitaji kitu cha kuegemea) basi ni Sunnah kwa sababu kusimama ni Sunnah kwani kinachosaidia Sunnah basi ni Sunnah. Ama ikiwa hakuna haja ya kukamata fimbo basi hakuna haja ya kukamata."
[Majmuw’ Fataawa wa Rasaail, Al-Mujallad 16, Baabu Swalaatil-Jumu’ah]
Na Allaah ni Mjuzi zaidi.