Bubu, Kiziwi Au Kipofu Wanafaa Kuwa Imaam Kuswalisha Watu?
Je, Bubu, Kiziwi Au Kipofu Wanafaa Kuwa Imaam Kuswalisha Watu?
SWALI:
Assalaam alaykum.....Hv bubu anaweza kuswalisha ikiwa hakuna mjuzi??
Swali jingine: Kipofu au kiziwi wanaweza kuwaswalisha watu?
JIBU:
AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.
Wa ‘Alaykumus Salaam wa RahmatuLLaahi wa Barakaatuh
Haifai kwa bubu kuswalisha wenye kuzungumza. Haya ni kwa mujibu wa Ahlul-'Ilm na ndio msimamo wa madhehebu zote nne za Ahlus-Sunnah.
Sababu mojawapo kubwa waliyoieleza ni kuwa bubu hatoweza kutekeleza baadhi ya nguzo za Swalaah kama Takbiyrah ya Ihraam na Kisomo cha Suwratul-Faatihah.
Lakini Ahlul-'Ilm wanasema bubu anaweza kuwaswalisha mabubu wenzake wakiwa wao wenyewe na kukiwa hakuna mwenye kuweza kuzungumza baina yao, kutokana na wao vilevile kuwa na hali moja kimaumbile na yeye.
Ama kipofu hakuna makatazo kuswalisha, na imethibiti ‘Abdullaah bin Ummi Maktuwm (Radhwiya Allaahu ‘anhu) aliwaswalisha Maswahaba (Radhwiya Allaahu ‘anhum) hali ya kuwa alikuwa kipofu, kama ilivyosimuliwa na Anas (Radhwiya Allaahu ‘anhu) na kukusanywa na Imaam Ahmad (Rahimahu Allaah) katika Musnad yake.
Ama kiziwi, usahihi anaruhusika kuswalisha kutokana na kuwa anaweza kutekeleza nguzo za Swalaah kama kusoma Qur-aan, Suwratul-Faatihah na Takbiyrah ya Ihraam. Ingawa kuna baadhi ya Wanachuoni wanaona ni makruhu kwa kiziwi kuswalisha kutokana na kutoweza kusikia Maamuma wakimsahihisha kwa kumwambia “Subhaana Allaah” pindi atakapokosea jambo katika Swalaah.
Na Allaah Anajua zaidi