Kwa Nini Swalaah Ya Adhuhuri Na Alasiri Hazisomwi Kwa Sauti?

SWALI:

 

A.A. INSHAALLAH MUNGU ATATUPA TAWFIQ NA MWELEKEO MWEMA. NIMEULIZWA SANA SWALA HILI KWA NINI SWALA YA ADHUHURI NA ALASIRI IMAMU HASOMI ALHAMDU KWA SAUTI.


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Kwanza kabla hatujajibu swali lako, tunakukumbusha kuwa unapoandika jina la Allaah au Mtume, usifupishe mbele yake kwa kuweka (S.W.) au (S.A.W.) kama ilivyozoelekea na wengi, bali andika kwa kirefu maneno hayo bila ya kuyafupisha. Andika (Subhaanahu wa Ta'ala) baada ya kumtaja Allaah, na andika Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) au (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) baada ya kumtaja Mtume. Hivyo ndivyo inavyopaswa, na ndio heshima zaidi na utukufu na ndivyo inavyotamkwa na si kama inavyofupishwa na wengi kimazoea au kivivu. Pia hiyo ni ibada, na ibada inatakiwa ifanywe kwa namna iliyofundishwa na haifai kugeuza, kuongeza au kupunguza. Hali kadhalika Maswahaba walikuwa wakiandikiana barua na hakuna aliyekuwa akikatisha Salaam, wala kumswalia Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) wala kumtukuza Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) kwenye barua zao. Tuige na tufuate nyendo zao tusalimike.

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kuswali kimya kimya katika Swalah ya Adhuhuri na Alasiri. Hili ni swali ambalo linajitokeza mara kwa mara na huwa linaulizwa ili Muislamu apate utulivu kwa lile lenye kumkera moyoni mwake.

 

Sababu kubwa inayotolewa katika kusomwa kimya katika Swalah hizo mbili ni kuwa Waislamu walikuwa na hofu wakati wa mchana wasije wakasikika na makafiri wa Kiquraysh na hivyo kuteswa na kuadhibiwa. Hata hivyo, ukilitizama suala hili kwa makini na utulivu wa moyo sababu hiyo haingii kabisa kwani Swalah ilifaradhishwa baada ya Israa’ na Mi‘raaj wakati ambalo ulinganizi wa siri ulikuwa ushakwisha na Waislamu walikuwa wanaswali hata kwenye al-Ka‘bah. Tufahamu kuwa Israa’ ilifanyika miezi kama 16 kabla ya kuhama kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Maswahaba zake Madiynah. Hata hivyo, pia haingii katika mantiki kwani ikiwa ni uwoga basi hali hiyo ingebadilishwa baada ya kuhama Madiynah kwani huko dola ya Kiislamu ilianzishwa na hofu ikawa haipo tena.

 

Sababu kubwa ya hilo ni kufuata mwendo wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), kwani Allaah Aliyetukuka Ametuambia:

 

Sema: Ikiwa nyinyi mnampenda Allaah basi nifuateni mimi, Allaah Atakupendeni na Atakufutieni madhambi yenu” (3: 31).

Pia,

 

Na anachokupeni Mtume chukueni, na anachokukatazeni jiepusheni nacho. Na mcheni Allaah” (59: 7).

 

Na zipo Aayah nyingi zinazotuamrisha kumfuata Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kufuata aliyokuja nayo. Ama Hadiyth ni ile inayosema:

 

Swalini kama mlivyoniona nikiswali” (al-Bukhaariy).

 

Baada ya kuelewa kanuni hizo basi matatizo yote yameondoka na huwa Muislamu hana tatizo tena kuhusu suala hilo na mengine kama hayo.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share