Vipi Kukidhi Swalaah Kama Shida Kuswali Kazini?

 

 

SWALI:

Asalam aleykum.

Samahani kama nilivyotuma haikuwa hivyo, mimi niliona nitume pamoja kwa kuwa yote yalikuwa yanahusu sala.

Mimi natoka nyumbani saa moja na nusu asubuhi baada ya kusali subhi, nakwenda kazini, narudi saa kumi na moja na nusu, swala ya dhuhuri na Asri zinanikuta kazini, je baada ya kufika nyumbani naweza kuzisali hizi  ambazo sikuweza kuzisali kwa wakati wake? kwa sababu kazini sipati muda wa kusali na sehemu ya kusalia pia hakuna, sasa nifanyeje ili niweze kuzisali hizi sala ambazo zimenipita?

Mungu awabariki katika kazi hii ngumu


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah (Subhaana wa Ta'aala) Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allahu 'anhum jamiy'an) na watangu wema mpaka Siku ya Qiyaamah.

Kuswali kwa wakati wake ni jambo Aliloliamrisha Allaah (Subhaana wa Ta'aala) kama Anavyosema:

َ (( إِنَّ الصَّلاَةَ كَانَتْ عَلَى الْمُؤْمِنِينَ كِتَابًا مَّوْقُوتًا))

((Kwani hakika Swalah kwa Waumini ni faradhi iliyo wekewa nyakati maalumu))) [An-Nisaa:103]

Na ndio maana hata mtu anapokuwa katika hali ya ugonjwa anatakiwa aswali japo kwa kukaa au kwa kulala kwa jinsi ilivyo muhimu kutimiza Swalah kwa wakati wake.

Hivyo Muislamu inampasa afanye kila juhudi aweze kutimiza Swalah zake kwa kuswali kila kipindi cha Swalah kinapowadia hata kama yuko kazini au hata kama yumo safarini, mfano katika basi au treni na anakhofu kuwa atakapofika anakoelekea, wakati utakuwa umeshatoweka.

Bila shaka kazini utakuwa unao muda wa kupumzika, hivyo ni bora kuutumia kwa kutimiza ibada yako ya fardhi. Na kupata wakati kazini hatudhani kama ni shida kokote ulipo haswa ikiwa ni nchi za Kiislamu. Na hata nchi za kikafiri, inavyojulikana kuwa kuna haki za kupewa wakati wa kuswali na hata sehemu nyingine Waislam wanatengewa sehemu ya kuswalia. Ni juhudi ya mtu binafsi kuuliza, kuomba ili apewe haki yake. Na ikiwa hapatiwi haki yake hiyo basi hadi kuna uwezekano wa kupeleka malalamiko yake kwa vyama vya wafanyakazi makazini au kwa wanasheria (Lawyers). Mfano nchi za Amerika ya Kaskazini wako ndugu zetu wa Kiislamu wanaogombania haki kama hizo nao wanajulikana kama CAIRCAN. Kwa faida ya wanaoishi nchi hizo wanaweza kuingia katika kiungo kifuatacho kuweza kuwasiliana nao kwa matatizo yoyote yanayohusiana na dini yao:  

http://www.caircan.ca/  (CANADA)

http://www.cair-net.org/  (USA)

Ikiwa umeshindwa baada ya juhudi zote kupata kuswali Swalah zako kwa wakati, basi utaweza kupata ruhusa ya kuunga Swalah ya Adhuhuri na Alasiri; ambazo zitakuwa ni Jam'u taqdiym (Kuswali  Adhuhuri na Alasiri wakati wa Adhuhuri), au ukachelewesha  Jam'u taakhiyr (Kuswali  Adhuhuri na Alasiri wakati wa Alasiri). Zote utaziswali kikamilifu yaani Rakaa nne za Adhuhuri na Rakaa nne za Alasiri. Hii ni kutokana na dalili ya Hadiyth ifuatayo:

عن ابن عباس رضي الله عنهما  قال : صلَّى رسول الله صلى الله عليه وسلم الظهر والعصر جميعا بالمدينة في غير خوف ولا سفر ، قال أبو الزبير : فسألت سعيداً – أي : ابن جبير - لم فعل ذلك ؟ فقال : سألت ابن عباس كما سألتني فقال : أراد أن لا يحرج أحداً من أمَّته  ( مسلم)  

Imetoka kwa ibn 'Abbas (Radhiya Allahu 'anhumaa) ambaye amesema: "Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliswali (Swalah ya) Adhuhuri na Alasiri pamoja alipoikuwa Madiynah wakati hakukuwa na khofu wala hakuwa katika safari". Akasema Abu Az-Zubayr: "Nikamuuliza Sa'iyd (yaani ibn Jubayr) kwa nini alifanya hivyo?" Akasema: "Nilimuuliza ibn 'Abbaas swali hilo hilo na akasema: "Hakutaka mtu yeyote katika Ummah wake apate shida" [Muslim]

Lakini jaribu sana isiwe ni mazoea ya kila siku kufanya hivyo ujitahidi uwezavyo kuswali kila Swalah kwa wakati wake.

Na Allah Anajua zaidi

 

 

 

Share