047-Aayah Na Mafunzo: Mukhtasari Wa Historia Ya Mayahudi Kuhusu Kuasi Kwao
Aayah Na Mafunzo
An-Nisaa
Mukhtasari Wa Historia Ya Mayahudi Kuhusu Kuasi Kwao
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ أُوتُوا الْكِتَابَ آمِنُوا بِمَا نَزَّلْنَا مُصَدِّقًا لِّمَا مَعَكُم مِّن قَبْلِ أَن نَّطْمِسَ وُجُوهًا فَنَرُدَّهَا عَلَىٰ أَدْبَارِهَا أَوْ نَلْعَنَهُمْ كَمَا لَعَنَّا أَصْحَابَ السَّبْتِ ۚ وَكَانَ أَمْرُ اللَّـهِ مَفْعُولًا ﴿٤٧﴾
47. Enyi mliopewa Kitabu! Aminini yale Tuliyoyateremsha (kwa Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) yanayosadikisha yale mliyonayo, kabla hatujabadilisha nyuso Tukazirudisha kisogoni, au Tukawalaani kama Tulivyowalaani watu wa As-Sabt. Na amri ya Allaah ni ya kufanyika tu.
Mafunzo:
Ifahamu historia ya Mayahudi kwa mukhtasari namna walivyokuwa jeuri kwa Manabii wao: Mayahudi walikatazwa na Allaah (سبحانه وتعالى) kuvua samaki siku ya As-Sabt (Jumamosi) lakini wao kwa ujeuri wao wakavua samaki siku hiyo na kwa kutumia hila. Pia Allaah (سبحانه وتعالى) Akawakumbusha wajukuu zao kuhusu siku hiyo ya As-Sabt (Jumamosi) ambayo babu zao Mayahudi waliasi ndani yake kiasi kwamba Allaah (سبحانه وتعالى) Aliwageuza kuwa nyani na nguruwe. Na mwenye kusoma visa vya Mayahudi dhidi ya Manabii wao na miongoni mwa swaalihiyna katika wao, atakuta kuwa waliwaudhi mno Manabii wao na wakawapinga na kwenda kinyume nao. Na pia wakafanyia inadi na ujeuri maamrisho ya Allaah (سبحانه وتعالى) na wakawa na ujeuri uliopindukia. Miongoni mwa mifano ya hayo ni; kisa cha ng’ombe na ndama. Pia kutaka kwao kumuona Allaah (سبحانه وتعالى) wazi wazi. Tena hayo wameyafanya baada tu ya kuvukishwa bahari kwa salama na kuokolewa kutona na adui yao Fir-‘awn aliyezamishwa baharini. Pia uasi wao kuwaua baadhi ya Manabii bila ya haki. Na mifano mingine mingi kuhusu uasi na ujeuri wa Mayahudi.