019-Asbaabun-Nuzuwl: An-Nisaa Aayah 019: يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا يَحِلُّ لَكُمْ أَن تَرِثُوا النِّسَاءَ كَرْهًا
أسْبابُ النُّزُول
Asbaabun-Nuzuwl
Sababu Za Kuteremshwa (Baadhi Ya Aayaat Za Qur-aan)
Imekusanywa na: Alhidaaya.com
An-Nisaa 019-Enyi walioamini! Si halali kwenu kurithi wanawake kwa kuwakirihisha
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا يَحِلُّ لَكُمْ أَن تَرِثُوا النِّسَاءَ كَرْهًا ۖ وَلَا تَعْضُلُوهُنَّ لِتَذْهَبُوا بِبَعْضِ مَا آتَيْتُمُوهُنَّ إِلَّا أَن يَأْتِينَ بِفَاحِشَةٍ مُّبَيِّنَةٍ ۚ وَعَاشِرُوهُنَّ بِالْمَعْرُوفِ ۚ فَإِن كَرِهْتُمُوهُنَّ فَعَسَىٰ أَن تَكْرَهُوا شَيْئًا وَيَجْعَلَ اللَّـهُ فِيهِ خَيْرًا كَثِيرًا ﴿١٩﴾
19. Enyi walioamini! Si halali kwenu kurithi wanawake kwa kuwalazimisha. Na wala msiwazuie kwa inda ili mpokonye baadhi ya vile mlivyowapa isipokuwa wakiwa wamefanya uchafu bayana. Na kaeni nao kwa wema. Na mkiwachukia, basi asaa ikiwa mnachukia jambo na Allaah Akalijaalia kuwa lenye khayr nyingi ndani yake.
Sababun-Nuzuwl:
Walikuwa Waarabu zama za Jaahiliyyah pindi anapokufa mwanaume na akaacha mke, basi wale ndugu wa mume wake wanakuwa na haki zaidi kwa mwanamke, na baadhi yao wakitaka wanamuoa, na wakitaka wanamuozesha, na wakitaka hawamuozeshi, na wao wanakuwa wana haki naye zaidi kuliko hata ndugu zake mwanamke na wazazi wake. Ndipo Allaah (عزّ وجلّ) Akateremsha Aayah hii. [Amehadithia Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما) na imepokelewa na Al-Bukhaary]